Rose Muhando
Na Mwandishi Wetu
MALKIA wa muziki wa Injili nchini, Rose Muhando, naye atakuwa miongoni mwa waimbaji watakaopamba tamasha la nyimbo za Injili litakalofanyika Aprili 8 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Kwa mujibu wa Alex Msama, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati inayoratibu tamasha hilo chini ya Kampuni ya Msama Promotions ya Dar es Salaam, Muhando amethibitisha kushiriki tamasha hilo.
"Katika tamasha la Pasaka mwaka huu ndipo Rose Muhando atapata fursa ya kutambulisha albamu yake ya nne ya Utamu wa Yesu ambayo haijawahi kuzinduliwa tangu aikamilishe," alisema Msama. Albamu ya Utamu wa Yesu inabeba nyimbo saba ambazo ni Utamu wa Yesu uliobeba jina la albamu hiyo, Raha Tupu, Tamalaki, Ndivyo Ulivyo, Woga Wako, Imbeni na Kusifu na Achia. Mbali na Utamu wa Yesu, Rose Muhando pia amewahi kutamba na albamu za Uwe Macho, Nyota ya Ajabu (Zawadi ya Krismasi) na Jipange Sawa Sawa.
Msama alisema pia Muhando ataimba pamoja na Anastazia Mukabwa wa Kenya aliyeshirikiana naye katika albamu ya Vua Kiatu, na baada ya kutikisa Uwanja wa Taifa, mashambulizi mengine yatahamia kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma Aprili 9 mwaka huu. "Mpaka sasa tunaendelea na mazungumzo na waimbaji wengine mahiri wa muziki wa Injili, lakini Muhando atakuwepo na Mukabwa atakuja na kundi la waimbaji wake," alisema Msama.
Albamu ya Vua Kiatu inabeba nyimbo nane ambazo ni Vua Kiatu uliobeba jina la albamu hiyo, Ee Mungu, Usiwe Manamba, Nzizilela, Nishike Mkono Bwana, Wanaokudharau na Mfalme. Mbali na Mukabwa, wengine waliothibitisha kushiriki tamasha hilo litakalofanyika Sikukuu ya Pasaka ni Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Christina Shusho wa Dar es Salaam, kundi la Glorious Celebration na Atosha Kissava kutoka Iringa.
Kwa mujibu wa Msama, tamasha hilo baada ya kufanyika Dar es Salaam, pia litarindima kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Aprili 9 mwaka huu. Tamasha la mwaka huu malengo yake makubwa ni kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwasomesha watoto yatima na kuwasaidia mitaji wanawake wajane. Kiingilio katika tamasha hilo kimetengwa katika kategoria tatu na kitakuwa sh. 2,000 kwa watoto, sh. 5,000 kwa viti vya kawaida na viti maalumu sh. 10,000.
Tamasha la Pasaka la mwaka huu pia litashirikisha waimbaji wa nyimbo za Injili kutoka nchi sita za Afrika ambazo ni Kenya, Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Afrika Kusini na Zambia. Pia kutakuwa na kwaya. Picha na FULLSHANGWE!
No comments:
Post a Comment