Monday, June 13, 2011

TRA KUKUSANYA KODI KWA M PESA


Naibu Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Placidus Luoga akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari wakati wa utambulisho rasmi wa huduma ya malipo ya kodi kupitia Vodacom M-pesa inayotolewa na kampuni ya Vodacom Tanzania, kulia ni Mkurugenzi wa Fedha wa Mamlaka ya mapato Tanzania Saleh Mshoro na kushoto ni Mkuu wa Mauzo wa Vodacom M-Pesa Franklin Bagalla.

Mkuu wa kitengo cha Mahusiano wa kampuni ya Vodacom Tanzania Nector Foya katikati akiwaonyesha Naibu Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Placidus Luoga na Mkuu wa kitengo cha Mauzo Vodacom M-pesa Franklin Bagalla bango litakalotumika kuelimisha umma njia za ulipaji kodi kupitia huduma ya Vodacom M-Pesa wakati wa utambulisho rasmi wa huduma hiyo kwa waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa mauzo wa kitengo cha Vodacom M-Pesa Franklin Bagalla kushoto akitoa maelezo kwa waandishi wa habari njia zinazotumika kulipia kodi kupitia huduma ya M-pesa, katikati ni Naibu Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Placidus Luoga na Mkurugenzi wa Fedha TRA Saleh Mshoro, Kampuni ya Vodacom kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) imetangaza rasmi kuanza kutumika kwa njia hiyo ya M-Pesa kulipia kodi.

Na Mwandishi Wetu
Kampuni ya simu za mkoni ya Vodacom Tanzania kwa kushirikiana na TRA zimetangaza huduma mpya ya ukusanyaji kodi huduma hiyo ni ya njia ya m-pesa inayotolewa na Vodacom Tanzania ambapo walipiaji wa kodi nchini wanaweza kulipia kodi na ada mbalimbali za leseni za udereva kupitia simu zao za mkononi.

Kuanzishwa kwa huduma hiyo ni mwendelezo wa azma na dhamira ya kampuni ya kamuni hiyo katika kubuni huduma bora zenye kuongeza thamani ya simu za mkononi kwa lengo la kuleta mapinduzi katika sekta ya mawasiliano ya simu za mkononi nchini.


Huduma hiyo mpya ya kulipia kodi kwa m-pesa inahusisha malipo ya kodi ya majengo, kodi ya mapato na malipo ya ada mbalimbali za leseni za udereva ambayo ni matokeo ya ushirikiano wa kampuni ya Vodacom na Mamlaka ya Mapato Tanzania – TRA.


“Tunapenda kuwatangazia umma mapinduzi mengine ya aina yake katika huduma ya m-pesa ambapo kuanzia sasa walipaji wa kodi hawatakuwa na sababu ya kuhofia njia rahisi ya kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwani kupitia m-pesa wanaweza kufanya hivyo kwa urahisi, usalama na uhakika zaidi”Alisema Mkuu wa Mauzo wa m-pesa Bw Franklin Bagalla.


Ili mlipa kodi aweze kutumia huduma hiyo atapaswa kuwa mteja wa Vodacom aliyejisajili na huduma ya m-pesa na kisha kuzingatia taratibu za kawaida za kuingia na kutumia mfumo wa m-pesa kwenye simu yake ya mkononi na badae kutumia kodi na nambari za kumbukumbu kulingana na aina ya kodi au ada anayolipa.


Katika kulipia kodi ya majengo mlipa kodi atapaswa kutumia nambari ya biashara (Business Number) 500300, nambari ya biashara kwa ajili ya kulipia kodi ya mapato – Persona Income Tax ni 600400.


Aidha kwa mteja wa TRA anaetaka kulipia ada ya leseni ya lena - Provisional Driving License nambari ya biashara ni 700500, anaelipia ada ya majaribio ya udereva nambari ya biashara ni 700500.


Mfumo huu wa malipo ya kodi kupitia m-pesa umehakikiwa vya kutosha kuhakikisha usalama,usiri na uhakika wa huduma yenye viwango na ubora kwa mlipa kodi hasa kutokana na unyeti wa suala zima la ulipaji wa kodi lilivyo.


Bagalla amesema kampuni ya Vodacom ni kampuni inayojali na kuthamini maendeleo ya Tanzania na watanzania na kwamba kodi ni sehemu muhimu ya mapato kwa ajili ya maendeleo. Miongoni mwa nguzo muhimu katika nyanja ya ukusanyaji kodi ni kuwepo na njia rahisi za ukusanyaji kodi na zenye kutumia gharama nafuu katika ukusanyaji, hivyo basi ni dhahiri m-pesa ni kielelezo cha nguzo hizo.


Huduma ya m-pesa hadi sasa inawateja zaidi ya milioni sita waliosajiliwa ambao kwa siku wastani wa shilingi bilioni tatu hupita katika mfumo huu kwa lengo la kulipia huduma mbalimbali au kutuma fedha miongoni mwa wateja.

No comments:

Post a Comment