Wednesday, June 8, 2011

MAKAMU WA RAIS KUIWAKILISHA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA UN KUHUSU UGONJWA WA UKIMWI!

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal yupo mjini New York, Marekani ambapo anahudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya Ukimwi ulioandaliwa na UNAIDS.

Makamu wa Rais anaiwakilisha Tanzania katika mkutano huu unaojumuisha pia asasi za kiraia, uwakilishi wa vijana, wabunge, wadau katika mapambano dhidi ya Ukimwi nchini na wawakilishi wa serikali zote yaani serikali ya Muungano pamoja na SMZ.

Makamu wa Rais kwa mujibu wa ratiba iliyopo atakuwa anatoa hotuba ya Tanzania Juni 08, 2011 na hotuba yake inafafanua kuhusu nafasi ya Tanzania katika kupambana na ugonjwa wa Ukimwi huku akisisitiza juu ya wananchi wa Tanzania pamoja na serikali yao wanavyojitahidi kuhakikisha kuwa maambukizi mapya yanazidi kupungua kuliko kuongezeka.

Makamu wa Rais ambaye ameingia hapa jana anaambatana na Mama Zakhia Bilal ambaye naye ataungana na wake wa viongozi wa nchi mbalimbali katika mijadala ya nafasi yao katika kukabiliana na janga la Ukimwi, pia yupo Waziri wa Afya wa SMZ Duni Haji Duni, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Mahadhi Juma Maalim, Waziri wa SMZ Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Fatma Fereji na viongozi wengine wa Wizara ya Afya waliokuwa wakitarajiwa kufika jijini hapa jana.


Katika siku hiyo hiyo ya Juni 08, 2011 Makamu wa Rais Dkt. Bilal anatarajiwa kukutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ambapo mazungumzo yao yanatarajiwa kuzungumzia nafasi ya Umoja wa Mataifa katika mapambanao dhidi ya Ukimwi.

Makamu wa Rais pia atakuwa na mikutano kadhaa iliyoandaliwa na nchi za Marekani na Uingereza ambao ni wadau wakubwa katika kuisaidia Tanzania katika mikkati yake ya kupambana na Ukimwi. Katika mkutano wake wa kwanza na wawakilishi wa Tanzania kabla ya mkutano hiuo, Makamu wa Rais ametoa rai kwa wawakilishi wa Tanzania, kuhakikisha wanafatilia mkutano huu kwa umakini na kuandika ripoti zao kwa lugha ya Kiswahili ili punde mkutano huu unapoisha ripoti hizo ziweze kuwafikia wananchi wa Tanzania kupitia njia zote za mawasiliano.

Tena amesisitiza juu ya umuhimu wa wawakilishi wa Tanzania kuhakikisha kuwa wanautumia mkutano huu vema na kuwakilisha mawazo ya Watanzania kwa ajili ya kuisaidia Tanzania.

Kwa mujibu wa Ratiba ya Makamu wa Rais, atakutana na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Dkt. Asha Rose Migiro siku ya mwisho ya mkutano, huku pia akitarajia kuwa na mahojiano na vyombo kadhaa vya kimataifa ili kufafanua nafasi ya Tanzania katika mapambano dhidi ya Ukimwi.


Imetolewa na: Boniphace Makene
Mwandishi wa Habari wa Makamu wa Rais.

No comments:

Post a Comment