Mratibu wa vikundi vya Pambazuko Klabu wilayani Arumeru, Bi. Vick Kimaro.
Mwalimu Philipo Meli wa Shule ya Sekondari Kimyak wilayani Arumeru.
Wanafunzi wenye ulemavu wa Chuo cha Mafunzo kwa Watu wenye Ulemavu Usa River wilayani Arumeru wakifanya mahojiano na mtandao wa The Habari.com
Mwanafunzi Kelvin Bosco (mlemavu wa akili) toka Shule ya Msingi Naurei wilayani Arumeru akiandika ubaoni baada ya kupewa maelekekezo.
Na Joachim Mushi, Thehabari.com-Arumeru
BAADHI ya waenezi wa Mkataba wa Haki za Watu wenye Ulemavu na wafanyakazi walemavu wilayani hapa wameitaka Serikali kuonesha kwa vitendo utekelezwaji wa madhiriano ya mkataba huo ili kundi hilo kuanza kupata haki sawa za kimsingi kama ilivyo kwa watu wa kawaida.
Changamoto hiyo imetolewa hivi karibuni na Bi. Vick Kimaro ambaye ni mmoja wa viongozi wawakilishi wa watu wenye ulemavu wilayani Arumeru, wanaofanya kazi kwa ushirikiano na Kituo cha Habari Kuhusu Walemavu (ICD) cha jijini Dar es Salaam.
Bi. Kimaro ambaye ni mlemavu wa viungo (mguu) alisema licha ya Serikali kuridhia utekelezaji wa Mkataba wa Haki za Watu wenye Ulemavu bado maeneo mengi, baadhi ya wananchi na hata viongozi hawatambui uwepo wa mkataba huo, ikiwa ni pamoja na kutojali haki za msingi kwa walemavu.
Alisema kutokana na hali hiyo bado watu wenye ulemavu wamekuwa wakikumbana na vikwazo vingi katika ufuatiliaji wa haki mbalimbali ambazo ni za msingi kwa jamii yote. “...unaweza kujiuliza kama tayari kuna mkataba wa Haki za Watu wenye Ulemavu ambao Serikali imeridhia kwanini tunaendelea kukubwa na vikwazo kwenye huduma anuai za msingi?,” alisema Bi. Kimaro.
“Pia huwezi kuamini hadi leo wapo baadhi ya viongozi ambao hawatambui chochote juu ya ujio wa mkataba huo na ndiyo maana wanashindwa kuusimamia katika ngazi zao,” alisema Bi. Kimaro ambaye ni Mwakilishi wa Watu wenye Ulemavu wa Chama cha Walimu Arumeru.
Akizungumza katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi, Philipo Meli ambaye ni mwalimu mlemavu (asiyeona) wa Shule ya Sekondari Kimyak wilayani Arumeru amesema Serikali ndiyo inayopaswa kuonesha njia ya kuwajali walemavu hasa katika elimu. Alisema bado nyenzo za kufundishia na kujifunzia kwa watu wenye ulemavu hazipewi kipaumbele jambo ambalo linaweza kuwadidimiza kundi hilo katika harakati ya kujikomboa na hata kujitegemea.
“Mimi ni mwalimu mlemavu wa macho nafundisha kwa kutumia nyenzo maalumu lakini nyenzo hizo sina...kitu cha msingi ambacho Serikali inatakiwa kukikazania kwa kundi hili ni kuwapa elimu kama ilivyo kwa makundi mengine. Binafsi nimetembelea kiwanda cha vitabu pale Dar es Salaam juzi hakuna vitabu kabisa vya walemavu, sasa utamsaidiaje mlemavu kwa mtindo huu...,” alisema Meli akizungumza kijijini Kimyak.
Alisema mara zote anapofuata vitabu kwa ajili ya kufundishia hapati vyote na hata vilivyopo vimepitwa na wakati jambo ambalo ni gumu kuwasaidia watu wenye ulemavu. “Kiwanda hiki ndicho kinachochapisha vitabu kwa watu wenyeulemavu...wanasema hawana vitabu kwa kuwa hawapati ruzuku ya kutosha serikalini, yaani kati ya vitabu 86, ambavyo vinahitajika kwa kada hii ni vitabu sita tu nilipewa nilipofuatilia nyenzo hizo Dar es Salaam, kwa hali hii utamsaidiaje mlemavu.
Aidha alisema elimu ndio nguzo ambayo Serikali inapaswa kuiongezea nguvu kwani iwapo idadi kubwa ya kundi hili litawezeshwa kielimu linaweza kufanya mabadiliko na kujikomboa kiuwezo kabla ya kuingia katika huduma nyingine. 'Habari hii imeandaliwa na mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com) kwa kushirikiana na Kituo cha Habari Kuhusu Ulemavu (ICD) Dar es Salaam'
No comments:
Post a Comment