Tuesday, June 5, 2012

HIKI NDICHO KILICHOMSIBU MBUNGE OMAR BADWEL!

HATIMAYE Mbunge wa Bahi na Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) Bw.Omary Badwel (43) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma ya kupokea rushwa ya sh.milioni moja.



Mbunge huyo kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) amefikishwa mahakaman hapo jana mbele ya Hakimu Bw.Faisal Kahamba na kusomewa mashitaka na wakili wa serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bi.Janeth Machullya.


Shitaka la kwanza analokabiliwa nalo ni la rushwa ambapo ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Mtuhumiwa huyo akiwa kaama Mbunge wa Jimbo hilo,Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pia mtumishi wa umma,alitenda kosa hilo kati ya Mei 30 hadi Juni 2 mwaka 2012 jijini Dar es Salaam.


Ilidaiwa kuwa kwa mujibu wa sheria ya kupambana na kuzuia Rushwa,alishawishi utolewaji rushwa ya sh.milioni 8 kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani Bi.Sipora Liana ili iwe kishawishi kwa wajumbe wa kamati hiyo kupitia ripoti ya bajeti ya Halmashauri hiyo ya mwaka 2011/12.


Katika shitaka la pili mtuhumiwa huyo alidaiwa kuwa Juni 2 mwaka huu katika Hotel ya Peacock jijini Dar es Salaam alipokea rushwa ya Sh.milioni moja kutoka kwa Bi.Liana ili kushawishi wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kupitisha ripoti ya bajeti ya Halmashauri hiyo ya mwaka 2011/12.


Hata hivyo mtuhumiwa huyo anayetetewa na wakili Bw.Mpare Mpoki alikana kutenda makosa hayo ambapo upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika. Walidai kuwa kutokana na hali hiyo wanaomba tarehe ya shauri hiyo kutajwa kabla ya kumsomea maelezo ya awali mshitakiwa huyo.


Kabla ya kutajwa kwa tarehe hiyo wakili Bw.Mpoki aliomba dhamana kwa mteja wake ambapo upande wa mashitaka haukuwa na pingamizi na ombi hilo. Akitoa vigezo vya dhamana Hakimu Bw.Kahamba alisema mshitakiwa anatakiwa awe na wadhamini wawili watakaosaini hati ya dhamana ya sh.milioni 5 kila mmoja na pia watatakiwa kuwasilisha hati zao za kusafiria.


Mtuhumiwa huyo alirudishwa rumande kutokana na wadhamini hao kushindwa kutimiza vigezo hivyo vya dhamana.Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 18 mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

No comments:

Post a Comment