Jeshi la Polisi nchini limeombwa kuwahamisha kazi mara moja askari sita wanaodaiwa kuwanyanyasa wakuu wa Polisi wa Wilaya wanaohamishiwa katika mkoa wa Geita kutokana na uhusiano waliojijengea na baadhi ya watu wakiwemo wafanyabiashara wakubwa kutokana na kukaa katika eneo hilo kwa muda mrefu.
Akichangia hoja ya Makadirio ya Matumizi ya Ofisi ya Rais, Bungeni mjini Dodoma Mbunge wa Mkanyageni (CUF) MOHAMED HABIB MNYAA amesema askari hao sita wamekuwa kama miungu watu wanaoweza kuwaamrisha wakuu wao wa kazi ili kutimiza matakwa yao binafsi.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa HABIB MNYAA ameiomba Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma kuhakikisha askari hao wanahamishwa kutoka kituo hicho cha kazi ili kutekeleza malengo ya Mkataba wa Utawala bora kazini unaotaka mfanyakazi asikae kwenye kituo kimoja zaidi ya miaka 20.
Usalama wa Taifa kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa TAKUKURU wameomba kuchungusa ufisadi mkubwa wa urasimishaji ardhi uliofanywa na Kampuni ya Twiga Chemical Industial Limited na serikali kutakiwa shilingi bilioni tatu kama fidia ya kazi hiyo.
Mbunge wa Ubungo (Chadema) JOHN MNYIKA amesema fidia hiyo ya mazingira yasiyoeleweka imeainisha wananchi wa Kimara Baruti walio katika eneo la ekari nane waondolewe jambo ambalo ni kinyume na maamuzi ya Kamati ya deni la Taifa yaliyotolewa mwaka 2006.
Katika bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012 Kampuni hiyo ya Twiga Chemical Industial Limited imetengewa tena jumla ya shilingi Bilioni nne nukta tano kama fidia ya mazingira yasiyoeleweka.
Watendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini TAKUKURU wameonywa kwamba taasisi hiyo haikuundwa kwa ajili ya wanasiasa na vigogo na badala yake ipo kwa ajili ya kutetea maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.
MICHAEL LAIZER Mbunge wa Longido (CCM) amesema Bungeni Mjini Dodoma kwamba ingawa kuna ufujaji mkubwa wa fedha za miradi ya TASAF, Halmashauri, Manunuzi na Miradi hafifu lakini watendaji wa taasisi hiyo wamekuwa hawafuatilii kwa kina ubadhirifu huo.
Kutokana na hayo Mheshimiwa LAIZER amewaasa watendaji wa TAKUKURU kutojihusisha na vitendo vya kupokea rushwa ili kutouweka rehani usalama wa taifa.
Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara imewaagiza Mawakala wa vipimo nchini kwa kushirikiana na vyombo vya dola kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria wafanyabiashara wezi wanaowaibia wakulima wa pamba kwa kutumia mizani ya rula.
Akiwasilisha kauli za Mawaziri Bungeni mjini Dodoma Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara LAZARO NYALANDU amesema ingawa serikali iliruhusu matumizi ya mizani hiyo, imechukua hatua hiyo kudhibiti vitendo vya unyonyaji vinavyofanywa dhidi ya wakulima wa pamba.
Katika hatua nyingine Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara zitashirikiana katika mchakato wa kufanya tathimini ya mizani itakayotumika katika upimaji wa pamba katika msimu ujao.
No comments:
Post a Comment