Tuesday, August 2, 2011

TAARIFA YA TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA YAZINDULIWA!

Jitihada zinahitajika katika kuhakikisha watoto wanapata malezi bora ili kujinusuru kujiingiza katika matukio ya uhalifu ambayo yanakinzana na sheria za nchi kufuatia Takwimu kuonyesha wazazi na walezi ndio chanzo kikubwa kinachochangia watoto kujiingiza katika matukio ya maovu.

Akizungumza katika Uzinduzi wa Taarifa ya Tume ya haki za binadamu na utawala, Mkurugenzi wa Utafiti na Nyaraka, EPIPHANIA MFUNDO amesema hatua ya mtoto kuhukumiwa kifungo iwe ya mwisho ili kuondokana na ukatili kwa watoto magerezani.


Aidha Mkuu wa kitengo cha Jinsia na watoto kutoka Jeshi la polisi, Bi ZUHURA MUNISI amesema usasa, uweledi na polisi jamii ndio itakayoweza kuwajenga watoto katika maeneo yao kwa kushirikiana na jamii.

VODACOM MISS TANZANIA 2011 KUINGIA KAMBINI TAREHE 8/8/2011!

Mkurugenzi wa Lino Internation Agency waandaji wa Miss Tanzania Hashimu Lundenga akiongea na kuwatambulisha baadhi ya warembo waliowahi kushiriki katika shindano la Vodacom Miss Tanzania miaka ya nyuma katika moja ya hafla jijini Dares Salaam.

Na Mwandishi Wetu
Lino Internation Agency chini ya Mkurugenzi wao Hashim Lundenga ambao ni waandaji wa shindano lenye hadhi ya kimataifa la urembo la Vodacom Miss Tanzania wametangaza rasmi jumla ya warembo thelathini (30) waliofanyikiwa kupata nafasi ya kushiriki katika shindano la Urembo la Vodacom Miss Tanzania 2011.

Warembo hawa wamepatikana baada ya kupitia ngazi mbali mbali za Mashindano ya Vodacom Miss Tanzania katika ngazi za chini, ikiwa ni pamoja na Vitongoji, Wilaya na Mikoa, na hatimaye ngazi ya Kanda, Jumla ya Kanda kumi na moja (11) zilishirikishwa katika Mashindano haya,alisema Lundenga


Alisema kambi ya shindano hili la "Vodacom Miss Tanzania 2011" inategemea kuanza siku ya Jumatatu ya tarehe 8 / 8 / 2011 jijini Dares Salaam. Lundenga alitoa wito kwa washiriki wote waliochaguliwa kwenye kambi hiyo kuripoti tarehe iliyotajwa hapo juu bila ya kukosa, katika ofisi za Miss Tanzania zilizopo mtaa wa Mkwepu saa 4.00 asubuhi.


Mkurugenzi huyo aliwataja warembo wanaotakiwa kufika kambini kuwa ni Chiaru Masonobo kutoka Dares Salaam,Zerulia Manoko,Maua Kimambo,Dalilah Ghalib,Christine Mwenegoha(kanda ya kati)Chritine William,Atu Daniel,Leyla Juma(Nyanja za juu kusini)Zubeda Seif,Stacey Alfred,Rose Hubert(kanda ya kaskazini)Husna Twalib,Cynthia Kimasha,Mwajab Juma(Kanda ya Temeke)Neema Mtitu,Weirungu David(Open University)Glory Lory,Blessing Ngowi(Higher Learning)Loveness Flavian,Asha Salehe,Mariaclara Mathayo,(Kanda ya Mashariki)Trace Sospeter,Irene Karugaba,Glory Samwel(Kanda ya Ziwa)Stella Mbuge,Husna Maulid,Hamisa Hussein(Kanda ya Kinondoni)Salha Israel,Alexia Willims,Jenifer Kakolaki(Ilala)


Nae Mkuu wa Udhamini wa Vodacom Tanzania Bw.George Rwehumbiza alisema kampuni yake ipo tayari kuwapokea warembo kwani mwaka huu wamejiandaa vya kutosha na wanatarajia kuyaweka mashindano haya ya urembo kuwa ya kimataifa zaidi kuendana na silogani ya Vodacom isemayo "Kazi ni Kwako"akimaanisha maandalizi yote yako vizuri kazi kubwa ni ni kwa warembo wenyewe tu kujiweka sawa na ili baadae waje kuipeperusha bendera ya Taifa letu kimataifa siku za usoni.


