TAARIFA KWA UMMA
CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO
Baada ya kupokea taarifa za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), juu ya kuwepo kwa uchaguzi katika Jimbo la Arumeru Mashariki, Sekretarieti ya CHADEMA tayari imekaa na kuandaa utaratibu mzima wa uchukuaji na urudishaji wa fomu, ambao utafuatiwa na vikao vya chama, kuanzia ngazi ya wilaya hadi taifa, kwa maana ya Kamati Kuu, katika kufanya uteuzi wa mwisho wa kumpata mgombea.
Ili kutoa muda wa kutosha kwa shughuli ya utoaji na urejeshaji fomu, Sekretarieti ya CHADEMA imeamua kuwa wanachama wa CHADEMA wenye nia ya kuwania uteuzi wa kugombea ubunge kwa tiketi ya CHADEMA, kwa ajili ya kuwatumikia watu wa Arumeru Mashariki, wataanza kuchukua na kurudisha fomu kuanzia leo tarehe 14 Februari 2012 hadi tarehe 25 Februari 2012 saa 10 Jioni.
Fomu zinatolewa kupitia ofisi ya CHADEMA ya Wilaya ya Meru zilizopo eneo la Maji ya Chai-USA River, na pia katika ofisi za CHADEMA za Mkoa wa Arusha zilizopo Ngarenaro katika Mtaa wa NHC.
Baada ya hapo, vikao vya chama vinavyohusika na uteuzi wanachama watakaokuwa wamechukua fomu na kutimiza masharti kadri inavyoelekezwa, vitakaa kufanya uteuzi na hatimaye kumpata mgombea mmoja, ambaye chama kitamsimamisha na kumsimamia kuwania jimbo hilo, ili ashinde na kuongeza nguvu ya wapambanaji ndani ya wabunge, kuwawakilisha Watanzania.
Mchakato wa uteuzi ngazi ya jimbo na wilaya utafanyika kati ya tarehe 26 Februari 2012 mpaka tarehe 29 Februari 2012 wakati uteuzi ngazi ya taifa utafanyika tarehe 3 Machi mpaka 4 Machi 2012.
Kupitia kwa Kurugenzi ya Habari na Uenezi, CHADEMA ikiwa ni chama mbadala katika kuunda serikali na chama kikuu cha upinzani nchini, kinawahakikishia wanachama, wapenzi wake na Watanzania wote kwa ujumla, kuwa kama ilivyo kawaida yake, kitashiriki katika uchaguzi huo mdogo wa Arumeru Mashariki, kwa lengo la kushinda.
Kwa umakini na uimara ambao kimeendelea kuudhihirisha katika kuwatumikia na kuwawakilisha Watanzania kupitia majukwaa mbalimbali, tangu Watanzania walipoonesha dalili zote za kukiunga mkono na kukiamini kuwa kinaweza kupewa dhamana ya uongozi wa nchi hii, ari ya chama hiki imezidi kuongezeka siku hadi siku, kikijiandaa kupokea dhamana kubwa zaidi kadri siku zinavyokwenda.
Hivyo katika uchaguzi wa Arumeru Mashariki Wanachama na wananchi kwa ujumla wazingatie kwamba CHADEMA itaendelea kutimiza dhima yake ya kuhakikisha uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganizesheni dhabiti kwa maendeleo endelevu ya Tanzania.
Imetolewa leo tarehe 14 Februari 2012, Dar es Salaam na;
John Mnyika
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
No comments:
Post a Comment