Tuesday, April 10, 2012

Taarifa kwa Vyombo vya Habari

                                                      
                                                           TAARIFA KWA UMMA

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinatoa taarifa kwamba maoni binafsi ya viongozi na wanachama wasiokuwa na mamlaka kwa mujibu wa katiba, kanuni na itifaki ya chama kuwa wasemaji wakuu wa masuala ya chama katika ngazi husika yasichukuliwe kuwa ni msimamo wa CHADEMA.

CHADEMA kinatoa taarifa hii kufuatia maoni binafsi ya muasisi na mwenyekiti mstaafu wa CHADEMA juu ya wajumbe wa tume ya mabadiliko ya katiba yanayoelezwa kutolewa katika mtandao wa jamii wa Jamii Forums kutafsiriwa kuwa ni msimamo wa CHADEMA.

CHADEMA kinatoa mwito kwa wachangiaji katika mitandao ya kijamii na wananchi kwa ujumla kuzingatia kuwa CHADEMA bado haijatoa kauli juu ya wajumbe wa tume husika kwa kuwa bado CHADEMA inaendelea kufanya uchambuzi juu ya wasifu wa wajumbe wa tume husika na mchakato wa uteuzi wao kama tulivyoeleza kwenye taarifa kwa umma tuliyotoa tarehe 7 Aprili 2012.

Hata hivyo, izingatiwe kwamba uchambuzi wa wasifu wa wajumbe walioteuliwa kwenye tume husika unaoendelea kufanywa na CHADEMA hauhusu dini za wajumbe wa tume kwa kuwa CHADEMA hakiamini katika udini bali unahusu uwezo na uadilifu wa wajumbe husika na iwapo umezingatia matakwa ya umma na dhamira ya kujenga muafaka wa kitaifa wa kuwa na katiba mpya na bora.

Izingatiwe pia kwamba kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA ibara ya 3B kifungu cha 3.1.9 ikiwa ni sehemu ya misingi iliyopo kwenye itikadi ya CHADEMA ya mrengo wa kati, CHADEMA inaamini katika umuhimu wa uhuru wa kuamini katika kujenga maadili ya mwanajamii mmoja mmoja bila kuifanya dini kuwa sehemu ya dola na na misingi mingine ya CHADEMA ya kujenga chama na taifa lenye kutoa fursa kwa kuzingatia uwezo na uadilifu bila kujali tofauti zingine.

Pamoja na kujulisha umma kwamba CHADEMA kinaendelea kufanya uchambuzi wa wajumbe walioteuliwa kwenye tume husika, tulieleza kuwa CHADEMA kilitarajia kwamba Rais Jakaya Kikwete angeeleza pia ratiba ya kufanyika kwa marekebisho mengine muhimu ya awamu nyingine kuhusu bunge maalum la katiba na hatua ya kutunga katiba mpya na usimamizi wa kura ya maoni itakayowezesha wananchi kufanya maamuzi kwa uhuru na kwa haki kabla ya mchakato kufikia katika hatua husika.

Tunasisitiza umuhimu wa Serikali kutoa kauli kwa umma kuhusu ratiba ya marekebisho ya awamu nyingine ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 kwa kuzingatia kuwa Ofisi ya Bunge imetangaza kuwa Mkutano wa Bunge utaanza tarehe 10 Aprili 2012 bila marekebisho ya sheria ya katiba kuwa sehemu ya orodha ya miswada ya sheria inayotarajiwa kujadiliwa katika mkutano wa saba wa Bunge.

Tunarejea kuutarifu umma kuwa Kamati Maalum ya Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) iliyoundwa tarehe 20 Novemba 2011 kwa ajili ya kukutana na Rais Jakaya Kikwete kuhusu sheria ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011 itafanya kikao chake karibuni mara baada ya uchambuzi kukamilika kupitia taarifa ya uchambuzi unaofanywa juu ya uteuzi uliofanyika wa wajumbe wa tume na tamko litatolewa kwa umma kuhusu mchakato huu muhimu kwa maslahi ya taifa.



Imetolewa tarehe 09 Aprili 2012 na:



John Mnyika (Mb)

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi

No comments:

Post a Comment