Sunday, January 8, 2012

CHAMA CHA MADAKTARI CHASEMA KUWASIMAMISHA MADAKTARI WANAFUNZI N UDHALILISHAJI WA KITAALUMA!


Chama cha Madaktari nchini MAT kimesema tukio la Serikali kuwasimamisha kazi madaktari wanafunzi , wafamasia na wauguzi ni ukandamizaji wa kitaaluma unaowanyima haki watumishi wa umma kudai haki zao za msingi pale zinapohitajika.

Katibu wa Chama hicho, DK RODRICK KABANGILA amesema kutokana na kitendo hicho, chama hicho kimepanga kuitisha mkutano wa wanachama wake ili kutoa msimamo wao juu ya ukandamizaji huo ikiwemo masuala ya kitaaluma kushughulikiwa kisiasa.


Akifafanua DK KABANGILA amesema baadhi ya watendaji wa Wizara la Afya na Ustawi wa Jamii wamekuwa wakiangusha serikali kwa kufanya maamuzi ambayo kama si ya kukomoana basi yanatekelezwa kwa ajili ya faida ya mtu mmoja. Aidha alieleza kwamba suala la kuwafukuza kazi madaktari wanafunzi zaidi 222, hakikufanywa kwa kufuata misingi ya haki na kwamba wao kama binadamu wengine walipaswa kwanza kutekelezewa stahiki zao kama wao walivyokuwa wakiwahudumia wagonjwa.
“Madaktari wanafunzi sio kama hawajui fani ya utabibu, tayari wamehitimu na kufuzu fani hiyo kinachofanyika ni kufanya kazi chini ya madaktari bingwa ili waendelee kupata ujuzi zaidi, hivyo kama wasipowezeshwa hawawezi kutoa huduma ipasavyo,” alisema Dk KABANGILA.Kwa upande wake Makamu wa Rais wa chama hicho DK PRIMUS SAIDIA amesema kwamba licha ya wao kukutana na uongozi wa Wizara ya Afya kufuatia barua ya kuwataka madaktari hao warudi Wizarani kwa ajili ya kupangiwa majukumu mengine.


Akifafanua DK Saidia amesema kuwa, inavyoonekana baadhi ya watendaji wa Wizara ya Afya hawafanyi kazi kwa ajili ya maslahi ya wananchi na badala yake wako serikali ili kutimiza matakwa yao. “Angalia baada ya serikali kuwalipa malipo yao madaktari wote waliokuwa wakishindwa kufika kazini kwa kukosa nauli walirudi hospitalini kutoa huduma. Kilichofuatia walifukuzwa wakitaka kutoa huduma kwa jamii,” alisema DK Saidia.


Kutokana na hilo aliuomba uongozi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili MNH kuliangalia upya suala hilo kwani wanaoumia sio wanasiasa ila ni wananchi wanyonge wasio na uwezo wa kwenda kutibiwa nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment