BIASHARA

MV SEAGULL YAIOMBA SERIKALI KUWASAIDIA WAWEKEZAJI WA NDANI

Akizungumza Jijini Dar es salaam, Meneja wa Masoko wa Kampuni ya Seagul, SADICK MOHAMMED, amesema endapo wawekezaji wa ndani watawezeshwa na kupewa kipaumbele watamudu kuongeza idadi ya vyombo vya usafiri wa majini na kupunguza adha wanayopata abiria hivi sasa.
                               Meli ya Mv Seagull ikitia nanga kwenye banadari ya Dar es Salaam
Serikali imeshauriwa kutoa kipaumbele zaidi kwa wawekezaji wa ndani hususani wanaotoa usafiri wa majini ili kuboresha zaidi huduma hiyo tofauti na ilivyo sasa ambapo kumekuwa na msongamano mkubwa kwa abiria wanaotumia huduma hiyo wakati wa siku za sikukuu.



                              OIKOCREDIT YAZIKOPESHA SACCOS TATU MILIONI 700/-
                 Hafla ya kukabidhiwa hundi kwa Saccos za mjini Mwanza, Musoma na Shinyanga

Meneja wa Oikocredit Tanzania, Deus Manyenye (Kulia) akiagana na Mwenyekiti wa Saccos ya Mwanza, Stephen Nhigula wakati wa hafla ya kukabidhi hundi ya jumla ya milioni 700/- zilizotolewa kwa mkopo na shirika hilo kwa Saccos za Mwanza, Musoma na Shinyanga Foundation Fund jijini Mwanza hivi karibuni. Wengine ni Phillip Matayi na Paulo Sangija.

Na Mwanaeastafrica, Mwanza

Shirika la Oikocredit Tanzania limezikopesha Saccos tatu za Mwanza, Musoma na Shinyanga Foundation Fund jumla ya milioni 700/- zitakazotumika kusaidia wanachama wa taasisi hizo kujikomboa na umasikini unaowakabili na hatimaye kujiletea maendeleo katika jamii zao.

Katika makabidhiano hayo yaliyofanyika jijini Mwanza hivi karibuni Saccos ya Mwanza imekopeshwa jumla ya milioni 350/-, Musoma Sacco milioni 200/- na ile ya Shinyanga Foundation Fund shilingi milioni 150/-.


Akikabidhi msaada huo Meneja wa Oikocredit Tanzania Deus Manyenye amesema kuwa taasisi nyingi za kifedha haziamini kusaidia kwenye miradi ya watu masikini hivyo shirika lake limejikita kukopesha miradi yenye manufaa kwa jamii hususani ile inayojumuisha ngazi ya madaraka kwa wanawake.


“Oikocredit hupendelea mno miradi ambayo wanawake wanajumuishwa kwenye ngazi za maamuzi. Sisi tunaamini kwamba watu masikini wanaweza kujijengea maisha mazuri wakipewa fursa kama kuwezeshwa kifedha,” alisema Manyenye.


Akifafanua Meneja huyo amesema, tangu Oikocredit ianzishwe nchini mwaka 2006 tayari wameshakopesha miradi 30 yenye thamani ya shilingi bilioni 30 ili kuwasaidia watu masikini na wasiojiweza wanaoishi mijini na vijijini.

Takwimu zilizotolewa na shirika hilo ni kwamba inakadiliwa watu zaidi ya Bilioni 1.5 duniani wanaishi kwenye umasikini. Hawa siyo kwamba hawana uwezo, ila wanakosa fursa za kupata hela na kujikwamua, alisema Manyenye.


Akizungumza kwa niaba ya wenyeviti wa Saccos zilizokopeshwa fedha hizo, Mwenyekiti wa Shinyanga Foundation Fund, Paulo Sangija alisema watatumia fedha hizo kwa wakati ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa ya kuikomboa jamii kuondokana na umasikini.


“Mkopo huu umefungua mlango wa pili, tutakachohakikisha sisi ni jamii inanufaika na fedha hizi kwani tukizifuja tutadidimia zaidi. Ukikosa uwezo vilevile mbinu za upatikanaji wa mikopo unakosekana, tunashukuru na hatutakuangusha,” alisema Sangija.


Mbali na hayo Oikocredit ilishazikopesha jumla ya shilingi bilioni 2.1/- kwa YWCA Moshi na Saccos ya Wazalendo ili zitumike kuiwezesha jamii ya watu wa kipato cha chini. Fedha zilizotolewa zilitumika kwa ajili ya ukarabati wa jengo la makao makuu ya YWCA Moshi na uwezeshaji jamii ili ijiendeleze kimaisha kupitia Wazalendo.

Shirika hilo lenye makao yake makuu nchini Uholanzi zaidi ya miaka 36 sasa hadi kufikia Septemba 2009 limekopesha miradi zaidi ya 780 duniani na hutoa misaada ya kifedha kwa taasisi ambazo zina mikopo.