Wednesday, June 15, 2011
BAJETI MBADALA YA KAMBI YA UPINZANI INADHIHIRISHA UONGO WA CHADEMA- CCM!
1.0 UTANGULIZI:
Leo tarehe 15/06/2011 kambi ya upinzani bungeni ambayo inaundwa na chama cha CHADEMA kupitia waziri wake kivuli wa fedha Mhe. Zitto Kabwe (Mb), imewasilisha bajeti yake aliyoiita bajeti mbadala kwa mwaka wa fedha 2011/2012.
Nichukue nafasi hii kumpongeza kijana mwenzangu kwa uwasilishaji wa bajeti na kwa baadhi ya mambo ya msingi yaliyomo ndani ya bajeti husika.Hata hivyo bajeti imeacha maswali kadhaa bila majibu.
Katika bajeti hiyo pamoja na mambo mengine kwa kiasi kikubwa imedhihirisha kuwa maneno mengi na ahadi nyingi zilizotolewa na CHADEMA wakati wa Uchaguzi kama sio zote basi nyingi zilikuwa ahadi hewa zilizolenga kuwa hadaa wapiga kura kwa nia ya kupata kura.
2.0 MANTIKI YA HOJA:
Moja kati ya misingi mikuu ya kutengeneza bajeti katika mazingira ya siasa za kwetu na nyingine nyingi duniani ni ahadi ambazo chama kimeahidi kwa Wananchi wake aidha kwa kupitia Ilani ya Uchaguzi au ahadi binafsi za Mgombea Uraisi alizozitoa kipindi cha kampeni ya uchaguzi. Kwa maneno mengine bajeti ni zao la Ilani ya Uchaguzi ya Chama husika na sera mbalimbali zilizopo.
2.1 Elimu Bure kwa Watanzania kwa ngazi zote;
Kwa mfano kupitia Ilani ya CHADEMA ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na ahadi kibao za kila mara za aliyekua mgombea urais wa chama hicho Dr. Slaa, waliahidi wakichaguliwa watatoa elimu bure kuanzia chekechea mpaka chuo kikuu.
Itakumbukwa hii ni moja ya ahadi zilizovutia sana wakati huo, lakini huku wakijua kuwa wanadanganya waliendelea kutoa ahadi hiyo kwa muda wote wa kampeni hizo, sasa imefika wakati tulitegemea wangeonyesha kwa vitendo kwa kuweka kwenye bajeti yao jinsi wanavyoweza kutoa elimu bure lakini bajeti hii mbadala ya 2011/2012 ni uthibitisho wa hadaa ya CHADEMA kwa umma wa watanzania.
Hapa namnukuu Waziri kivuli wa fedha,
“..(ix)kuondoa ada kwa wanafunzi wa shule za sekondari za kutwa na kupunguza ada kwa sekondari za bweni kwa kiwango cha asilimia hamsini kwa wavulana na bure kwa wasichana...”
Lakini katika Ilani yao ya Uchaguzi ya mwaka 2010 ukurasa wa 15. Inaeleza CHADEMA itahakikisha “ Elimu ya ngazi ya msingi na sekondari itagharimiwa na serikali kuu pamoja na serikali za mitaa”.
Hapo ndipo tunapouona uongo dhahiri wa CHADEMA wa kukiri kuwa Serikali haiwezi ikatoa Elimu bure kwani katika Bajeti yao mbadala wanakiri kuwa watapunguza ada kwa asilimia hamsini kwa wavulana.
Kwa mantiki hiyo suala la wanafunzi wa sekondari kuchangia wanalikubali ila walitumia ghiliba kipindi cha kampeni ili kuwaongopea Watanzania kwa kitu ambacho hawawezi kukitekeleza.
Kinachosikitisha zaidi, kwenye bajeti hii mbadala iliyosomwa leo, inaonyesha dhahiri kwa upande wa elimu; hakuna mpango wowote unaozungumzia “Elimu ya Juu” kama vile si kitu kwao ukilinganisha na walivyokuwa wakihubiri kwenye majukwaa wakati wakitafuta kura. Hakika huu ni usanii mkubwa kumbe walikuwa wakitafuta kura za vijana hawa tu hawana mpango nao!!
