TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UTEUZI WA MWISHO WA MGOMBEA WA CHADEMA KATIKA BUNGE LA AFRIKA MASHARIKI
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia Kurugenzi ya Habari na Uenezi, kinatoa taarifa kwa umma kuwa mchakato wa kumpata mgombea Ujumbe Bunge la Afrika Mashariki (EALA) umekamilika na uteuzi umefanyika leo, Aprili 9, 2012.
Katika uteuzi huo ulioamuliwa kwa kura za wajumbe, Ndugu Antony Ecalit Komu aliweza kuwashinda wenzake wengine tisa, kwa kupata zaidi ya asilimia 50 katika mzunguko wa pili, baada ya wagombea wote kushindwa kukidhi kigezo cha katiba ya chama kuwa mshindi lazima apate asilimia 50 ya kura za wajumbe wa mkutano husika wa uteuzi.
Wagombea ambao majina yao yalipigiwa kura katika mzunguko wa kwanza ni pamoja na Godfrey Mnubi, Edgar William Chibura, John Simon Malanilo, Patrick Lubango Nkandi, Anna E. Maghwira, Deogratias George Assey, Pasquina Ferdinand Lucas, Deusdedit Jovin Kahangwa, Antony Calist Komu na Mwantum Khamis Mgonja.
Katika mzunguko wa pili, mchuano ulikuwa kati ya Mghwira, Malanilo na Komu. Baada ya kura, Komu aliibuka mshindi kwa kupata asilimia zaidi ya 50 ya kura zote zilizopigwa.
Uteuzi huo wa mwisho wa kupata mgombea wa EALA kwa tiketi ya CHADEMA umefanyika baada ya kukamilika kwa hatua zote za awali ikiwemo uchukuaji na urejeshaji fomu za wagombea waliojitokeza kuwania nafasi hiyo.
Itakumbukwa kuwa Machi 12, 2012 Katibu wa Bunge alitoa Taarifa kwa Umma kwamba, Uchaguzi wa wajumbe tisa (9) watakaoiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki utafanywa na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, wakati wa Mkutano wake wa Saba utakaofanyika Dodoma, kuanzia tarehe 10 hadi 20 Aprili, 2012.
Uchaguzi huo wa Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki unafanyika kwa kuzingatia kuwa maisha ya Bunge hilo lililoingia madarakani mwaka 2006 yatafikia ukomo wake 04 Juni, 2012.
Taarifa imetolewa kwa vyombo vya habari na:
Tumaini Makene
Afisa Habari wa CHADEMA
Aprili 9, 2012
No comments:
Post a Comment