Friday, May 13, 2011
CHADEMA YAMWEKA HATARINI KIKWETE!
• MBOWE: TUTAENDELEA KUKOMAA NAO HADI KIELEWEKE
NA Edward Kinabo, Songea
Freeman Mbowe na Mohamed Dewji (MO)
BAADA ya kuiteka miji na vijiji vya mikoa ya Mbeya, Rukwa na Katavi, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), jana kiliuteka mji wote wa Songea, mkoani Ruvuma kwa maandamano na mkutano wa hadhara, huku viongozi na wanasiasa kadhaa wa chama hicho wakionya kuwa Rais Jakaya Kikwete anaweza kung’olewa kabla ya mwaka 2015.
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, akihutubia maelfu ya wakazi wa mji wa Songea alisema sasa chama hicho kina uhakika wa kuchukua nchi wakati wowote ikiwa Rais Jakaya Kikwete hatachukua hatua za dharula kupunguza makali ya maisha na kuwapa wananchi uhuru wa kutengeneza katiba yao.
Alisema hatua ya serikali ya CCM kunywea na kuanza kujadili Katiba mpya ambayo waliipinga wakati wa kampeni, ni dalili tosha kuwa umma wa Watanzania chini ya muongozo wa CHADEMA unaweza kujiletea neema muda wowote ukitaka.
Alisema badala ya kusubiria miaka mitano CHADEMA tayari imeanza kazi ya makusudi ya kuishinikiza serikali na mamlaka husika kupunguza makali ya maisha kwa kuondoa kodi kwenye bidhaa na huduma muhimu, huku akionya kuwa serikali itakuwa hatarini kama haitaheshimu matakwa ya umma.
“Utamaduni wa kusubiriana miaka mitano, ni janja yao ya nyani, sasa tumeamua tuwapige mtiti, tunapiga maandamano na mikutano ya nguvu. Tumegundua ukicheka na nyani unavuna mabua. Tumevuna umaskini kwa kuchekacheka na CCM kwa miaka 50. Sasa tunawakomalia hadi kieleweke,” alisema Mbowe na kushangiliwa.
Alisisitiza kuwa CHADEMA inapenda sana amani lakini haiko tayari kuona amani ikitumika kama giza la kukandamiza watu wasidai haki na maslahi yao.
Alibainisha kuwa CCM tayari imeshaonyesha udhaifu wa kisera na kihoja ndio maana imeamua kudandia propaganda za kidini na kikabila ili kujaribu kuigawa na kuidhohofisha CHADEMA, jambo ambalo alisema tayari limeshindwa.
“Tunasema hatutatishwa na propaganda za kutugawa. Walisema CHADEMA ni chama cha Kichaga tukawapiga pembeni, walisema CHADEMA ni cha kidini nayo tumewapiga chini. Mchungaji Msigwa, Sugu, Chiku Abwao, Josephat Nyerere ni Wachagga? Hawana hoja. Hapa tuna Waislamu wengi, kuna Wakristo wengi, lakini tunaunganishwa na dhamira yetu ya kupigania maslahi ya nchi, tusikubali kugawanywa. CCM wanatumia sera ya kikoloni ya wagawe uwatawale, lakini hatutaruhusu hilo litokee. Tutakomaa hadi dakika ya mwisho,” alisema.
Aliwataka wakazi wa Songea kuungana na Watanzania wa mikoa mingine katika kushinikiza kushushwa kwa gharama za maisha na kuhakikisha kunaandikwa katiba mpya.
“Na tunawaambia kule bungeni, CCM wakiendelea kupandisha kodi za mafuta na bidhaa nyingine mbalimbali zinazosababisha maisha yawe magumu, haki ya Mungu nawaambia tutaandamana nchi nzima hadi kieleweke. Na huo ndio ujumbe wangu mkubwa kwenu,” alisema Mbowe na kushangiliwa.
Naye Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Slaa, akiwashukuru wakazi wa Songea kwa kura nyingi walizompa katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana, alisema kwa hali ngumu ya maisha ilivyo na jinsi Watanzania wengi wanavyoichukia CCM, uko uwezekano mkubwa kwa wananchi kumng’oa Kikwete kabla ya mwaka 2015.
Akitoa mfano alisema katika nchi nyingine ya Japan, wananchi wakiona kiongozi wao hatimizi ahadi, matakwa na maslahi yao humuondoa kwa kumpigia kura ya maoni kabla ya muda wake kukamilika.
“Mjadala wa Katiba ya nchi hii ndio mwanzo wa kuwaondoa madarakani, Kikwete asipotimiza matakwa ya umma anaweza kung’oka kabla ya mwaka 2015. Walichakachua kura, lakini hawakujua kwamba tuna watu wengi nyuma yetu,” alisema Dk. Slaa.
Alisema tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka jana, Rais Kikwete hajathubutu kufanya ziara hata moja ya kuwashukuru wananchi kwa sababu anajua fika hana wa kumshukuru kwani alichakachua kura.
“Tungetaka wakati ule tungefanya vurugu kama Ivory Coast lakini nilikataa nikasema sitaki kwenda Ikulu kwa kumwaga damu. Leo mwenzangu tangu uchaguzi umalizike hajaja kushukuru wananchi, anajua hamkumchagua kwa hiyo hana wa kumshukuru. Amshukuru nani wakati alichakachua kura?” alihoji Dk.Slaa na kuacha umati mzima ukimshangilia.
Alisema tangu awe Rais kwa kipindi kingine cha pili, Rais Kikwete amekuwa akifanya ziara za mara kwa mara nje ya nchi hususan Ulaya huku akiweka wazi kuwa mpaka sasa ndani ya kipindi cha miezi sita ameshakwenda nje ya nchi takriban mara 12.
“Badala ya kuja kusikiliza matatizo yenu, yeye kila mwezi anakwenda Ulaya. Jana amekwenda tena Afrika Kusini …kule amewaambia kwamba Tanzania inapambana na umaskini. Hayo mambo alipaswa kuja kuwaeleza ninyi na sio watu wasiomhusu. Kwa mwezi anakwenda nje mara mbili na mpaka sasa ndani ya miezi sita ameenda nje mara 12,” alisema Dk. Slaa na kuongeza.
“Akishindwa kuwapa wananchi elimu bure, tutamwondoa. Akishindwa kutupa nyumba bora za bati, tutamwondoa na akishindwa kushusha bei za bidhaa na huduma mbalimbali ili maisha yawe nafuu, tutamwondoa.
Japan, waziri mkuu akishindwa kutekeleza wanayotaka wanamwondoa. Usalama wake wa Kikwete wa kufika miaka 5 ni kutimiza matakwa ya Watanzania,” alisema Dk. Slaa.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe aliendelea kumtuhumu Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo, kuwa ni waziri wa madeni kwani tangu ateuliwe deni la taifa limekuwa likongezeka hadi kufikia trilioni 16 hivi sasa.
Alisema kwa deni hilo sasa kila Mtanzania anadaiwa wastani wa sh laki tatu.
“Mkulo ni Waziri wa Madeni asijaribu kabisa kushindana na mimi, tangu ameingia nchi yetu imekuwa ikikopa tu. Tunakopa kununua mafuta, tunakopa kununua vipuri, karatasi na tunakopa kulipa watu mishahara. Ndio maana tunasema katika bajeti mbadala tutataka waziri huyu awajibike,” alisema Zitto.
Maandamano ya jana sawa na yale yaliyotangulia katika mikoa mingine yaliongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, Makamu mwenyekiti Said Issa Mohamed na Katibu Mkuu, Dk. Willbrod Slaa, yakianzia nje kidogo ya mji wa Songea katika eneo la Msamala.
Kutoka eneo hilo maandamano hayo yalitembea kwa umbali wa takribani kilometa tano yakipitia barabara kuu inayopita katikati ya mji huu hadi katika viwanja vya shule ya msingi Kibulang’oma kata ya Lizaboni, kulikofanyika mkutano mkubwa wa hadhara.
Maelfu kwa maelfu ya waandamanaji walijitokeza kuunga mkono maandamano hayo huku wakiimba nyimbo mbalimbali za mshikamano na za kukikejeli Chama cha Mapinduzi (CCM), kama “Kama sio juhudi Mafisadi presha inapanda, presha inashuka, CCM tumewashika pabaya.”
Waandamanaji hao pia walibeba mabango yaliyokuwa na ujumbe wa aina mbalimbali kama “Ameshindwa Luteni Makamba sembuse wewe mgambo Mukama, CHADEMA okoa Ruvuma na ufisadi wa mbolea na CCM someni alama za nyakati, Watanzania hatuwataki.”
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment