Wednesday, September 7, 2011

KUNDI LA T-MOTO MORDEN TAARAB HILOOOOO MAFICHONI ZENJI KWA KAMBI!


Baadhi ya Wasanii wa kundi jipya la Tanzania Moto Modern Taarab, wakiwasili kwenye Bandari ya Dar es Salaam jana wakati wakisafiri kuelekea Zanzibar kwa ajili ya kuanza kambi yao ya muda kujiandaa na utambulisho ya kundi hilo unaotarajia kufanyika Septemba 30 mwaka huu jijini Dar.
NA MWANDISHI WETU
KUNDI jipya la taarab lijulikanalo kama T Moto Modern Taarab (T Moto), limeondoka jijini Dar es Salaam jana Jumanne kwenda Zanzibar kwa ajili ya kuanza kambi maalum kujiandaa na utambulisho wao.
Utambulisho wa bendi hiyo inayomilikiwa na Amin Salmin ambaye ni mtoto wa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Salmin Amour (Komandoo) unatarajiwa kufanyika Septemba 30, mwaka huu jijini Dar es Salaam. Akizungumza na mwandishi wa gazti hili, akiwa bandarini jijini jana alipokuwa akiwasindikiza wasanii wa kundi hilo, Amini, alisema kuwa anaamini baada ya vijana wake kurejea Dar es Salaam wakitoka huko, watakuwa wameiva vilivyo kutoa upinzani wa nguvu kwa makundi mengine.


“Vijana wangu ndio wanaondoka kwenda Zanzibar kwa ajili ya kambi ya kujinoa hasa, naamini watakaporejea, watakuwa wameiva kiasi cha kuwawezesha kutoa upinzani wa hali ya juu kwa makundi yanayojiita makongwe katika muziki wa taarab,” alisema Amini. Kwa upande wake, kiongozi wa kundi hilo, Jumanne Ulaya (Vidole vya Biashara) ambaye alikuwa ndiyo injini ya kundi la Jahazi Modern Taarab, alisema: “Tunakwenda Zanzibar kujipanga vizuri tutakapotoka huko, tuweze kutoa upinzani wa kweli kwa makundi mengine. Na pia tumejipanga kuweza kuonyesha uwezo zaidi wa kuandaa muziki huu na hasa ukizingatia kundi letu hili jipya linatumia magita matatu ili kuongeza radha ya muziki, tofauti na makundi mengine yanayotumia magita mawili pekee.
Kiongozi wa kundi hilo, Jumanne Ulaya, akihojiwa na waandishi wa habari kuhusiana na safari hiyo na maandalizi ya kundili hilo, wakati akiwa na wanamuziki wenzake wa kundi hilo katika Bandari ya Dar es Salaam jana.

“Tushatoa nyimbo mbili ni nzuri ambazo tayari zimeshatutangaza, tunakwenda kuongezea nyingine zenye ubora zaidi.” Aidha alisema kuwa tayari kuna nyimbo nyingine walizoanza kuzifanyia mazoezi Dar es Salaam, hivyo wanakwenda kuanza kambi kwa lengo la kuziandaa kwa umakini zaidi na kuzimalizia ili waweze kurekodi mapema na kuwapa raha mashabiki wa muziki huo.


Juu ya wanamuziki wake, alisema: “Jeshi langu limekamilika, nina wasanii wenye vipaji vya hali ya juu ambao wengi wao ni wazoefu waliotoka katika makundi mbalimbali yanayotamba kwa sasa katika muziki huu wa taarab.” Aliyataka makundi yote ya taarab kujipanga hasa kwani ujio wa kundi lao linalojiita ‘Real Madrid’ kutokana na kunasa nyota kutoka makundi kadhaa ya taarab, si wa kitoto, kutokana na kujipanga na mashambulizi ya kila aina.
Wasanii wa kundi hilo, Hassan Ally (kushoto) akipozi na mwenzake, Mrisho Rajab, wakiwa bandarini hapo kabla ya kuanza safari yao kuelekea Zanzibar.

“Ninaye Bi Mwanahawa, huyu wimbo wake nimemuandalia mzuri tu, pia tuna Joha wimbo wake ndiyo tumesharekodi wa kwanza. Jembe langu jingine ni Mrisho Rajab ambaye yeye atatoka na wimbo wa Mchimba Kaburi Sasa Zamu Yake Imefika, pia tuna nyimbo nyingine kama Aliyeniumba Hajakosea na nyinginezo,” alisema.


Kuhusiana na uamuzi wao wa kwenda kujichimbia Zanzibar, alisema: “Tunaenda Zanzibar tuweze kukaa pamoja tofauti na hapa (Dar es Salaam) kila mmoja anakaa kwake hivyo inakuwa vigumu kukusanyana kwa wakati mmoja na kuweza kufanya mazoezi ya ‘Siriasi’.” Miongoni mwa waimbaji wa kundi hilo, Mosi Suleiman aliyetokea Dar Modern Taarab, aliwataka wapenzi wa taarab kukaa mkao wa kula kwani hawaendi Zanzibar kuuza sura bali ni kujifua hasa ili waweze kuyasambaratisha makundi mengine yote ya muziki huo.
                Mhasibu wa kundi hilo, akiwa na msanii chipukizi wa kundi hilo, Hasina Kassim.
Hassan Ally aliyetokea New Zanzibar Modern Taarab, aliwataka waimbaji wa taarab, wakiwamo Mzee Yusuph wa Jahazi na Babu Ayoub wajipange upya kwani kundi lao la T Moto si mchezo. “Babu Ayoub na wengine wakae sawa, nimejipanga kufanya mambo makubwa katika taarab nikiwa na kundi langu jipya la T Moto ambalo litakuwa moto wa kuotea mbali,” kama jina lake lilivyo, alijigamba Ally.


Mbali ya Ulaya, Mosi na Ally, wasanii wengine walioondoka na kundi hilo Jumanne ni Mrisho Rajab, Hasina Kassim, Fadhil Mnara, Rajab Kondo, Mussa Mipango, Moshi Mtambo, Ally Kabula, Khanifa, Asha Mashanja, Sabra, Rahma na wengineo.Bi Mwanahawa, Omari Kisila na wasanii wengine chipukizi watatu, watakuwa ni wenyeji wa wenzao hao kwani tayari walishatangulia mjini Unguja ili kuweka mambo sawa, huku Joha Kassim akitarajiwa kuungana na wenzake leo Jumatano.

No comments:

Post a Comment