Bw. Donatius Kamamba, Mkurugenzi wa Mambo ya Kale katika Wizara ya Maliasili na Utalii , ameteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirika la Kimaifa lisilo la Kiserikali liitwalo The International Council on Monuments and Sites - ICOMOS” kwa kipindi cha miaka mitatu (3) hadi Novemba, 2014. Uteuzi huo ulifanywa na Gustavo Araoz, Rais wa ICOMOS tarehe 3 Julai, 2012.
ICOMOS ni Shirika la Kimataifa lisilo la kiserikali lenye jumla la nchi wanachama 98. Majukumu yake ni pamoja na kutoa ushauri kwa UNESCO kuhusu Uhifadhi wa Urithi wa Utamaduni na hufanya tathmini ya maeneo yanayopendekezwa kuingizwa kwenye Orodha ya Urithi wa Utamaduni - World Heritage Sites. Aidha, ICOMOS inalo jukumu la kutathmini shughuli za uhifadhi zinavyotekelezwa katika maeneo ambayo tayari yapo katika Orodha ya Urithi wa Utamaduni.
Kuteuliwa Bw. Donatius Kamamba kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya ICOMOS ni ishara kuwaTanzania inayo taaluma katika fani ya Uhifadhi wa Urithi wa Utamaduni na inayatunza vizuri maeneo husika yaliyoko nchini. Maeneo hayo ambayo ni vivutio vya utalii ni kama vile: Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songomnara, Michoro ya miambani ya Kondoa, Eneo la Bonde la Oldupai, Nyayo za Zamadamu zilizoko Letoli, Miji ya Kihistoria ya Pangani, Kilwa Kivinje na Mikindani, Majengo ya kihistoria ya Ikulu , Maboma ya Kijerumani ya Biharamlo na Mahenge na Njia ya Kati ya biashara ya Utumwa.
Aidha Bwana Kamamba anazo nyadhifa nyingine za kimataifa. Mwaka 2007 alichaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Uongozi wa Kituo cha Kimataifa cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Urithi wa Rasimali za Utamaduni (International Centre for the Study of Preservation and Restoration of Cultural Property - ICCROM), kilichopo Roma, Italia. Pia mwaka jana Novemba, 2011, aliteuliwa kuwa Rais wa nchi wanachama wa ICCROM kwa kipindi cha miaka miwili Novemba ,2001 mpaka Novemba, 2013.
No comments:
Post a Comment