Wednesday, May 11, 2011

NYUMBA 1748 ZA WAATHIRIKA WA MABOMU GONGOLAMBOTO KUKARABATIWA!

SAIDI MECK SADIKI akipokea baadhi ya misaada kwa ajili ya waathirika wa mabomu!
                         Moja ya nyumba iliyoathiriwa na milipuko ya mabomu Gongolamboto
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, BWANA SAIDI MECK SADIKI, amesema Serikali inatarajia kukarabati nyumba 1748 zilizothibitika kuwa zimeharibiwa na pia imetenga eneo la Kinyerezi kwaajili ya ujenzi wa nyumba 77 ambazo zimethibitika kuwa zimebomolewa kabisa na milipuko hiyo.

Ameongeza kuwa milipuko hiyo imegharimu maisha ya watu 30 na kujeruhi watu 600 na kwamba wengi wao wamesharuhusiwa na walioko hospitalini mpaka sasa ni majeruhi wanne.
Hivyo jumla zaidi ya bilioni moja zinatarajiwa kutumika katika ujenzi na ukarabati wa makazi ya waathirika wa milipuko ya mabomu katika Kambi ya Jeshi iliyoko Gongo la Mboto, Jijini Dar es salaam, huku zaidi ya milioni 130,zikiwa zimeshatumika kwa waathirika wa milipuko hiyo mpaka sasa.
Wakati huo huo Mkoa wa Dar es salaam unatazamiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 27 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa ( ALAT), ambao umepangwa kufanyika Mei 14 mwaka huu hapa jijini.
Sadiki amesema miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kujadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na kupitisha makisio ya mapato na matumizi ya jumuiya hiyo katika kipindi cha mwaka 2010/ 2011 sanjari na kupokea na kujadili mada mbalimbali zitakazowasilishwa na Wizara, Idara pamoja na wakala wa Serikali nchini.
Ameongeza kuwa Mkutano huo unatarajiwa kufunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, MIZENGO PINDA na kwamba kufanyika kwa mkutano huo Jijini Dar es salaam kutatoa fursa kwa Wafanyabiashara, Sekta binafsi, taasisi na vyama visivyo vya Serikali kuweza kujitangaza kibiashara.

No comments:

Post a Comment