Tuesday, January 10, 2012

ZITTO AIMBA SERIKALI KUPUNGUZA MATUMIZI YA POSHO NA SIYO MATUMIZI YA RELI, BARABARA, ELIMU NA AFYA

                                     MPANGO WA SERIKALI KUPUNGUZA MATUMIZI

Mwezi Disemba mwaka 2011 Waziri wa Fedha na Uchumi alimwandikia barua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) kumwahidi mambo yepi Serikali ya Tanzania itafanya ili kurekebisha Bajeti yake. Utaratibu huu hufanyika kila mwaka kupitia mpango unaoitwa ‘Policy Support Instrument (PSI).
Katika barua hiyo Waziri wa Fedha wa Tanzania ameahidi kwamba Serikali itafanya juhudi kupunguza matumizi ili kuweza kupunguza uwiano wa nakisi ya Bajeti na Pato la Taifa (fiscal deficit to GDP ratio) kutoka asilimia 7.2 mpaka asilimia 6.6 ya Pato la Taifa.


Waziri wa Fedha na Uchumi ameiambia IMF kwamba ifikapo mwisho wa Mwezi Disemba mwaka 2011 (wiki mbili zilizopita) Baraza la Mawaziri la Tanzania limefikia maamuzi ya kupunguza nakisi ya Bajeti kwa kiwango kilichotajwa. Maeneo yanayotajwa ni Pamoja na Miradi ya Maendeleo ambapo jumla ya miradi yenye thamani ya Tshs 157bn itakatwa. Waziri wa Fedha ametaja miradi hiyo katika Ukarabati na Ujenzi wa Miundombinu.


Kambi ya Upinzani Bungeni inapinga kuondolewa kwa miradi ya maendeleo ili kupunguza matumizi ya Serikali. Kimsingi wakati kama huu ambapo hali ya uchumi ni mbaya na vijana wengi vijijini na mijini hawana ajira tunasisitiza umuhimu wa kutumia zaidi kwenye miradi ya maendeleo.
                             Punguza matumizi ya kawaida
Kambi ya Upinzani Bungeni inarejea wito wake kwa Serikali kupunguza matumizi ya kawaida ili kupata fedha za kutosha kwa ajili ya maendeleo. Haiwezekani kamwe tukawa Taifa huru iwapo miradi yetu yote ya maendeleo inafadhiliwa na wahisani.

Kiwango kidogo tulichokiweka katika Bajeti ya mwaka huu ndicho hicho sasa kinakatwa na hivyo miradi yote ya maendeleo kubakia kwa wahisani ama kwa mikopo au misaada. Kiwango cha Tshs 203bn sawa na 0.5% ya Pato la Taifa ambacho Serikali imeahidi kupunguza ni kidogo mno na kinalenga kuumiza watumishi wa kada ya chini ya Serikali na sio viongozi wakubwa.

Bajeti ya Mafunzo inayoenda kukatwa itaumiza Manesi na Walimu au watumishi wanaoongeza ujuzi ili kuboresha kazi zao. Serikali ikate matumizi yote yasiyo ya lazima na hasa posho (360bn), ipunguze matumizi ya magari na yale yasiyo na uhitaji yapigwe mnada na viongozi wote isipokuwa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika na Jaji Mkuu washushwe madaraja ya kusafiria kwenye ndege. Safari zote ambazo hazina mahusiano na miradi ya maendeleo zipigwe marufuku kwa muda wote wa miezi sita ya Bajeti iliyobakia.


Serikali ihakikishe matumizi katika Sekta ya Elimu na Afya hayakatwi kabisa ili kuhakikisha tunalinda mafanikio kiduchu ya upanuzi wa sekta hizi na kuongeza uwezo wa Serikali kutoa huduma bora kwa wananchi hasa wa vijijini.
              Matumizi ya Maendeleo yasiguswe, yaongezwe
Tayari imeonekana kwamba katika kipindi chote cha nusu ya Bajeti Halmashauri za Wilaya hazijapata fedha za maendeleo. Mfano Halmashauri ya Wilaya Kigoma imepata asilimia 0.3 tu ya Bajeti ya Maendeleo ilhali Halmashauri ya Mji wa Mpanda imepata asilimia 4 tu.

Ni dhahiri miradi ya maendeleo kwa maeneo mengi ya vijijini itakwama kwani ni wazi kabisa kwamba Halmashauri hazipati fedha zote za Bajeti ya Maendeleo. Serikali itambue kwamba miradi ya maendeleo sio anasa bali ndio vyanzo vya baadaye vya mapato ya serikali. Miradi ya maendeleo hutoa ajira kwa wananchi na hivyo kuwapunguzia umasikini wa kipato.

Jumla ya Tshs 157bn zinazotakiwa kukatwa zisikatwe bali ziongezwe ili kupata fedha za kurekebisha miundombinu kama Reli ya Kati.Kwa mfano Reli ya Kati inahitaji Tshs 200bn katika kipindi cha miaka 3 ili iweze kusafirisha mizigo tani 1.5m kwa mwaka kila siku na kuzalisha faida.
                            Ongeza Mapato ya Ndani
Inashangaza kwamba katika mpango wa Serikali kupunguza nakisi ya Bajeti mkazo umewekwa kwenye kuondoa miradi ya maendeleo badala ya kuongeza mapato. Nakisi hupunguzwa ama kwa kupunguza matumizi au kwa kuongeza Mapato. Serikali katika Taarifa yake kwa IMF imeibua njia moja tu ya kuongeza mapato, kodi ya mapato kutoka Kampuni ya Geita Goldmine. Huu ni uvivu wa kufikiri.


Serikali imeambiwa mara kadhaa suala la kuanza kutumika kwa sheria mpya ya madini kwa Kampuni za Madini zilizokuwapo. Makusanyo ya Mrahaba peke yake kwa sheria mpya, kiwango kipya na kanuni mpya ya kukokotoa ingeongeza mrahaba mpaka Tshs 203bn kutoka Tshs 99bn za sasa. Kwanini Serikali ianvuta miguu katika kutekeleza hili? Waziri wa Nishati na Madini aliahidi Bungeni kwamba mazungumzo na Kampuni za Madini yanaisha Mwezi Septemba. Mbona Serikali imekuwa BUBU katika hili?


Serikali iliahidi kuangalia suala la mauzo ya mali za makampuni zilizoko Tanzania na kodi ambayo tunapaswa kukusanya, Serikali imekuwa kimya kabisa katika suala hili. Marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa kuondoa msamaha kwenye ‘deemed capital goods yangeongeza mapato ya Serikali kwa kiwango kikubwa na kupunguza mzigo wa misamaha ya Kodi.

                                  Uwajibikaji kwa Bunge
Inashangaza zaidi kwamba sasa imekuwa ni mtindo kwa Serikali kutoa ‘commitments’ muhimu za kibajeti kwa Shirika la IMF badala ya wananchi kupitia Bunge. Bunge limepitisha Bajeti, mapitio yeyote ya Bajeti yanapaswa kuidhinishwa na Bunge. Bila kufanya hivyo maana ya Bunge kupitisha Bajeti inakuwa haina mantiki na uhuru wa Taifa letu unakuwa haupo kwetu.


Umuhimu wa Bunge kutunga haraka Sheria ya Ofisi ya Bajeti ya Bunge (Parliamentary Budget Act) sasa unaonekana waziwazi. Muswada umewasilishwa Bungeni na Wabunge binafsi kutaka kuundwa kwa mfumo wa kuisimamia Serikali katika Bajeti. Ofisi ya Spika wa Bunge ihakikishe muswada huu unachapishwa katika Gazeti la Serikali mara moja ili usomwe kwa mara ya kwanza katika mkutano wa Sita wa Bunge na kutungwa kuwa sheria katika mkutano wa Saba.


Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali ilete mpango wa kupunguza matumizi Bungeni ili ujadiliwe na kuidhinishwa na Bunge kabla ya kuanza kutumika. Vinginevyo Mpango wa Serikali kwa IMF utakuwa ni kudharau wananchi na kuuza uhuru wetu kwa Shirika la Fedha la Kimataifa. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema mwishoni mwa miaka ya Sabini ‘toka lini Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limekuwa Wizara ya Fedha ya Kimataifa (International Ministry of Finance)?’

Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Waziri Kivuli Fedha na Uchumi
Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni (NKUB)
Dar es Salaam, 10 Januari 2012.

No comments:

Post a Comment