Lundenga aliongeza kwa kusema iwapo itatokea mshiriki kushindwa kufika kwa wakati na tarehe iliyotajwa hapo juu basi mshiriki huyo atakuwa amejiondoa mwenyewe katika Mashindano haya na nafasi yake kupewa mshiriki mwingine.

IDDI AZZAN AZUNGUMZIA MSONGAMANO WA MAGARI JIJINI DSM!

Licha ya juhudi inazofanya katika kutengeneza barabara nchini, Serikali imeombwa kushughulikia suala la msongamano wa magari Jijini Dar es Salaam kwa upendeleo mkubwa ili jiji hilo liendelee kutoa mchango katika kukuza uchumi wa Tanzania.

Mbunge wa Kinondoni Mheshimiwa IDD AZZAN amesema kwa kuwa Dar es Salaam imekuwa ikitoa karibia asilimia 80 ya pato la Taifa kuna kila sababu ya kuliongezea bajeti ya barabara ili liweze kukabiliana na msongamano wa magari unaoathiri ukuaji wa uchumi wake.


Kuhusiana fedha zitakazotumika kujenga barabara ya juu katika makutano ya barabara za Nyerere na Mandela Mheshimiwa AZZAN ametoa wito kwa serikali kutenga fedha za ndani badala ya kutegemea fedha kutoka kwa wahisani.

VOLCANO ZA VILELE VYA SHIRA NA MAWENZI MLIMA KILIMANJARO ZIMEKUFA!

Imebainika kwamba kadri miaka inavyokwenda ndivyo asili ya Mlima Kilimanjaro wenye vilele vitabu inapotea baada ya kuelezwa kuwa Volcano za vilele vya Shira na Mawenzi kufa na haziwezi kulipuka tena.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) DK TEREZYA LUOGA HUVISA amesema, tafiti mbalimbali za hivi karibuni zimebainisha volcano za vilele hivyo kufa na ile ya kilele cha Kibo imelala na kuna dalili bado ni hai.


Katika hatua nyingine Waziri HUVISA amesema kutokana na matukio ya milipuko ya hivi karibuni Wizara yake kwa kushirikiana na Shirika la Hifadhi za Taifa TANAPA inakusudia kutafuta wataalam wa milipuko ili kungalia uwezekano wa kulipuka tena.

MREMA AMSHUKIA CHIKU ABWAO KWA KUMWITA YEYE NI KIBARAKA WA CCM!

Mbunge wa Vunjo kupitia TLP Mheshimiwa AUGUSTINO LYATONGA MREMA amewaomba wabunge kujadili kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wao badala ya kuzungumzia masuala binafsi yasiyo na tija kwa taifa.

Akijibu tuhuma zilizotolewa na Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) CHIKU ABWAO bungeni kwamba yeye ni kibaraka wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa MREMA amesema hiyo ni kashfa na kwamba chama hicho hakihitaji msaada wowote kutoka kwake.


Katika hatua nyingine Mheshimiwa Mrema amebainisha kwamba ingawa baadhi ya wapinzani wanapinga uhuru wake wa kutoa maoni yeye haoni sababu ya kufanya hivyo kwani serikali iliyoko madarakani inatekeleza ahadi zake kama ilivyoahidi kwa wananchi wa Vunjo.

MAKAMU WA RAIS DKT BILAL ATEMBELEA NA KUKAGUA MRADI WA KILIMO CHA ZABIBU DODOMA!