2.2 Kushusha bei ya vifaa vya ujenzi;
Ahadi nyingine kubwa iliyovuta hisia za wengi ni ya kushusha bei ya mfuko wa saruji kufikia shilingi za kitanzania elfu tano, pamoja na vifaa vingine vya ujenzi. Kwenye bajeti hii mbadala tulitegemea wangewaeleza watanzania hili wangelifanyaje lakini badala yake waziri kivuli wa fedha anaishia kusema;
“..itakuwa marufuku kwa kituo cha uwekezaji kutoa ruhusa ya msamaha wa kodi kwa makampuni ya uwekezaji kwa bidhaa zinazozalishwa nchini na hasa Saruji....”
Hapa hakuna mkakati wowote wa kufanya mfuko wa saruji uuzwe shilingi za kitanzania elfu tano kama CHADEMA walivyotaka watanzania waamini wakati wa uchaguzi. Huu ni ushahidi wa hadaa ya CHADEMA.
Kwenye bajeti hii mbadala waziri kivuli anasema.... “ujenzi wa barabara za vijijni utatumia kwa kiasi kikubwa nguvu kazi watu (labour intensive)..”
Viongozi wengi wa CHADEMA wanasifika kwa kuzuia wananchi wasichangie shughuli mbalimbali za maendeleo huko vijijini, leo inashangaza kusema watatumia kwa kiasi kikubwa nguvu kazi watu, huu bila shaka ni unafiki na hadaa kwa wananchi.
2.3 Suala la kukwepa kodi;
Umejengeka utamaduni wa watu na taasisi mbalimbali kukwepa kodi na kuona kuwa suala hilo ni la kawaida. Lakini ikumbukwe kuwa kukwepa kodi kunaipunguzia mapato serikali na hivyo kupunguza uwezo wake wa kutoa huduma kwa jamii.
CHADEMA wanakiri hili kupitia Bajeti yao mabadala iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha Kivuli Mhe. Zitto Kabwe, kuwa ......”kuna watu wengi sana ambao wanapata mapato makubwa lakini hawalipi kodi......” Kauli hii ya CHADEMA inapingana na matendo yao halisi, kwani itakumbukwa wanamlipa katibu Mkuu wao Dr. Wilbroad Slaa zaidi ya shilingi Milioni saba, fedha ambayo haikatwi kodi yeyote.
Chakushangaza zaidi pamoja na CHADEMA kuendelea kumlipa Dr. Slaa mamilioni yasiyotozwa kodi, bila aibu Zitto anatoa wito kwa kila Mtanzania mwenye kipato alipe kodi ya kipato chake.
Na anaendelea kusema kuwa ... “kulipa kodi ndio ishara ya Uzalendo na ili raia aweze kuinyoshea kidole serikali yake lazima awe na uchungu na uchungu unapatikana kwa kulipa kodi.”
Kwa kauli hii ya Zitto, anauthibitishia umma wa Tanzania kuwa Dr. Slaa siyo mzalendo na wala CHADEMA pia siyo wazalendo. Kwani Dr. Slaa alitakiwa kukataa kuchukua mshahara usiokatwa kodi, na Chama chake kilipaswa kupeleka kodi za watumishi wake serikalini.
2.4 Kima cha chini cha mshahara;
Katika bajeti yao mbadala, CHADEMA wanaahidi kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa Umma mpaka kufikia Tshs. 315,000 kwa mwezi na kutoa motisha kwa walimu wanaofundisha Vijijini kwa kuwapa Mshahara mara moja na nusu ya wenzao wanaofundisha mijini.
Cha kushangaza hawajaainisha fedha hizo za ziada watazitoa wapi, hata katika mchanganuo wao wa mapato hawajaonesha kuwa kiasi hicho cha pesa kitatoka wapi. Huu ni usanii mkubwa na uongo ulikithiri.
3.0 HITIMISHO:
Ukipitia mambo haya machache kama mifano utagundua kuwa sehemu kubwa ya ahadi za CHADEMA kwa wananchi ni ulaghai na uongo usio na mfano, hivyo wananchi wanapaswa kuutambua mti kwa matunda yake si majani yanayoonekana na kutamanisha machoni.
Ukiifahamu kweli itakuweka huru, ni muhimu kuitafuta na kuifahamu kweli.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Imetolewa na;
Nape Moses Nnauye,
Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi.
15.06.2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment