Mkurugenzi Mkuu wa EWURA HARUNA MASEBU
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji EWURA imesema kuwa kitendo cha kupanda tena kwa bei ya mafuta nchini kunatokana na ongezeko la bei kwenye soko la dunia na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na thamani ya Dola ya Marekani.
Akitoa ufafanuzi kuhusiana na bei elekezi iliyotangazwa na mamlaka hiyo kuanza kutumika leo kote nchini, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA HARUNA MASEBU amebainisha kuwa katika toleo la bei lilianza kutumika Juni 8 mwaka huu bei za zilishuka kwa asilimia nne nukta tatu kwa Petroli.
Hivi karibuni serikali iliingia kwenye mgogoro na wafanyabiashara wa mafuta nchini baada ya kugomea kuuza bidhaa hiyo wakipinga bei mpya zilizotangazwa na EWURA hali iliyochangia ukosefu wa mafuta katika maeneo mbalimbali nchini.
Baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wametoa maoni yao kuhusiana na kupanda tena kwa bei ya mafuta katika maeneo yote nchini iliyotangazwa jana na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini EWURA.
Wakizungumza katika mahojiano na kituo hiki wakazi hao wamesema kupanda kwa bei mara kwa mara kuendana na soko la dunia kunazorotesha shughuli za kiuchumi kwani mafuta yanatumika katika nyanja mbalimali ikiwemo usafirishaji wa bidhaa na shughuli zingine za kimaendeleo.
Katika hatua nyingine wameiomba EWURA kutofanya kazi kwa shinikizo la wafanyabaishara wa mafuta nchini na badala yake watekeleze wajibu wao kwa kufuata taratibu na kanuzi za mamlaka hiyo.
No comments:
Post a Comment