Sunday, August 28, 2011

TANZANIA HAIUTAMBUI UONGOZI WA BARAZA LA MPITO LA WAASI NCHINI LIBYA!

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imesema kuwa inaungana na nchi nyingine 40 za Afrika kutolitambua Baraza la Mpito la Waasi nchini Libya baada ya kukosa sifa za msingi ikiwemo kutoshikilia mihimili ya nchi kama Bunge na Mahakama.

Akizungumza Jijini Dar es salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, BERNARD MEMBE, ametaja idadi ya baadhi ya nchi za Afrika zilizotangaza kutambua Baraza hilo kuwa ni 13 zikiwemo Kenya Burundi, Ethiopia, Bukina Faso pamoja na Nigeria.
Katika hatua nyingine Waziri MEMBE, amesema kufuatia Wananchi wa Somalia kuendelea kupoteza maisha kutokana na baa la njaa lililoikumba pembe ya Afrika Tanzania iko tayari kuuza tani elfu kumi na moja za chakula kupitia Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP.
Wakati huo huo mmoja wa Waandishi wa habari aliyeko nchini Libya, SULEIMANI YUSUFU, amesema kuwa mpaka sasa hakuna uthibitisho wowote juu ya kuwepo kwa taarifa kuwa Kiongozi wa nchi hiyo Kanali MUAMMAR GADDAFI yuko tayari kukabidhi madaraka kwa waasi huku waasi nchini humo wakibainisha kuwa hawako tayari kwa mazungumzo yoyote dhidi ya Kiongozi huyo mpaka atakapojisalimisha.

No comments:

Post a Comment