Hivi karibuni kumejitokeza upotoshaji kwenye baadhi ya vyombo vya habari juu ya masuala yaliyojadiliwa na Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa iliyokutana Novemba 23-24, 2011 mjini Dodoma.
Katika kujenga uhalali wa upotoshaji huo, taarifa zinazotolewa katika baadhi ya vyombo vya habari nchini zinaendelea kutoeleza ukweli juu ya ajenda zilizojadiliwa ndani ya Kikao hicho cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, na badala yake kutoa taarifa zilizojaa upotoshaji mwingi.
Moja ya gazeti la kila siku lililochapishwa Desemba 6,2011 limeeleza katika sehemu ya Maoni yake kuwa;
“Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kilichoketi Dodoma mwezi jana hakikujadili masuala magumu yanayoikabili nchi na watanzania kwa ujumla, kama vile ukosefu wa ajira, mfumuko wa bei na maisha ya mwananchi wa kawaida”. Wanaendelea kuzusha kuwa; “Badala yake wakawa wanajadili mifumo na namna ya kujiweka vizuri kwa ajili ya uchaguzi ujao-jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limetufanya tuwe tunajadili watu badala ya namna ya kulinasua taifa letu katika umaskini”
Sehemu hiyo ya Maoni ya gazeti la “Mtanzania” la desemba 6, 2011 linadhihirisha kusudio la kiuandishi katika kuelezea mantiki ya mijadala mbalimbali iliyoibuka ndani ya Kikao hicho cha NEC mjini Dodoma limebeba malengo binafsi yenye dhamira mahususi ya kuendeleza jitihada za kuupotosha ukweli ndani ya umma. Ukweli ni kwamba katika kikao hicho cha NEC kilichofanyika mwishoni mwa mwezi uliopita, kilijadili kwa kina mambo mbalimbali yanayolikabili taifa na wananchi wake kama ifuatavyo:-
1. UNUNUZI WA MAHINDI
Iliipongeza Serikali kwa kuruhusu uuzaji wa mahindi nje ya nchi, hali ambayo itasaidia mahindi yaliyobaki kwa wakulima kupata soko. Hata hivyo, imesisitiza kuwepo na tahadhari sasa na siku zijazo, ili chakula chote kisiuzwe nje ya nchi na kusababisha tatizo la njaa nchini. Iliitaka Serikali iimarishe Wakala wa Chakula wa Taifa kwa kuuwezesha kwa na fedha zaidi na kujenga maghala mengi na makubwa zaidi ili uweze kununua kiasi kikubwa cha mazao.Iliiagiza Serikali ihimize kuundwa kwa Vyama vya Ushirika vya Mazao ya Chakula, ambavyo navyo viwezeshwe kujenga maghala ya kuhifadhi nafaka katika maeneo yao pamoja na kuanzisha mfumo wa ununuzi wa mazao wa stakabadhi ghalani.
2.NISHATI YA UMEME NA MAFUTA NCHINI
Halmashauri Kuu ya Taifa iliipongeza Serikali kwa kutengeneza mpango wa umeme wa dharura, licha ya gharama kubwa, lakini umesaidia kuleta nafuu katika uzalishaji umeme na kupunguza kero kwa wananchi. Pia NEC iliitaka Serikali kutoa taarifa sahihi kwa wakati kuhusu mgao wa umeme na maeneo yanayoathirika ili kupunguza lawama kwa Serikali. Aidha iliitaka Serikali kuongeza jitihada za kuzalisha umeme kwa vyanzo vingine, hasa makaa ya mawe ambayo yapo nchini na umeme wake ni nafuu. Halmashauri Kuu ya Taifa ilipongeza pia jitihada za Serikali kusambaza umeme nchini, ambapo sasa karibu kila Makao Makuu ya Wilaya yana umeme.
Hata hivyo, iliitaka Serikali, kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), iongeze kasi ya usambazaji umeme vijijini ili kufikia lengo la Ilani ya Uchaguzi ya CCM. NEC ilipongeza jitihada za Serikali za kutafuta fedha (dola za Kimarekani takriban bilioni 1) za ujenzi wa bomba kubwa la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ambalo litawezesha kuongeza uzalishaji wa umeme na kuondokana na matumizi ya mafuta kuzalisha umeme. Aidha, Serikali ilitakiwa kuharakisha taratibu zote za upatikanaji wa fedha hizo ili utekelezaji wa mradi huo uanze mara moja.
3. UPANGAJI WA BEI ZA NISHATI YA MAFUTA.
Kutokana na umuhimu wa nishati ya mafuta kwa ustawi wa uchumi wa nchi yetu, Halmashauri Kuu ya Taifa iliitaka Serikali kuhakikisha kwamba EWURA inakuwa na uwezo, utaalamu na weledi wa kuisimamia sekta hii ipasavyo. Aidha iliipongeza Serikali kwa uamuzi wa kuwa na hifadhi ya Kimkakati ya Mafuta, na wa kuanzisha Kampuni ya Mafuta ya Taifa kwa sababu itasaidia kuziba pengo pale linapotokea tatizo la hujuma kwa waagizaji wa sekta binafsi.
4. MIGOGORO YA ARDHI
Halmashauri Kuu ya Taifa iliitaka Serikali ihakikishe kwamba katika uwekezaji unaohusisha umiliki wa maeneo makubwa ya ardhi, wananchi wasiporwe au kudhulumiwa au kushurutishwa kuhama kwenye ardhi yao bila fidia stahiki. Iwahamasishe pia wawekezaji waliopewa maeneo ya kulima mashamba makubwa kusaidia wakulima wadogo walio karibu na mashamba hayo makubwa kuinua kilimo chao. Kuhakikisha uongozi wa Serikali katika ngazi zote kushughulikia kwa haraka migogoro ya ardhi nchini ili kupunguza kero kwa wananchi.
Iliipongeza Serikali kwa kushughulikia migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima, ambayo kwa sasa imepungua kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo imesisitiza jitihada ziendelezwe serikali katika kupanga matumizi ya ardhi, hasa kutenga maeneo maalum ya wakulima na wafugaji ili kuepusha muingiliano ambao husababisha migogoro. Hayo ni miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa na NEC katika kikao chake hicho. Inapoibuka hoja kuwa pamoja na kikao hicho kujadili mambo hayo, bado tathimini yake ni sawa na hakuna kitu kilichojadiliwa, lazima kumtilia au kukitilia shaka chombo husika, kwani kusudio lake litakuwa na malengo maalum.
Kuhusu upotoshaji wa taarifa za kikao hicho ambao unaendelea kufanywa na gazeti la Mtanzania, si busara kuendelea kuzifanyia kazi kupitia majibizano katika vyombo vya habari, kwani taarifa zinaeleza kuwa wanamkakati wa kuendelea kwa muda mrefu kueneza upotoshaji huo. Naamini mnafahamu kuwepo kwa kesi ya uchaguzi iliyofunguliwa kupinga ushindi wa CCM jimboni Igunga. Kutokana na utaratibu wa mahakama kutoruhusu mashauri yaliyopo mahakamani kufanyiwa mijadala nje ya mahakama, gazeti hilo limeendeleza hoja zenye malengo tarajali kwa kuzusha kuwa ushindi wa CCM Igunga ulitokana na kugawanywa kwa Mahindi ya msaada wa njaa, jambo ambalo si kweli.
Chama tumeamua tuwaachie nafasi ya kutosha kutekeleza mkakati wao na wakimaliza watutaarifu tutatolea ufafanuzi mambo yote mwanzo mpaka mwisho.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Nape Moses Nnauye
KATIBU WA HALMASHAURI KUU ITIKADI NA UENEZI
7/12/2011.
No comments:
Post a Comment