Sunday, May 15, 2011

MBUNGE WA UGUNGO JOHN MNYIKA KUANZA MATENGENEZO BARABARA YA MBEZI MAKABE.

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika amesema kwamba matengenezo maalum ya barabara ya Mbezi mpaka Makabe kupitia Lubokwe na mji mpya yataanza mwezi huu mara baada ya kupungua kwa mvua zinazoendelea hivi sasa.

Mnyika aliyasema hayo juzi (8/5/2011) akizungumza katika mkutano wa wananchi wa Mtaa wa Mbezi Luis uliofanyika katika eneo la Kona ya Miembesaba.
Mnyika amesema matengenezo hayo ambayo yanatarajia kugharimu takribani milioni 170 yametokana na malalamiko ya muda mrefu ya wananchi wa Mbezi Makabe kuhusu ubovu wa barabara hiyo.
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Barabara Mtaa wa Mbezi Luis, Samwel Kirama alimshukuru mbunge kwa kushiriki katika mkutano huo na kumweleza kwamba fedha kutoka mradi wa TASAF awamu ya pili cha shilingi milioni 28 zimeingizwa katika akaunti ya mradi kwa ajili ya ujenzi wa barabara nyingine katika eneo hilo.
Kirama alisema kwamba fedha hizo zitatumika kufanya ukarabati wa barabara ya Mazulu mpaka Kwa Kidevu kupitia Miembesaba kwa kiwango cha changarawe pamoja na kuweka mifereji ili barabara iweze kupitika katika vipindi vyote.
Mkutano huo uliazimia kwamba ramani ya ujenzi wa barabara hiyo ijulikane kwa wakazi wote ili kutoa ushirikiano katika maeneo ambayo yanagusa miti na kuta kutokana na ujenzi holela.
Aidha mkutano huo wa wananchi ulikubaliana kwamba tathmini ya maeneo ya barabara ya mbele ya mradi huo iendelee ili kuweza kujua mahitaji kwa ajili ya kutafuta vyanzo mbadala kwa kadiri iwezekanavyo.
Diwani wa Kata hiyo, James Kajale aliahidi kufuatilia Manispaa ya Kinondoni kuhusu uwiano kati ya matumizi nguvu kazi na suala la ufanisi wa utekelezaji wa mradi ili hatua za ujenzi zianze mapema.

No comments:

Post a Comment