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, na mkewe Mama Asha Bilal, wakifurahia ngoma ya asili kabira la Wagogo, wakati walipowasili Kijiji cha Chilangali (ii) Wilaya ya Chamwino Mkoa wa Dodoma leo Agosti 02, 2011 kukagua mradi wa kilimo cha Zabibu (FUNE) katika shamba hilo lenye ukubwa wa Hekari 300.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal na mkewe, wakiangalia Pikipiki aina ya Bajaj, aliyoizindua na kumkabidhi Mwenyekiti wa SACCOS ya FUNE, Jones Mazengo. Bajaj hiyo imetolewa na Benki ya CRDB ili itumike katika shughuli za kutembelea shamba la Mizabibu lililopo kijijini Chilangali (ii), likiwa na hekari 300 ambazo zinamilikiwa na wananchi.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi funguo ya Bajaj, Mwenyekiti wa SACCOS ya FUNE, Jones Mazengo baada ya kuzindua rasmi leo Agosti 02, Bajaji hiyo iliyotolewa msaada na Benki ya CRDB kwa ajili ya kutumika kwa shughuli za kutembelea shamba la Mizzabibu lililopo kijiji cha Chilangali (ii) Wilaya ya Chamwino mkoa wa Dodoma, likiwa na ukubwa wa hekari 300.Katikati ni Mama Asha Bilal.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal na mkewe, Mama Asha Bilal, wakiangalia Bwawa la kuhifadhia maji ya kumwagilia mashamba ya Zabibu, wakati walipowasili Kijiji cha Chilangali (ii) Wilaya ya Chamwino Mkoa wa Dodoma leo Agosti 02, 2011 kukagua mradi wa kilimo cha Zabibu (FUNE) katika shamba hilo lenye ukubwa wa Hekari 300. Picha na Muhidin Sufiani-OMR.

RAIS WA UGANDA AKAMILISHA ZIARA YAKE NCHINI RWANDA!

Rais wa Uganda Yoweri MuseveniSerikali za Rwanda na Uganda zimekubaliana kushirikiana kwenye nyanja mbalimbali za maendeleo. Maazimio hayo yamefikiwa na pande mbili kwenye kilele cha ziara ya siku nne ya Rais wa Uganda Yoweri Museveni nchini Rwanda.
Ziara ya Rais Museveni licha ya kujikita katika ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo, imekuwa ikitazamwa na wadadisi kama inayofungua ukurasa mpya wa uhusiano wa nchi hizo ambao ulikuwa umedorora kwa muongo mmoja uliopita.


Waziri wa mashauri ya kigeni wa Rwanda Louise Mushikiwabo ndiye aliyelisoma tangazo la pande mbili lililotiwa saini na mawaziri wa mashauri ya kigeni wa Rwanda na Uganda. Tangazo hilo linaainisha sehemu ambazo nchi hizo zitashirikiana, ikiwa ni pamoja na uchumi, sayansi na teknolojia na hifadhi ya mazingira. Punde tu marais hao wakaanza mazungumzo na waandishi wa habari.


                             Madai ya mvutano kati ya Rwanda wa Uganda yapuuzwa
Waandishi wa habari walikuwa na shauku ya kujua ukweli wa jitihada za marais hao kuondoa tofauti zao ambazo zimekuwa zikiendelea ingawa chini kwa chini kwa takribani muongo mmoja uliopita. Hata hivyo marais wote walionekana kupuuza ikiwa kumekuwepo na mgogoro wowote, huku wakisisitiza kuwa nchi za Rwanda na Uganda zimekuwa na mafungamano ya kihistoria.

NIMEKUBALI HARUNA MOSHI HANA NIDHAMU - KOCHA WA STARS

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Taifa ‘Taifa Stars’ Jan Poulsen(pichani mwenye kofia) amekerwa na tabia ya utovu wa nidhamu iliyooneshwa na mchezaji Haruna Moshi ‘Boban’ ya kushindwa kuripoti katika kambi ya timu ya vijana ya chini ya miaka 23 iliyokuwemo jijini Arusha.

Poulsen aliwaita wachezaji watatu Gaudence Mwaikimba, Juma Seif ‘Kijiko’ na Boban kuja jijini Arusha kucheza michezo miwili ya kirafiki kati ya Vijana Stars na Shelisheli ili aangalie uwezo wao kama anaweza kuwaita katika kikosi cha Taifa Stars.


Akizungumza na waandishi wa habari mjini Arusha jana, Poulsen alisema ni mchezaji mmoja tu aliyeitikia mwito huo ambaye ni Kijiko, huku Mwaikimba akitoa taarifa kuwa ni mgonjwa lakini Boban hakukuwa na taarifa zozote juu yake.

Kocha huyo raia wa Denmark alisema, wakati wanaondoka Dar es Salaam mchezaji huyo alisema atakuja na usafiri wake binafsi lakini hadi sasa haijulikani alipo.


“Sijawahi kumwona Boban akicheza lakini niliambiwa ni mzuri na pia niliambiwa kuwa ni mchezaji ambaye hana nidhamu na kweli nimeliona hilo mwenyewe,”alisema.

