NCHI ZINAZOENDELEA KUPATA BILIONI 100 KUPAMBANA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI.
Benjamin Sawe, MaelezoDodoma
Imeelezwa kuwa nchi zinazoendelea zitapata kiasi cha dola za Marekani bilioni 100 ifikapo mwaka 2020 ili kutekeleza mipango ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi
Akijibu swali Bungeni Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Dkt Terezya Huvisa amesema,Tanzania imeendelea kutetea maslahi ya nchi kwa kuhakikisha kuwa msimamo uliopitishwa na Baraza la Mawaziri kuhusu kuunda mfumo wa dunia ili kusaidia nchi zinazoendelea kupunguza gesi joto.
Alisema Tanzania imetakiwa kuhakikisha nchi zinazoendelea zinashiriki kikamilifu katika mpango wa kimataifa wa hatua muafaka za kitaifa za kupunguza gesi joto ambapo maandalizi ya utekelezaji wa mpango huo yameanza.
Katika majibu yake Dkt.Huvisa alisema kwa sasa Tanzania inaandaa mkakati wa kitaifa pamoja na mpango kazi ili kunufaika na kiasi cha dola 100 zitakazotolewa kwa ajili ya kutekeleza mipango ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Alitumia fursa hiyo kuliarifu Bunge kuwa Tanzania kwa sasa ni Makamu wa Rais wa Afrika wa Mkutano wa Mawaziri wa mazingira ambapo mwaka 2012 Tanzania itakuwa mweneji wa mkutano huo.
HUDUMA YA MAWASILIANO KUENDELEA KUBORESHWA
Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia imesema juhudi za kupeleka huduma za mawasilino katika baadhi ya maeneo nchini zinahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali,Kampuni za simu na wananchi kwa ujumla.
Akijibu swali la msingi liloulizwa na Mbunge wa Lushoto Mheshimiwa Henry Daffa Shikifu Naibu Waziri wa Sayansi na Mawasiliano Mhe Charles Mhangwa alisema jitiada hizo za pamoja zinaendelea chini ya mfuko wa Mawasiliano na katika kipindi cha miaka miwili ijayo maeneo mbalimbali yatafikiwa na huduma hiyo.
Alisema kata ya Mlola na nyingine za jirani tayari zimewekwa kwenye mpango wa kufanyiwa tathmini yakinifu na kampuni ya Airtel kabla ya mwisho wa mwaka 2011. Mheshimiwa Naibu Waziri alisema kampuni ya Vodacom imeahidi kufanya utafiti wa maeneo yaliyotajwa ili kuona uwezekano wa kupanua mtandao wake Wilayani Lushoto ambapo utafiti huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.
Aidha kampuni ya Zantel kwa upande wake imeahidi kupanua mtandao wake kupitia miundombinu ya kampuni nyingine za simu ili kufikisha na kuboresha huduma ya mawasiliano katika maeneo mbalimbali nchini.
No comments:
Post a Comment