Wednesday, July 27, 2011

KAMANDA KOVA MGENI RASMI REDDS MISS ILALA!

Kamanda wa Kanda maalum ya Kipolisi Suleiman Kova ndiye atakuwa mgeni rasmi siku ya Ijumaa 29.7. 2011 kwenye mashindano ya kumtafuta mrembo wa Kanda ya Ilala katika viwanja vya Mnazi mmoja Dar es salaam.
Washindi watatu au zaidi wa shindano hilo la Redds Miss Ilala wataiwakilisha Manispaa hiyo, kwenye shindano la kumtafuta Mrembo wa Tanzania litakalo fanyika mapema mwezi wa Septemba.


Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Kamanda Kova kushiriki kwenye mashindano ya Urembo ya Miss Ilala kama mgeni rasmi tangu alipohamia Dar es salaam miaka michache iliyopita.


“Waandaji wa Redds Miss Ilala mwaka huu tunajivunia kuwa pamoja na Kiongozi huyu ambaye ndiye mwenye dhamana ya usimamizi wa Ulinzi na Usalama katika jiji la Dar es salaam. Pia ukizingatia kuwa warembo wanaoshiriki kwenye shindano hili, walishiriki katika shughuli za kuhamasisha Ulinzi shirikishi anao simamia yeye” Uwepo wa kamanda Kova binafsi katika viwanja hivyo, ni hakikisho tosha kwamba ulinzi wa uhakika utakuwepo kwenye maeneo hayo.


Shindano la Redds Miss Ilala ambalo kwa mara ya kwanza litakuwa linafanyika katika viwanja vya Mnazi mmoja litaanza saa mbili usiku, na linategemewa kumalizika saa saba kamili usiku huo.


Ulinzi wa maeneo yanayozunguka uwanja umeimarishwa na siku hiyo ulinzi utaongezeka kuhakikisha usalama wa kila atakayeingia na mali yake viko salama. Magari na Piki piki za watu wote watakao ingia kwenye shindano hili yataruhusiwa kuingia ndani ya viwanja na yatapewa ulinzi bila malipo yoyote ya parking au ulinzi .


Mandhari ya uwanja wa Mnazi mmoja yatabadilishwa na kugeuzwa kuwa eneo la starehe na burudani. Michoro ya viwanja hivyo imetengenezwa kwa kufananishwa na Taman Mini Indonesia park iliyoko katika jiji la Jakarta.


Watu wote wenye tiketi za VIP au watu mashuhuri watapewa makaribisho wanayo stahili na kula chakula cha jioni uwanjani hapo. Wageni wengine watapewa nafasi ya kujinunulia vyakula na vinywaji viwanjani hapo.


Shindano la Redd Miss Ilala mwaka huu linafanyika huku Wakazi na wale wanaofanyia kazi au biashara zao katika maeneo yaliko kwenye Manispaa ya Ilala wakiwa na usongo wa kurudisha taji la Miss Tanzania lililopotea kwa muda wa miaka tisa sasa!

Katika miaka yote hiyo, Ilala imefanya vizuri sana kuliko kanda nyingine yoyote kwa kulikosa kosa na kuambulia nafasi ya pili, ya tatu au ya nne.


Mara ya mwisho Ilala kushinda Taji la Miss Tanzania ilikuwa ni mwaka 2002 aliposhinda Angela Damas. Mwaka 2003, Ilala ilipata nafasi ya tatu kupitia kwa Nargis Mohamed, 2004 nafasi ya pili kupitia kwa Verdiana Kamugisha, 2005 nafasi ya nne na tano kupitia kwa Feza Kessy na Parminda Raj, 2008 nafsi ya pili kupitia kwa Sylivia Mashuda, 2009 nafasi ya pili na nne kupitia kwa Juliet Lugembe na Sylivia Shally na mwaka 2010 nafasi ya tatu kupitia kwa Consolata Lukosi.


Kwa hiyo kuna kila dalili kwamba wale watakao hudhuria shindano la Redds Miss Ilala watakuwa wamemshuhudia Vodacom Miss Tanzania ajaye.

No comments:

Post a Comment