Tuesday, July 19, 2011

LEO KATIKA HISTORIA NI SIKU YA MAPINDUZI YA NICARAGUA!

Leo ni Jumanne tarehe 17 Shaaban 1432 Hijria sawa na tarehe 19 Julai 2011 Miladia. Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita mapinduzi ya wananchi wa Nicaragua yalipata ushindi dhidi ya dikteta Anastasio Somoza wa nchi hiyo na muitifaki wake mkubwa yaani Marekani.

Dikteta huyo kibaraka wa Marekani alichukua hatamu za uongozi wa Nicaragua mwaka 1967 na tangu wakati huo wimbi kubwa la upinzani lilianza kuenea nchini kote na katika America ya kati dhidi ya kiongozi huyo. Mapambano ya silaha ya wapiganaji wa mwituni wa harakati ya Sandinista ya FSLN yaliyoanza mwaka 1963 yalipamba moto zaidi katikati ya mwongo wa 1970 na kuungwa mkono na wananchi.


Hatimaye Somoza alilazimika kukimbia nchi baada ya jeshi la Sandinista kuingia Managua mji mkuu wa Nicaragua katika siku kama ya leo. Karibu watu elfu 40 waliuawa katika mapinduzi ya Nicaragua. Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita alizaliwa msomi mashuhuri wa Kiislamu Muhammad Hussein Kashiful Ghitaa.


Ayatullah Kashiful Ghitaa alizaliwa katika mji mtakatifu wa Najaf katika familia ya wasomi na wachamungu na kuanza kutafuta elimu akiwa bado mtoto mdogo. Baada ya kukamilisha elimu ya msingi na ya kati, Ayatullah Kashiful Ghitaa alihudhuria darsa za maulamaa wakubwa wa zama hizo na kukwea daraja za juu za elimu katika kipindi kifupi. Alifanikiwa kulea wasomi na maulamaa wakubwa na kufanya safari katika nchi nyingi za Kiislamu kwa ajili ya kueneza elimu na maarifa.


Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu pia alikutambua kushiriki katika masuala ya kisiasa na kutilia maanani masuala ya serikali na utawala kuwa ni katika mambo ya wajibu na alikuwa na mchango mkubwa katika kuanzisha Harakati ya Kitaifa ya Iraq.


Ayatullah Kashiful Ghitaa alishiriki vilivyo katika mapigano ya jihadi ya wananchi wa Iraq wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia dhidi ya jeshi vamizi la Uingereza. Mwanazuoni huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi katika nyanja mbalimbali.


Na siku kama ya leo miaka 118 iliyopita alizaliwa malenga wa Russia Vladimir Mayakovsky. Mashairi yake yalitoa huduma kubwa katika mapinduzi ya Kikomunisti huko Urusi hapo mwaka 1917 na kuwa marejeo muhimu ya wanamapinduzi hayo. Aliamini kwamba fasihi inapaswa kuenezwa baina ya wananchi wa kawaida na kueleza mashaka na matatizo yao.

No comments:

Post a Comment