Friday, July 8, 2011

SPIKA SITTA ATAKA MAAMUZI MAGUMU YA VIONGOZI YAENDANE NA UADILIFU!

Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki SAMUEL SITTA amesema suala la serikali kufanya maamuzi magumu bila kuwepo kwa uadilifu wa viongozi ikiwemo wale wasioingia mikataba ya nchi kwa ajili ya kujipatia kamisheni ya asilimia kumi hakutaleta maana yoyote katika kuliletea taifa maendeleo.


Akizungumza bungeni mjini Dodoma Mheshimiwa SITTA ambaye pia ni Naibu Mkuu wa Shughuli za Serikali Bungeni amesema ndani ya maamuzi magumu lazima kuwe na uadilifu utakaosaidia kuliepusha taifa na uingiaji wa mikataba ya kitoto inayoingiwa kwa ajili ya maslahi ya watu binafsi.


Katika hatua nyingine Spika Mstaafu SITTA ametumia fursa hiyo kuwaonya wanasiasa wanaomwita Baba wa Taifa Mwalimu JULIUS KAMBARAGE NYERERE dikteta waache mara moja kwani yeye ndiye aliyeleta umoja unaowaunganisha Watanzania hadi sasa.


                  HALIMA MDEE AMSHUKIA WAZIRI LUKUVI BUNGENI MJINI DODOMA
 
Mbunge wa Kawe kupitia Chadema HALIMA MDEE amewaomba Mawaziri na viongozi wengine nchini kuacha kufanya kazi kwa kujionesha na badala yake watekeleze majukumu yao ikiwemo kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.


Akichangia Makadirio ya Matumizi ya Ofisi ya Rais Muungano na Mazingira Bungeni Mjini Dodoma Mheshimiwa MDEE amesema kuna kampuni zinajenga hoteli kwenye mifumo ya maji machafu lakini viongozi wenye dhamana hawachukui hatua zozote hali inayoleta usumbufu kwa wananchi.


Wakati huohuo Mbunge huyo wa Kawe ameiomba serikali kumfuatilia kwa kina mkazi wa jijini Dar es Salaam anayeendelea kujenga ndani ya eneo la mto eneo la Kawe Darajani licha ya tume iliyoundwa na Wizara ya Ardhi kumtaka kusitisha ujenzi mara moja.


               WANASIASA WAONYWA KUTOWAKEBEHI WAASISI WA MUUNGANO!
Wanasiasa nchini wameonywa kuacha kuwatukana waasisi wa muungano wa Tanzania, Mahayati Baba wa Taifa Mwalimu JULIUS KAMBARAGE NYERERE na ABEID AMANI KARUME kwani kitendo hicho kinakera na kuzaa chuki miongoni mwa Watanzania.


Naibu Mkuu wa shughuli za serikali bungeni ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki SAMUEL SITTA amesema kuwabeza kwamba walikuwa mbumbumbu na madikiteta ni sawa kuwadharau Watanzania wote.


Akimzunguzia zaidi Mwalimu NYERERE, Mheshimiwa SITTA ameeleza kwamba kiongozi huyo ndiye aliyepigana na kuleta ukombozi wa bara la Afrika na alipinga udikiteta katika mataifa mengine duniani.

No comments:

Post a Comment