WACHUUZI 10,000 WAPOTEZA MALI BAADA YA SOKO KUU KAMPALA KUUNGUA!

Wachuuzi kama elfu kumi katika soko kuu la Owino mjini Kampala, wamepoteza mali zao zilizoteketea kwenye moto uliotokea Jumapili alfajiri. Hii ni mara ya pili moto kutokea hapo katika kipindi cha miaka miwili. Polisi walisema wanachunguza tukio hilo.
Salim Uhuru diwani wa mtaa huo alisema "hii ni mara ya pili soko limeshika moto. Ripoti ya polisi ya kwanza bado haijatoka na sasa moto umetokea mara ya pili. Hatujui kama moto umetokana na stima, au walichoma au jambo la kawaida. Hatujui."


"Lakini tunaomba wachuuzi warudi sokoni kwa sababu habari tulizopata ni kuwa watu wameshanunua ardhi hii. Na wakinunua ardhi hii, kutufukuza wanachochoma vitu vya watu," aliongeza. "Lakini sisi kama madiwani wa eneo hili, tumewaambia wachuuzi warudi katika maduka yao. Hakuna mtu aliyewahi kuokoa mali yake. Yote imeungua."

ZOMBE AMTUHUMU LEMA KUHUSIKA NA MTANDAO WA WIZI WA MAGARI!

Aliyewahi kuwa mkuu wa upelelezi wa mkoa wa DSM ABDALAH ZOMBE ameibua tuhuma dhidi ya mbunge wa ARUSHA mjini GODBLESS LEMA zikiwa zimepita siku chache baada mbunge huyo kuhoji bungeni namna kesi ilivyokuwa ikimkabili ZOMBE ilivyoendeshwa.

Bwana ZOMBE alizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama Kuu ya Tanzania hapo jana. Aidha zombe amedai kuwa wakati alipokuwa mkuu wa upelelezi mkoa wa DSM alipata taarifa kuwa Bwana LEMA ana mtandao wa wizi wa magari kutoka Tanzania na kuyapeleka Kenya.


Hata hivyo Mbunge wa ARUSHA mjini Bwana GODBLES LEMA amekanusha kuhuisna na madai hayo ya wizi wa magari.

MAITI AAMKA AFRIKA KUSINI NA KUANZA KUPIGA KELELE MONCHWARI!

Raia mmoja wa Afrika Kusini aliamka akajikuta yupo kwenye chumba cha kuhifadhia maiti mwishoni mwa juma, na akaanza kupiga kelele akitaka atolewe- akiwatisha wahudumu wakidhani ni mzimu.
Familia yake ilidhani amekufa baada ya kushindwa kumwamsha Jumamosi usiku na kuwasiliana na ofisi moja yenye vyumba vya kuhifadhia maiti ya mtu binafsi katika kijiji kimoja mjini Eastern Cape.


Alikuwepo kwenye chumba hicho kwa muda wa saa 24, msemaji wa idara ya afya mjini humo aliliambia shirika la habari la Sapa. Wahudumu hao baadae walirejea na kupiga simu kuita gari la wagonjwa. Mtu huyo ambaye jina lake limehifadhiwa, alitibiwa hospitalini kwa kukosa maji mwilini. Msemaji wa idara ya afya ya Eastern Cape Sizwe Kupelo alisema, "Daktari walimfanyia uchunguzi na kuona kuwa anaendelea uzuri."


"Hakuhitaji matibabu ya ziada." Bw Kupelo alisema mtu huyo aliamka saa tisa za Afrika Mashariki siku ya Jumapili, akitaka kutolewa kwenye chumba hicho chenye baridi kali kwenye kijiji cha Libode, na kuwatisha wahudumu waliokuwa zamu. Bw Kupelo alisema, "Mwanzo watu hao walikimbia kwa kasi." Maafisa wameusihi umma kuwasiliana na madaktari au wanaotoa huduma za dharura ili waweze kumtangaza mtu kufariki dunia kabla ya kuwaita wahudumu wa vyumba vya kuhifadhi maiti.


Bw Kupelo alisema, "Unaanza kujiuliza ni watu wengine wangapi waliokufa kwa namna hiyo katika chumba cha kuhifadhia maiti."