MGOMO wa madaktari umeanza rasmi katika baadhi ya hospitali za wilaya mkoani Dar es Salaam na Hospitali ya Rufaa Bugando, huku katika mikoa mingine hali ikiwa shwari na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili huduma zikitolewa kwa kusuasua.
Hata hivyo, madaktari wamedai mgomo huo utaendelea nchi nzima hadi Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda na Naibu wake, Dk. Lucy Nkya watakapojiuzulu. Mgomo huo pia utanogeshwa ama kuungwa mkono na mkugomo wa madaktari bingwa kutoka hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Muhimbili pamoja na hospitali za Wilaya huku pia ukitarajiwa kusambaa nchi nzima.
RAIS wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Namala Mkopi, amesisitiza kuendelea na mgomo nchi nzima.Akizungumza katika Mkutano wa Madaktari waliokutana kwenye ukumbi wa Kituo cha Utamaduni cha Urusi, jijini Dar es Salaam, Mkopi alisema, wamepata taarifa kutoka kikao cha madaktari bingwa cha jana asubuhi kuwa nao wanaungana nao katika mgomo huo.
Mkopi alisisitiza kuwa masuala mengine yanazungumzika wao wakiwa kazini, lakini hawatarejea mpaka mawaziri hao wawili watakapowajibika au kuwajibishwa.Walipoulizwa kuvuta subira kabla ya kuchukua uamuzi huo mgumu, Mjumbe wa MAT, Godbless Charles, alisema Waziri Mkuu katika mkutano nao, aliwaahidi kuisafisha
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, baada ya kuwasimamisha kazi Katibu Mkuu Blandina Nyoni na Mganga Mkuu, Deo Mtasiwa.
“Tumesubiri kwa mwezi mmoja kwani ingekuwa mshahara wangesema wanasubiri bajeti au ingekuwa inataka utafiti,“ alisema. Alisisitiza kuwa walielewa msimamo wa Pinda jana (juzi), lakini siku ya kikao nao angetoa msimamo wa jana (juzi) kuhusu mawaziri hao wangemwelewa vizuriUtafiti uliofanywa na katika hospitali ya Muhimbili, Amana, Temeke na Mwananyamala, ulionesha katika baadhi ya hospitali wagonjwa walitakiwa kusikiliza vyombo vya habari kisha warejee watakaposikia kuwa mgomo umekwisha.
Amana, Katibu wa Madaktari wa Hospitali hiyo, Dk. Shani Mwaluka, alithibitisha kuwapo kwa mgomo na kusema hali ni mbaya, kwani wamegoma madaktari wengi walioajiriwa na walioko katika mafunzo kwa vitendo.Alisema wameamua kuwarudisha nyumbani wagonjwa ambao hawako katika hali mbaya na madaktari waliobaki wanawahudumia walio katika hali mbaya zaidi.
“Mgomo huu ni tofauti na wa awali kwani sasa wamegoma madaktari wengi hata wale walioajiriwa, kwani asubuhi walifika na kusaini lakini wakaondoka,” alisema. Alisisitiza kuwa wanaendelea kujipanga kuhakikisha huduma zinaendelea kwa waliopo kwa madhumuni ya kuhudumia walio katika hali mbaya zaidi.
Katika hospitali hiyo, wagonjwa walikuwa wakifika katika dirisha la Mapokezi na kuelezwa kuwa madaktari wamegoma, hivyo waende katika vituo vya afya vingine vilivyo karibu na kwao. Temeke, wagonjwa walitakiwa kurudi majumbani hadi watakaposikia kwenye vyombo vya habari kuwa mgomo umemalizika.
Mmoja wa wauguzi katika hospitali hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema ni historia katika hospitali hiyo, kwani haijawahi kuwa na mgomo lakini huo ulioanza jana walishangaa kutoona madaktari. HABARI KWA HISANI YA HABARILEO.
No comments:
Post a Comment