Sunday, January 29, 2012

MGOMBEA WA CHADEMA UZINI KUMKATIA RUFAA MO RAZA!

                                         Freeman Mbowe- Mwenyekiti Chadema Taifa
Ali MBAROUK MSHIMBA mgombea wa Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Jimbo la Uzini kwa tiketi ya chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) atakata rufaa dhidi ya uamuzi wa msimamizi wa uchaguzi juu ya pingamizi dhidi ya uteuzi wa Bwana. Mohammed Raza Hassanali kuwa mgombea wa Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi katika uchaguzi mdogo Jimbo la Uzini utakaofanyika tarehe 12, Februari 2012. Mwanasheria wa CHADEMA Zanzibar yuko katika mchakato wa kuandaa rufaa baada ya kupokea nakala ya uamuzi huo uliofanyika jana tarehe 26 Januari 2012 hivyo maelezo ya rufaa yatatolewa baada ya kuwasilishwa kwa pingamizi husika.


Wakati taratibu za rufaa hiyo zikiendelea timu ya kampeni ya CHADEMA inaendelea na maandalizi ya uzinduzi wa kampeni za chama katika uchaguzi husika. Kwa mujibu wa mpango wa CHADEMA katika uchaguzi husika, Katibu Mkuu Dr Wilbroad Slaa anatarajiwa kuwasili Zanzibar leo tarehe 27 Januari 2011 na kupokewa na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Hamad Mussa Yusuph. Aidha uzinduzi wa kampeni za CHADEMA katika uchaguzi husika unatarajiwa kufanyika kesho kutwa tarehe 29 Januari 2011 ukiongozwa na Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe (Mb). Itakumbukwa kwamba 25 Januari 2011 mgombea wa CHADEMA alimwekea pingamizi Mohammed Raza Hassanali Mohamedali mgombea wa Uwakilishi kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) inakwenda kinyume na Sheria ya uchaguzi namba 11/1984 Kifungu cha 46 (3) (a).


Katika pingamizi hilo ilielezwa kuwa kiapo cha Muombaji na au Mgombea wa Uwakilishi kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeshindwa kukidhi matakwa ya kisheria za viapo kwa sababu hakuna kumbukumbu za nambari katika kuonyesha stakabadhi halali za malipo (Paid in Receipt no) na kwamba mlaji kiapo hakulipa malipo halali kwa mujibu wa Sheria na wala hakuomba nafuu yeyote iwapo uwezo wa malipo hayo hana. Aidha, kiapo hicho cha muombaji kimeliwa kinyume cha sheria za viapo Zanzibar (Laws and Decree) pamoja na kukosa stempu halali na ambapo ni kinyume na matakwa ya sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Namba 11 ya mwaka 1984 pamoja na marekebisho yake, kifungu 46 (3) (a).

Pia kiapo cha Muombaji kimekosa sifa kwa mujibu wa Sheria ya uchaguzi ya Zanzibar namba 11 ya mwaka 1984, (3) (a) ambapo Mlaji kiapo alitakiwa aape mbele ya Hakimu kwa mujibu wa kifungu nilichokitaja kwenye aya hii, badala yake yeye alikula kiapo aidha mbele ya Jaji au amegushi muhuri wa Mahakama Kuu.
Kadhalika mgombea wa CHADEMA aliweka pingamizi kuwa Mlaji kiapo hakuweza kufuata utaratibu wa kisheria ambapo alitakiwa ale kiapo mbele ya Hakimu, na badala yake alikiuka utaratibu huo na kwa vyovyote vile kiapo hicho hakiwezi kukidhi matakwa ya kisheria kwa kuwa kinapingana na Sheria za Viapo na Sheria ya Uchaguzi Zanzibar.

Kutokana na mapingamizi hayo, Ali Mbarouk Mshimba alitaka Msimamizi wa Uchaguzi utengue Uteuzi wa Mohammedraza Hassanali Mohamedali kuwa ni Mgombea halali, na kumuondoa katika orodha ya wagombea wa Uwakilishi Jimbo la Uzini katika uchaguzi mdogo, kwa kuwa hakuweza kutimiza sifa za kuwa mgombea kwa mujibu wa sheria. Katika maamuzi yake, msimamizi wa uchaguzi alikubali hoja za pingamizi kwamba fomu husika imegongwa muhuri tofauti kinyume na mahitaji lakini akatupilia mbali pingamizi kwa maelezo kuwa makosa hayo yamefanywa na mahakama.


Katika maelezo yake ya Rufaa pamoja na hoja kutoka katika sheria za uchaguzi wa Zanzibar na maamuzi mengine yaliyofanyika, mwanasheria wa CHADEMA Zanzibar anatarajiwa pia kufanya rejea kwenye hoja zilizojitokeza wakati wa uamuzi kuhusu rufaa ya aliyekuwa mgombea wa CHADEMA katika Jimbo la Mbeya Vijijini Sambwee Mwalyego Shitambala ambaye alienguliwa katika uchaguzi kwa kile kilichoelezwa kuwa ni upungufu katika kiapo.

Imetolewa na Kurugenzi ya Habari na Uenezi

No comments:

Post a Comment