Rais wa Uganda Yoweri MuseveniSerikali za Rwanda na Uganda zimekubaliana kushirikiana kwenye nyanja mbalimbali za maendeleo. Maazimio hayo yamefikiwa na pande mbili kwenye kilele cha ziara ya siku nne ya Rais wa Uganda Yoweri Museveni nchini Rwanda.
Ziara ya Rais Museveni licha ya kujikita katika ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo, imekuwa ikitazamwa na wadadisi kama inayofungua ukurasa mpya wa uhusiano wa nchi hizo ambao ulikuwa umedorora kwa muongo mmoja uliopita.
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Rwanda Louise Mushikiwabo ndiye aliyelisoma tangazo la pande mbili lililotiwa saini na mawaziri wa mashauri ya kigeni wa Rwanda na Uganda. Tangazo hilo linaainisha sehemu ambazo nchi hizo zitashirikiana, ikiwa ni pamoja na uchumi, sayansi na teknolojia na hifadhi ya mazingira. Punde tu marais hao wakaanza mazungumzo na waandishi wa habari.
Madai ya mvutano kati ya Rwanda wa Uganda yapuuzwa
Waandishi wa habari walikuwa na shauku ya kujua ukweli wa jitihada za marais hao kuondoa tofauti zao ambazo zimekuwa zikiendelea ingawa chini kwa chini kwa takribani muongo mmoja uliopita. Hata hivyo marais wote walionekana kupuuza ikiwa kumekuwepo na mgogoro wowote, huku wakisisitiza kuwa nchi za Rwanda na Uganda zimekuwa na mafungamano ya kihistoria.
No comments:
Post a Comment