Na Benjamin Sawe, Maelezo
Dar es Salaam
Baraza la madiwani la Jiji la Dar es Salaam limeazimia na kukubaliana kuuita mtaa wa Garden jina la Jiji la Hamburg la nchini Ujerumani ikiwa ni heshima na kuimarisha mahusiano yaliyoanzishwa baina ya Jiji la Dar es Salaam na Jiji hilo. Taarifa iliyosainiwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Dkt. Didas Massaburi imesema kuwa katika Mkutano huo Baraza limeazimia na kukubali hoja ya mtaa mmoja wa Jiji la Hamburg la nchini Ujerumani kuitwa jina la Dar es Salaa Square.
Aidha katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Karimjee tarehe 7 Septemba, 2011 Baraza la madiwani liliomba kuondolewa kwa hoja mbili za kusoma na kuthibitisha baadhi ya mihtasari ya vikao vilivyopita na taarifa ya Kamati za kudumu. Taarifa hiyo iliendelea kusema kuondolewa kwa hoja hizo kumetokana na Baraza la madiwani kumtaka Mkurugenzi wa Jiji awasilishe mihtasari ya vikao vya nyuma ili vijadiliwe kwa pamoja badala ya kuleta baadhi ya mihtasari ya kuanzia Julai 2010 hadi Februari 2011
Pia limemwagiza mkurugenzi atoe na kupeleka sababu za kutoweza kuandika na kuwasilisha mihtasari kwa wakati katika Kamati ya uongozi ili kubaini kama kuna uzembe na kuchukuliwa hatua stahiki.
No comments:
Post a Comment