Tuesday, April 10, 2012

TAARIFA YA TANZIA KUTOKA CHADEMA.

                                                           

                                                 
                                                                     TAARIFA ZA TANZIA

IDARA ya Sanaa na Utamaduni ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa masikitiko makubwa inatuma salaam za rambirambi na pole kwa Watanzania wote, hususan wasanii kwa kuondokewa na mmoja wa wasanii guli nchini, Steven Charles Kanumba.

Idara ya Sanaa na Utamaduni inatoa salaam hizi ikisamia moja ya imani kubwa za CHADEMA kuwa chama hiki kinaamini katika wananchi kumiliki mali kunawapa uhuru zaidi na kutoa fursa ya kila mtu bila kujali asili na hali yake anaweza kutimiza na kufanikiwa kadiri ya vipaji vyake.

Marehemu Kanumba kupitia kazi zake za usanii wa maigizo na hatimaye filamu alionekana wazi kujibidiisha kufanikiwa kadri ya uwezo wake wote kupitia kipaji chake, huku wakati huo huo akitumia juhudi hizo kuhakikisha wasanii wengine wananufaika na tasnia hiyo.

Daima alikuwa msanii ambaye hakukubali kushindwa na kitu. Alipambana kadri ya uwezo wake wote kama msanii kutimiza wajibu wake ili hatimaye tasnia ya usanii iweze kupata stahili yake katika mchango wa maendeleo kwa taifa na jamii ya Watanzania kwa ujumla.

Watanzania watamkumbuka Kanumba kwa uimara wake katika fani, uthubutu wa kujaribu vile ambavyo wengine walifikiri hawawezi au itawachukua muda mrefu kuvifanya na kufanikiwa.

Kanumba ameacha somo kubwa kwa wasanii na Watanzania wenzake kuwa inawezekana mtu kufanikiwa na kutimiza ndoto zake na hatimaye maendeleo ya jamii pana kupitia kipaji na kujifunza kutoka kwa wengine.

Tunapenda kutoa salaam za pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa Kanumba na Watanzania wote kwa ujumla walioguswa na msiba huu kwa namna moja ama nyingine. Tunawatakia moyo wa subira wakati huu wa majaribu makubwa.

Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya Marehemu Kanumba, Amina.

Fulgence Mapunda (Mwana-Cotide)
Afisa wa Sanaa na Utamaduni-CHADEMA
Aprili 9, 2012

No comments:

Post a Comment