Monday, August 29, 2011

MBUNGE WA SINGIDA MJINI ASIKITIKIA KUTOTUNZWA KWA VISIMA VYA MAJI ALIVYOSAIDIA!

                                          Mbunge wa SINGIDA Mjini Mohammed Dewji
Na Mwandishi wetu.

Mbunge wa SINGIDA Mjini Mohammed Dewji, amesikitikia hali ya visima alivyotengeneza kwa gharama kubwa katika kata mbalimbali mkoani humo, ambavyo vimeharibiwa kwa uzembe wa wananchi wenyewe. Akizungumza Ofisini kwake wakati wa kujibu hoja iliyotolewa na baadhi ya wanasingida, kwamba visima vilivyochimbwa kwa sasa havitoi maji , Mbunge huyo amesema, jukumu la kusimamia visima hivyo ni la wananchi wenyewe na kwamba amehuzunishwa kwa kupewa lawama asizostahili pamoja na msaidizi wake.


Mh. DEWJI ameongeza kuwa, wakati anazindua visima hivyo vilivyogharimu zaidi ya milioni Mia Tano zilizotoka kwake binafsi, alitoa maelekezo kwa wakazi wa sehemu husika kuunda kamati ambazo zingesimamia na kuweza kuchangisha kiasi kidogo kwa lengo la kuwezesha linapotokea tatizo kufanya ukarabati au marekebisho.


“ Mimi jukumu langu lilikuwa ni kuwachimbia visima ili kuwaondoa na tatizo la maji, lakini niliwaambia wachague kamati maalum itakayokuwa na mfuko maalum wa kuchangisha japo shilingi Ishirini kwa watumiaji wa maji ili waweze kutatua lolote linaloweza kutokea.” Aidha amesema,kwa kawaida wananchi hao walipaswa kuchangia maendeleo yao kwa asilimia Tano na yeye kutoa gharama nyingine, lakini kwa upendo wake aliamua kuingia gharama yote kwa ajili ya wananchi hao ambao walipaswa kuthamini jitihada zake hizo badala ya kumlaumu.


“Unajua kwa kawaida wananchi wanatakiwa kuchangia asilimia Fulani na mimi kama mbunge nichangie iliyobakia, lakini ingechukua muda mrefu kutimiza hilo, hivyo niliamua kutoa fedha zote kwa kazi hiyo ambayo pia ni jukumu la serikali, ila kwakuwa tatizo limeshatokea nitahakikisha linatatuliwa.” Katika hoja hiyo ilidai kuwa Mbunge huyo amekuwa na jitihada za kusaidia wananchi wake lakini kumekuwepo na mapungufu ya usimamizi kwa upande wa wasaidizi wake mkoani SINGIDA jambo ambalo Bwana DEWJI amewataka hao wanaotoa madai hayo kuwa wawazi, na kusisitiza kutokuwa sababu ya kujichukulia hatua mikononi .


Visima ambavyo vinalalamikiwa kuwa kwa sasa havitoi maji ni pamoja na Mtamaa na Unyianga mkoani humo. Na wakati huo huo naye Msaidizi wa Mbunge huyo ametoa ufafanuzi juu ya tatizo kwa kudai kuwa Tatizo la kutotoa maji kwenye visima hivyo linatokana na uongozi wa maeneo hayo ,ambao haukuweka udhibiti na usimamizi kama walivyotakiwa na mheshimiwa Mbunge Dewji tofauti na maeneo mengine ambayo visima vyao tangu vizinduliwe vimekuwa vikitoa maji bila ya matatizo.


Amesema, sababu kubwa kwa maeneo ya visima visivyotoa maji , ni pamoja na kuwaacha watoto wadogo wakichezea visima hivyo, sambamba na kutokuwa na utaratibu Wa ulinzi na uongozi Wa wateka maji.

No comments:

Post a Comment