Monday, May 16, 2011

KIJANA MWENYE MATATIZO YA AKILI AUA WAZAZI WAKE WAWILI!

                                   Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Bibi.Celina Kaluba
KIJANA mmoja anayesadikiwa kuwa na matatizo ya akili, amewaua wazazi wake wote wawili Mkoani Singida, baada ya kuwajeruhi kwa kuwakata na panga kwenye sehemu mbalimbali za miili yao, kabla ya kutiwa mbaroni na Polisi.



Kamanda wa polisi mkoa wa Singida, kamishina msaidizi mwandamizi Bibi.Celina Kaluba amesema kuwa, tukio hilo limetokea jana jumapili, saa 1: usiku, katika Kijiji cha Ngimu, halmashauri ya Wilaya ya Singida.


Kaluba amewataja waliouwa katika tukio hilo kuwa ni, mzee Erasto Kilakuno na mkewe Frida Dule , ambao wote ni wazazi wa mtuhumiwa huyo aliyejulikana kwa jina la Raymond Erasto ,wote wakazi wa kijiji cha Ngimu.


Amesema siku ya tukio jioni, ghafla mtuhumiwa huyo alipandwa ghadhabu kutokana na kinachosadikiwa kuwa ni kichaa, akachukua panga na kuanza kuwajeruhi wazazi wake mmoja baada ya mwingine katika sehemu mbalimbali za miili yao.


Kaluba amesema licha ya kupiga kelele za kuomba msaada, lakini juhudi za majirani kuwapeleka hospitalini hazikuzaa matunda, baada ya wazee hao kupoteza maisha muda mfupi kutokana na kuvuja damu nyingi kwenye majeraha yao.


Mtuhumiwa anashikiliwa na polisi kwa upelelezi zaidi ikiwemo kupelekwa hospitalini kwa ajili ya kupimwa akili zake, kisha atapandishwa kizimbani kujibu shitaka la mauaji na kujeruhi.

No comments:

Post a Comment