Monday, June 27, 2011

ZAIDI YA WATANZANIA 211 WANAOTUHUMIWA KWA DAWA ZA KULEVYA WAFUNGWA NJE YA NCHI!

Zaidi ya Watanzania 211 wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya nje ya Mipaka ya Tanzania wamebainika kuwekwa kizuizini katika nchi mbalimbali ikiwemo China, India, Pakistan pamoja na Iran, huku baadhi yao wakihukumiwa kunyongwa.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Kupiga Vita Madawa ya kulevya Duniani, ambayo kitaifa yamefanyika Jijini Dar es salaam, Makamu wa Rais wa Tanzania, DK. MOHAMMED GHARIB BILAL, amesema tatizo la dawa za kulevya nchini limekuwa likiongezeka mwaka hadi mwaka huku watoto wakiwa katika hatari kubwa zaidi ya kuangukia katika janga hilo.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera, Uratibu na Bunge), STEPHEN WASSIRA, amesema kufuatia Tanzania kutumika kama njia ya kusafirisha dawa ya kulevya kuelekea nchi mbalimbali Duniani hali hiyo imesababisha baadhi ya dawa hizo kubakizwa nchini na kusababisha tatizo hilo kuendelea kuwa kubwa zaidi.
Katika hatua nyingine Kamishina wa Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini, CHRISTOPHER SHEKIONDO, amesema katika kukabiliana na tatizo hilo Tume hiyo imejiwekea mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa Wananchi juu ya madhara yatokanayo na mihadarati na kuongeza huduma za tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya nchini.
Miongoni mwa waathirika wameziomba taasisi mbalimbali nchini kuunga mkono juhudi za mapambano dhidi ya Madawa ya kulevya huku wakiwaasa vijana kujiepuha na makundi yanayojihusisha na matumizi ya dawa hizo. Aidha kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni Miaka hamsini ya uhuru bila dawa za kulevya inawezekana.

No comments:

Post a Comment