Thursday, April 26, 2012

TANZANIA INAENDELEA NA MAANDALIZI YA KONGAMANO LA KIMATAIFA KUHUSU UHIFADHI WA MBUGA ZA WANYAMAPORI NA UTALII!

Ningependa kuanza kwa kuwajulisha kuwa Tanzania imejiwekea mkakati wa kukuza utalii kwa njia mbalimbali ikiwemo kujitangaza kwa njia ya utalii wa mikutano.


Itakumbukwa kuwa mwezi Oktoba mwaka jana Tanzania ilichaguliwa kuwa mjumbe katika Baraza la Utendaji (Executive Council) la Shirika la Utalii Duniani – United Nations World Tourism Organisation (UNWTO). Nafasi hiyo ilipatikana wakati wa Mkutano Mkuu wa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO General Assembly) ambao ulifanyika nchini Korea tarehe 14 Oktoba, 2011.

Kwa kuwa Tanzania ni mjumbe katika baraza hilo ambalo hufanya maamuzi inategemewa kuwa mikakati yetu itafanikiwa kwa ufanisi zaidi.


Baadhi ya mafanikio ya mwanzo ni ushawishi tulioufanya wa kuuleta Mkutano wa kimataifa ambao utafanyika nchini mwaka huu. Kama mnavyokumbuka mwishoni mwa mwezi uliopita Wizara ilitoa taarifa kuhusu nchi yetu kuwa mwenyeji wa Kongamano la Kwanza la Afrika kuhusu Uendeshaji, Changamoto na Fursa za Uhifadhi wa Mbuga za Wanyamapori na Maeneo Yaliyohifadhiwa (The 1st Pan-African Conference on Sustainable Tourism Management In National Parks and Protected Areas: Challenges and Opportunities) litakalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) tarehe 15 hadi 19 Oktoba 2012.


Walengwa wakuu wa mkutano huu ni watendaji wakuu wanaosimamia Hifadhi za Taifa na Mapori ya Akiba barani Afrika na wadau wa sekta ya Utalii. Tanzania imepata fursa ya kuwa mwenyeji wa Kongamano hili kutokanana na sifa nzuri na uzoefu ilizo nazo katika kuanzisha na kuendeleza Hifadhi zetu za Taifa.


Leo nimewaita kuwajulisha kuwa, Wizara ya Maliasili na Utalii, pamoja na mambo mengine, imeshaunda Kamati ya Wataalamu kwa ajili ya kuandaa kongamano hilo ambayo itaongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Bw. Ibrahim Mussa. Wajumbe wa kamati hiyo wameteuliwa kutoka Idara ya Misitu na Nyuki, Idara ya Wanyamapori, Idara ya Utalii na Idara ya Mambo ya Kale. Wengine ni kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Kamisheni ya Utalii Zanzibar na Wadau wa Utalii na Uhifadhi.


Kuundwa kwa kamati hiyo kunafuatia kusainiwa kwa mkataba wa maandalizi ya kongamano hilo kulikofanyika Berlin Ujerumani wakati wa maonyesho ya utalii tarehe 9 Machi 2012 kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Shirika la Utalii Duniani (UNWTO). Kwa upande wa Tanzania mkataba huo alisainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bibi Maimuna Tarishi na kwa upande wa Shirika la Utalii Duniani alisaini Katibu Mkuu, Dkt. Caleb Rifai.


Mkataba huo unabainisha majukumu yatakayotekelezwa na Tanzania, UNWTO na yale yatakayotekelezwa kwa pamoja.


Majukumu ya Tanzania ni: • Kuhakikisha usalama wa washiriki; • Kushugulikia masuala ya uhamiaji;
• Kugharamia usafiri wa wataalamu 8 kutoka UNWTO ambao ni sehemu ya sekretalieti watakapokuwa hapa nchini katika muda wote wa Kongamano;  • Kuandaa ukumbi wa kutosha washiriki mia tatu;
• Kutoa ofisi 2 za kufanyia kazi, moja ya secretarieti na nyingine ya kamati ya kuratibu maandalizi hapa nchini. • Kuanda na kuratibu wakarimani watakaotafsiri kongamano hilo kwa lugha 3 ambazo ni Kifaransa, Kihispania na Kiingereza.


Majukumu ya UNWTO ni:- • Kulipia wataalamu wa sekretarieti watakaotoka UNWTO gharama za usafiri wa kuja nchini pamoja na masurufu yao.


Majukumu ya pamoja ni: • Kuandaa ratiba ya kongamano na kuratibu kongamano kwa ujumla. Pia ni kubaini na kuratibu mada zitakazowasiliswa katika kongamano.


Kutokana na uzito wa kongamano hili, wajumbe wa sekretalieti kutoka UNWTO na wale wa hapa nchini watajumuika pamoja na kuanza vikao vyao mapema mwezi Aprili ambapo mkutano wa kwanza utahudhuriwa na Mtendaji Mkuu wa UNWTO, Zoltán Somogyi.

Aidha kamati itakuwa na jukumu la kulitangaza kongamano hili kwani kufanikiwa kwake kutasaidia kukua kwa sekta ya utalii nchini, na kama inavoeleweka utalii wetu kwa kiasi kikubwa unategemea Hifadhi za Taifa.


Katika kongamano hili kila nchi itapewa fursa ya kupendekeza wajumbe wenye sifa za kuhudhuria. Kwa mfano, hapa nchini shughuli za kuratibu na kupendekeza washiriki zitafanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo itapendekeza washiriki kutoka sekta binafsi, sekta za umma, asasi za kiraia na wanazuoni.


Wizara inatoa wito kwa wananchi, wafanyabiashara na wadau wote wa uhifadhi na utalii kujiandaa ipasavyo ili kunufaika na ujio huo wa kimataifa.


Mwisho, nachukua fursa hii kuwahakikishia washiriki wa kongamano hilo kuwa wanatakiwa wafanye maandalizi ya kuja nchini bila kusita maana Tanzania ni nchi ya amani. Pia watapata fursa ya kujifunza kutoka Tanzania maana ni nchi ambayo imetenga robo ya eneo lake kwa ajili ya shughuli za uhifadhi.

Taarifa mbalimbali zitaendelea kutolewa kuhusu maendeleo ya matayarisho ya kongamano hili.


Mhe. Ezekiel M. Maige (MB)


WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII


23 Februari 2012

No comments:

Post a Comment