Sunday, August 7, 2011
NAPE: CCM KUWAREJESHA KWENYE UKWELI VIJANA WALIOPOTOSHWA NA WAPINZANI
NA MWANDISHI WETU
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kitahakikisha katika mabadiliko yake ya sasa kinawarejesha katika kuujua ukweli vijana waliopotoshwa na wapinzani hadi kufikia hatua ya kudhani hakuna mazuri yaliyofanywa tangu uhuru.
Mikakati hiyo ilisemwa jana na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye wakati akizungumza na baadhi ya viongozi na watangazaji wa Clouds Media Group, Mikocheni Dar es Salaam, alipofanya ziara ya kujitambulisha katika wadhifa wake huo na kueleza mabadiliko yaliyofanywa na Chama, mapema Aprili mwaka huu.
Alisema, wakati wapo vijana ambao hawakuipigia kura CCM katika uchaguzi mkuu uliopita kwa sababu zinazoonekana kuwa za msingi, lakini ipo idadi kubwa ya vijana ambao walifanya hivyo kutokana na chuki tu kutokana na kushibishwa na uongo na baadhi ya vyama vya upinzani.
Nape alisema katika miaka ya karibuni hasa baada ya kupevuka kwa kiwango kikubwa mawasiliano kwa njia ya mitandao kwenye kompyuta, baadhi ya vyama hivyo vimetumia na vinaendelea kutumia mawasiliano hayo kueneza uongo kwa njia hiyo na kufanikiwa kuwanasa vijana wengi kwa kuwa ndio wanaopendelea zaidi kutumia mawasiliano hayo ya mtandao.
"Baada ya vyama vya upinzani kujua kwamba vijana wengi wanapenda zaidi upashanaji habari kwa njia ya mitandao kwenye kompyuta, kuliko mikutano ya hadhara na njia nyingine za kawaida, baadhi ya vyama hivi vimetumia sana njia hii kuwajaza uongo vijana", alisema Nape.
"Na kwa sababu uongo ukizidi kuenezwa bila kupingwa huweza kuonekana ndiyo ukweli, baadhi ya vijana wameamini uongo huo, na matokeo yake wamejenga chuki kiasi cha kutoyaamini hata mambo ya maana na ya msingi wanayoambiwa na CCM na serikali yake jambo ambalo ni hatari kwa hatma ya taifa", alisema Nape.
Alisema katika mikakati yake ya sasa CCM itahakikisha inawapa ukweli kupitia njia hiyo ya mawasiliano ya mitandao ya kwenye kompyuta kama 'face book' na kueleza matumaini yake kwamba hatua hiyo itazaa mafanikio kwa kuwa yameanza kuonekana katika hatua za awali ambazo CCM imeanza kufanya.
Nape alisema, CCM inafanya hivyo kwa kuwa bado kina uwezo wa kuongoza huku kukiwa hakuna chama cha upinzani ambacho kinaweza kujitapa kuwa kinaweza kuongoza nchi kwa uhakika ikilinganishwa na hali inayojionyesha katika vyama hivyo hadi sasa.
Alisema, mbali ya kuyaendea makundi ya vijana, CCM pia imejipanga kuyafikia kwa ufanisi zaidi makundi yote, kwa kutumia njia mbadala, ikiwemo kufuatilia kwa karibu maoni ya vyombo vya habari hasa vile vinavyoonekana kuwa makini zaidi katika kutoa habari zake.
Nape aliahidi CCM kutoa ushirikiano mkubwa kwa vyombo vya habari katika kuhakikisha vinapata habari za ukweli, sahihi na kwa wakati kuhusu chama na hata za ndani ya serikali.
"Tunaamini sisi CCM tukifungua masikio yetu vilivyo kwa vyombo vya habari tuyaweza kuongoza nchi kwa usahihi zaidi, kwa sababu ninyi vyombo vya habari ndiyo mliopo mitaani wakati mwingi, hivyo mnaweza kuwa mnayajua mengi kuliko sisi, ni vizuri tukawa tunawasikiliza na kufanyia kazi mnayosema", alisema Nape.
Katika ziara hiyo, Nape alizungumzia kwa kina dhana ya mabadiliko ndani ya Chama na utekelezwaji wake unavyoendelea na baadaye waandishi wa Clouds Media Group walipata fursa ya kuzungumza na kumuuliza maswali yaliyoona yanafaa.
Baadaye Nape akiongozwa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa kampuni hiyo ambayo ni walimiki wa vituo vya Clouds FM, Choice FM na Clouds TV, Ruge Mutahaba alipata fursa ya kutembelea baadhi ya vituo hivyo kuona kazi zinavyofanyika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment