Wednesday, August 3, 2011

MAREKANI YALEGEZA VIKWAZO KURUHUSU MISAADA KWENDA SOMALIA!

Misaada ikishushwa Mogadishu Serikali ya Marekani imetangaza kulegeza baadhi ya vikwazo vyake kwa kuruhusu mashirika ya misaada kupeleka misaada hiyo kwenye maeneo yanayodhibitiwa na kundi la Al Shabaab.
Hatua hiyo ina maana kuwa mashirika ya kujitolea hayatokabiliwa na hatua za kisheria dhidi yao kwa kupeleka misaada kwenye maeneo hayo. Hata hivyo vikwazo dhidi ya wale wanaojiita wababe wa vita vinaendelea kubakia.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Mark Toner amesema nchi yake kuanzia sasa itayapatia vibali na kandarasi mashirika hayo ya kujitolea hata kama kwa bahati mbaya misaada hiyo itaangukia katika mikono ya wanamgambo wa Al Shaabab.


Wanamgambo wa Al Shaabab wanadhibiti eneo kubwa la kusini na katikati mwa Somalia maeneo ambayo ndiyo yaliyoathiriwa zaidi na ukame uliyosababisha njaa.


Mwaka 2008 Marekani ililiwekea vikwazo kundi hilo la Al Shaabab na kutangaza kuwa ni kosa la uhaini kwa yoyote atakayelipatia msaada wowote kundi hilo. Marekani imesema vikwazo hivyo vya mwaka 2008 havina nia ya kuathiri shughuli za makundi ya misaada.

No comments:

Post a Comment