Friday, August 5, 2011

VODACOM KUFURAHIA RAMADHANI NA MAKUNDI MAALUM!

Katika kuendeleza utamaduni wa kujali makundi mbalimbali ya kijamii nchini mfuko wa kusaidia jamii wa kampuni ya mawasiliano Vodacom Tanzania" Vodacom Foundation" unazindua rasmi kampeni yake ya share and care kwa ajili ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Kampeni hiyo ambayo ni utamaduni wa kila mwaka wa kampuni hiyo kupitia kitengo chake cha"Vodacom Foundation" hufanywa nyakati za siku kuu kubwa za kidini ikiwemo Ramadhani na Krisimasi ambapo makundi mbalimbali ya kijamii yasiyojiweza hupatiwa chakula na vitu vingine mbalimbali ili kuwafanya kuwa wenye furaha na kuwapunguzia upweke.


"Mwaka huu Ramadhani share and care inazinduliwa Mafia Jumamosi Agosti 6, 2011 ambapo kama ilivyo desturi itakuwa na fursa ya kupata futari pamoja na watoto yatima na wazee wasio na uwezo hususan wajane na baada ya hapo tutaendelea na kampeni hii katika mikoa mbalimbali nchini"Alisema Mkuu wa Mfuko huo Bw.Yessaya Mwakifulefule.


Vodacom Foundation itatumia kiasi cha shilingi milioni hamsini kuwafikia waislamu kwenye maeneo mbalimbali kwa lengo la kuwafuturisha na kuwapatia sadaka ya vyakula. Azma ya Vodacom Foundation kufuturisha makundi yenye uhitaji maalum ni kuwafanya kuwa na furaha wakati huu wa mwezi mtukufu na kufurahia ibada ya swaumu na pia hulenga kuwaweka pamoja wanajamii wa makundi hayo na kuwafanya kuwa kitu kimoja huku ikiwapa fursa ya kujenga undugu miongoni mwao.


"Tumekuwa tukifanya hivi tangu mwaka 2007 na tunafurahia kuwa na kampeni ya aina hii ambayo ni ya kipekee kwa makampuni hapa nchini ni sehemu ya kuonesha utu na kujali kwetu kwa vitendo kila mmoja tunamjali kwa wakati wake hii ikimaanisha wakristo wakati wa Krismasi na waislamu kwa Ramadhani, tunadhani ni jambo jema na tunajivunia"Aliongeza Mwakifulefule

Mbali na kupata futari kwa pamoja Vodacom Foundation hutumia wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani kutoa sadaka ya vyakula na vitu mbalimbali kwa vituo vya watoto yatima na kwa makundi mengine ya wasiojiweza wakiwemo wajane na wazee.Baada ya uzinduzi wa Mafia kampeni hiyo itagusa mikoa ya Arusha,Mwanza na Pemba na inatarajiwa kutoa faraja kubwa kwa waumini wa kiislamu wasiojiweza katika maeneo yatakayoguswa na kampeni hiyo ambao kwa sasa wanatekeleza ibada ya swaumu.


Waumini wa kiislamu nchini wameanza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani Agosti Mosi mwaka huu. Uongozi na wafanyakazi wa Vodacom Tanzania unawatakia kheri na fanaka tele katika kipindi chote cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.

No comments:

Post a Comment