Sunday, July 15, 2012

MATARAJIO YA SERIKALI KATIKA SENSA YA WATU NA MAKAZI MWAKA 2012!



Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi akisisitiza jambo wakati akifunga mafunzo ya siku saba kwa wakufunzi wa Sensa ngazi ya Taifa Mjini Dodoma.



Na Mwandishi WetuSerikali inatarajia kuwa zoezi la sensa ya watu na makazi litakalofanyika kwa muda wa siku saba kuanzia Agosti 26 mwaka huu litakuwa la mafanikio makubwa katika kupata taarifa na takwimu mbalimbali. Taarifa na takwimu hizo zitatumika kama moja ya mtaji katika kupanga, kutekeleza, na kusimamia mipango na mikakati mbalimbali ya maendeleo kwa mustakabali wa nchi.


Hayo yalisemwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi alipokuwa akifunga mafunzo ya siku saba kwa wakufunzi wa Sensa ya Watu na Makazi ngazi ya Taifa yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano Chuo cha Mipango mjini Dodoma.


Dr. Nchimbi aliwataka watendaji na viongozi wote watakaoendesha na kusimamia zoezi la Sensa kutotekeleza zoezi hili kwa malengo na matakwa yao binafsi yakiwemo ya kisiasa bali wakumbuke kuwa kila zoezi la Sensa linaloandaliwa na kuendeshwa na serikali linakuwa na malengo yake maalumu ya kuiwezesha serikali kupata taarifa na takwimu sahihi zitakazoiwezesha kupanga na kutekeleza mipango yake mbalimbali sawasawa na mahitaji halisi.


Akizungumza na wakufunzi hao wa Sensa ya Watu na Makazi ngazi ya Taifa, Dr. Nchimbi aliwasisitizia kuwa watakapotenda sawasawa na matakwa yao binafsi watakuwa hawaitendei haki serikali na wananchi kwa ujumla kwani serikali imewapa dhamana kubwa sana hivyo wanatakiwa kuibeba na kutenda sawasawa na dhamana hiyo waliyopewa na matarajio ya wananchi wote kwa ujumla.


Akitoa maelezo juu ya mafunzo hayo ya siku saba kwa wakufunzi wa Sensa ngazi ya Taifa Mkurugenzi Mkuu Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dr. Albina Chuwa alibainisha kuwa jumla ya wakufunzi 150 wamefunzwa ipasavyo katika nadharia na vitendo kwa ajili ya kwenda kufanya kazi ya Sensa lakini pamoja na mafunzo hayo wakufunzi hao wamefanya mtihani wa nadharia na vitendo na majibu yatatolewa, kwa wale watakaofaulu watakwenda kufanya kazi ya Sensa na kwa wale watakaoanguka kwenye mitihani hiyo hawataruhusiwa kufanya kazi ya Sensa.


Vilevile aliwataka wakufunzi hao kulipa zoezi la Sensa uzito wa kipekee na umakini mkubwa kwani zoezi hili ni muhimu sana kwa nchi yetu na serikali inaingia gharama kubwa sana kuendesha zoezi la Sensa hivyo hawana budi kuhakikisha kazi inafanyika kama ilivyopangwa na matokeo yaliyotarajiwa yanapatikana na kuwa mafanikio ya zoezi la Sensa yatabainika katika zoezi la utoaji taarifa na takwimu za awali juu ya zoezi la Sensa hapo mwezi Disemba.

No comments:

Post a Comment