Monday, April 30, 2012

NA MWANDISHI WETU

KATIBU wa NEC, Uchumia na Fedha Mwigulu Nchemba ameahidi kuzungumza na Mbunge wa jimbo la Ukonga, Dar es Salaam, Eugine Mwaiposi kuangalia uwezekano wa kuifanyia ukarabati wa barabara ya Majohe ili iweze kupitika kwa urahisi misimu yote.

Amesema kukarabatiwa kwa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa tano, inaungana na barabara ya Pugu kwenda katika maeneo mbalimbali ya Majohe, kutasaidia shughuli nyingi za kijamii kufanyika kwa urahisi.

Mwigulu alisema hayo, leo wakati akizungumza kwenye mahafali ya Chuo Cha Ualimu cha West Dar es Salaam, kilichopo Majohe Rada, jimboni humo, ambapo aliwatunuku pia vyeti wahitimu 98 wa ualimu daraja la III A.
"Kwa bahati nzuri naijua, kwa kweli si nzuri kupitika hasa nyakati za mvua, nitazungumza na mbunge wa jimbo hili ili tuone uwezekano wa kuifanyia ukarabati ikiwemo kuwekwa lami", alisema.

Alisema pamoja na kumshauri mbunge lakini wakati wa kikao cha bajeti kijacho atakuwa mstari wa mbele kuunga mkono ombi la kujengwa barabara hiyo kupitia bajeti kuu ya serikali.

Mwigulu alitoa majibu hayo kufuatia ombi lililotolewa na mkuu wa chuo hicho, Kenedy Makuza ambaye alisema wakazi wa Majohe na wanafunzi wa chuo chake wamekuwa wakipata taabu kwenda mjini kutokana na ubovu wa barabara hiyo.

Wakisoma risala, wahitimu waliomba utaratibu wa kuruhusu wanafunzi wenye ufaulu wa daraja la VI-27 kujiunga na vyuo vya ualimu uendelee angalau kwa miaka miwili ijayo kwa kuwa ukiondolewa utaratibu huo wengi watashindwa kujinga na vyuo hivyo.

Walisema, wengi wa wanafunzi wamekuwa wakishindwa kupata daraja kubwa katika mitihani ya sekondari kutokana si kwa kkukosa akili kimasomo lakini ni kutokana na mzingira ya shule wanamosoma ambazo walisema nyingi hazina mazingira bora na vifaa vya kusomea kuwawezesha kushinda vizuri.

Katika hotoba yake, Mwigulu aliunga mkono ombi hilo na kuahindi kulipeleka kwenye vikao vya juu vya uongozi wa CCM ili liweze kutolewa maamuzi na serikali.

Pia Mwigulu ameahidi kuisaidia Chuo hicho kwa kukipatia vifaa vya michezo ikiwemo mipira.

Aliwataka wahitimu kwenda kuwa mabalozi bora katika jamii na kutumia uelewa wao kutokana na elimu waliyonayo, kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa chanjo na wa kushiriki kutoa maoni wakati wa mchakato wa kupata amaoni ya wananchi kuelekea uundwaji katiba mpya.

No comments:

Post a Comment