Wednesday, February 22, 2012

IKULU ILIVYOJITOA SAKATA LA DK MWAKYEMBE KUWEKEWA SUMU!

OFISI ya Rais (Uhusiano na Uratibu), imejitenga na taarifa tata za ripoti kuhusu ugonjwa unaomsumbua Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe, kama unatokana na kulishwa sumu au la. Badala yake, Ikulu imezitaka wizara mbili zilizoibua mkanganyiko huo; Mambo ya Ndani ya Nchi na Afya na Ustawi wa Jamii, kukaa chini na kuondoa utata huo.
Akizungumza kwenye mahojiano na gazeti hili Dar es Salaam jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira, alisema Ikulu haina sababu ya kulizungumzia suala hilo kwa sasa. “Nataka unielewe, Ikulu hatuna statement (taarifa) ya suala hilo kwa sasa,” alisema Wasira alipotakiwa kuzungumzia utata ulioibuka siku za karibuni baada ya wizara hizo kutofautiana kwa kauli.


Wasira alisema ni mapema mno kwa Ikulu kuingilia mkanganyiko huo, kwa sababu inaamini wizara husika zina nafasi ya kufanya utafiti wa kutosha kuondoa mkanganyiko na kuwapa wananchi taarifa sahihi.Alienda mbali zaidi akisema waandishi wa habari bado wana nafasi ya kuwaondolea wananchi kiu ya kupata habari za kweli, iwapo watatumia uwezo wao zaidi kwa wizara hizo ili zitoe ukweli badala ya kuibana Ikulu.


“Msitake State House (Ikulu) ianze kulizungumzia suala hilo kwa sasa… bado nyie waandishi wa habari mna nafasi ya kulifanyia kazi zaidi na kupata ukweli,” alisema. Dk Mwakyembe alianza kuugua Oktoba mwaka jana na baadaye kupelekwa India kwa matibabu, ambako alikaa takriban miezi miwili na kurejea nchini Desemba mwaka jana.
Ugonjwa unaomsumbua Dk Mwakyembe umekuwa ukihusishwa na kulishwa sumu na mara kadhaa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amekuwa akishinikia uchunguzi makini kufanyika kwa vile kuna kila dalili za hujuma.
Wasira alisema iwapo waandishi watafanya uchunguzi wa kutosha kupitia wizara hizo wanaweza kupata taarifa sahihi juu ya jambo hilo.Hali hii ilitokana na Mkurugnzi wa Makosa ya Jinai, Robert Manumba, alitoa ripoti akisema uchunguzi wao unaonyesha ugonjwa unaomsumbua Dk Mwakyembe hautokani na kulishwa sumu.


Siku mbili baadaye, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda, aliiruka taarifa ya Manumba akimtaka aeleze alikoipata kwamba hakulishwa sumu. Wakati Wasira akizitaka wizara kuondoa mkanganyiko huo, Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, ameelezea kuchefuliwa na utata uliopo kwenye ripoti hizo kiasi kwamba hataki kusikia jambo hilo.


“Wala usiniulize kuhusu jambo hilo. Hilo suala wala sitaki kulisikia,” alisema Kombani na katika kuonyesha kuwa suala hilo linamchefua alikata simu alipoona anazidi kumbanwa. Habari hii imepatikana kwa msaada wa tovuti ya Gazeti la Mwananchi kwa habari zingine motomoto tembelea www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment