Ardhi, Maji na Ajira kuamua Ubunge Arumeru Mashariki.
Na Zitto Kabwe
"Uchaguzi wa Ubunge Arumeru Mashariki ni kipimo cha namna wananchi mnavyoridhika na watawala, namna mnavyoridhika na mgawo wa Ardhi na namna mnavyoridhika na mgawanyo wa Maji katika Wilaya yenu". Haya yalikuwa baadhi ya maneno yangu katika hotuba ya kumkaribisha Mwenyekiti wa Taifa CHADEMA ndugu Freeman Mbowe kuzindua kampeni za chama chetu katika viwanja vya Leganga katika mji mdogo wa USA River wilayani Arumeru.
Siku moja kabla ya siku ya uzinduzi nilikuwa najisomea makala mbalimbali kuhusu Wilaya ya Arumeru. Pia nilitumia muda mrefu kuzungumza na wananchi wa Meru ili kujua uchaguzi huu una maana gani kwao. WaMeru wengi niliozungumza nao waliniambia namna wanavyochukizwa na ukosefu wa Ardhi kwa wananchi. Baadhi waliniambia kwamba Kama Serikali haitachukulia suala la Ardhi kwa uzito wake Meru kutatokea vurugu kubwa sana.
Vurugu Meru sio Jambo jipya kabisa. Inakumbukwa kwamba miaka ya 1950 kulitokea fujo na wananchi kuchomewa nyumba zao ili kupisha wakulima wakubwa kutoka Afrika Kusini (makaburu) katika eneo la Engarananyuki. Vurugu hizi ndio zilipelekea WaMeru kuchanga fedha kumpeleka ndugu Jafet Kirilo huko Umoja wa Mataifa kutetea Ardhi ya Wameru mwaka 1952 kufuatia vurugu za mwaka 1951. Licha ya juhudi hizo bado Ardhi ni tatizo kubwa kwa wananchi wa Meru.
Mashamba makubwa ambayo walipewa walowezi wakati wa Uhuru yaligawiwa kwa familia chache sana Meru. Wanasiasa walijipa mashamba makubwa na mengine mpaka Leo hayakugawiwa. Ujamaa na utaifishaji wa mashamba haukufanyika Meru kwa mshangao mkubwa sana na hata mashamba ambayo Serikali ya Mwalimu Nyerere iliagiza wapewe wananchi walipewa Wabunge, Madiwani, Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri (soma Brian Cooksey kuhusu uwekezaji katika Maua, June 2011).
Hivi Leo Ardhi kubwa ya Meru imeshikwa na matajiri na kulimwa Maua. Kilimo hiki cha Maua mwaka 2008 kiliingizia Taifa fedha za kigeni takribani tshs 150bn. Hata hivyo kuna malalamiko makubwa sana ya wananchi wanaofanya kazi katika mashamba haya kuhusu malipo duni na nyenzo za kufanyia kazi. Kuna malalamiko kuhusu kemikali na madawa yanayotumika na afya ya mfanyakazi kutozingatiwa.
Ifahamike kwamba Benki ya Rasilimali Tanzania inasimamia mikopo ya zaidi ya tshs 50bn ambazo kampuni za Maua zilipewa kwa Dhamana ana ya Serikali. Katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, suala hili liliibuliwa na Mkurugenzi Mkuu wa TIB kukiri kwamba hakuna kampuni umeanza kulipa mikopo hii. Ni dhahiri Serikali itajikuta inalipa madeni haya yaliyokopeshwa kwa kampuni binafsi! Hii pia inaonyesha namna amabvyo serikali inafanya haraka na wepesi kusaidia wawekezaji kuliko wananchi wanaoteseka na kukosa Ardhi ya kulima na kujipatia ruziki.
Wawekezaji wanapewa Ardhi na mtaji!
Haya ndio yanajenga hasira ya wananchi wa Meru. Hasira hii kwa vyovyote itahamishiwa katika sanduku la kura ili kumpata Mbunge kutoka miongoni mwao atakayeweza kusimama kidete kuhakikisha Ardhi inapatikana kwa wananchi wa Meru. Kwa nini huko nyuma, katika chaguzi zilizopita Jambo hili halikuwapa hasira wananchi? Ni dhahiri hapakuwa na Mwanasiasa ambaye ana uwezo mkubwa wa kulieleza na kuwapa imani wananchi. Ndugu Joshua Nassari amedhihirisha kwamba analijua tatizo hili kwa dhati kabisa. Nilivyomsikiliza akiongea katika kampeni, na pia katika mazungumzo yetu binafsi amenithibitishia kuwa ni mwanasiasa kijana mwenye kipaji kikubwa katika kujenga hoja na ku articulate masuala ya msingi.
Changamoto nyingine kubwa kwa Meru ni haki ya kupata Maji. Meru kuna Maji mengi sana lakini matajiri wenye mashamba wameyazuia Maji hayo na hivyo wananchi wa kawaida hawapati Maji ya kumwagilia mazao Yao na pia kwa matumizi ya nyumbani. Hili nalo linajenga hasira kubwa sana kwa wananchi wa kawaida. Ardhi na Maji ni masuala yanayokwenda pamoja wilayani Meru.
Mwisho kabisa nimeona makundi ya vijana wasio na ajira na hivyo kukosa Kipato. Vijana wengi wanashinda kwenye stendi za mabasi na kuita abiria. Ukosefu wa Ajira kwa vijana Kama tusemavyo kila wakati ni changamoto kubwa sana kwetu viongozi na hasa viongozi vijana. Natumai ndugu Joshua Nassari atahusisha suala la Ardhi na Maji katika muktadha mzima wa Ajira na Kipato kwa wananchi wa Arumeru Mashariki. Uchaguzi wa Arumeru ni uchaguzi kati ya kuwa na Ardhi au kuendelea kutokuwa nayo. Ni uchaguzi muhimu kwa watu wa Meru. Wasio na Ardhi watamchagua mgombea atakayesimamia mgawo wa Ardhi unaozingatia haki. Mgombea huyo ni mgombea wa CHADEMA ndugu Joshua Nassari.
Mh Zitto Kabwe.
No comments:
Post a Comment