Na Andrew Chale
MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Farid Kubanda, maarufu kama FID Q ni miongoni mwa nyota wa muziki huo waliocheza filamu ya Machweo iliyozinduliwa usiku wa kuakia jana ndani ya New Maisha Club jijini Dar es Salaam ambayo inazungumzia maisha halisi ya wasanii wa muziki huo nchini.
Katika uzinduzi huo, wasanii hao pia waliweza kupiga shoo kali na ya aina yake huku Fd Q na Snare walipagawisha mashabiki waliofurika ndani ya ukumbi huo huku Fid Q akipagawisha zaidi ya saa moja na nusu na kukonga mashabiki walioacha viti na kucheza nao kwa muda.
Filamu hiyo imetayarishwa na kampuni ya Bonta Arts Production kwa ushirikiano na kampuni ya Event World. Nyota wengineo waliomo kwenye filamu hiyo ni pamoja na Steve RnB, Snare, Suka, Abby Skyles, Tatyana, Buff G na Victoria na itaingia sokoni baada ya kufanyika uzinduzi kwenye Ukumbi wa Dar Live hivi karibuni.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Bonta Production, Davis Kabole alisema filamu hiyo ni filamu yenye uhalisia wa maisha ya wasanii wa Bongo Fleva na ina ubora wa kipekee. Alisema filamu hiyo imejikita katika maisha ambayo msanii wa muziki huo anapita katika kufanikisha kazi zake kama vile kurekodi hadu kuingia sokoni na changamoto ambazo zinamkabili.
“Wadau wa filamu nchini wategemee makubwa kutoka kwenye filamu hii ya Machweo, ni filamu ambayo wote wataipenda na kuifurahia,” alisema Kabole. Naye Mratibu wa kampuni ya Event World, Dimo Debwe, alisema filamu hiyo italeta mapinduzi nchini na wanatarajia kuisaambaza mikoa yote ya Tanzania.
“ Machweo ni filamu iliyojikita katika uhalisia na ni muda wa kujipanga kwa ajili ya kesho na kutokata tamaa, hivyo Event World ni ulimwengu wa matukio, tunatengeneza na kutarajia kufaidia baadae,” alisema Debwe.
No comments:
Post a Comment