Thursday, April 26, 2012

TAMKO LA THTU TAWI LA UDOM KUHUSU MAAMUZI YA BARAZA LA CHUO KIKUU CHA DODOMA!


TAMKO LA THTU TAWI LA UDOM KUHUSU MAAMUZI YA BARAZA LA CHUO KIKUU CHA DODOMA KUKATAA KUPOKEA MAJIBU YA KAMATI YA RUFAA YA NIDHAMU YA WAFANYAKAZI


UTANGULIZI


Mwaka 2011 na mwanzoni mwa mwaka 2012, kumekuwa na wimbi la kufukuza kazi wafanyakazi kwa sababu mbalimbali zikiwepo za kinidhamu. Matukio haya ya kufukuza kazi yamekuwa yakikiuka taratibu halali za sheria Na 6, 2004 ya Ajira na Mahusiano Kazini, pamoja na sheria na kanuni nyingine za umma. Tafsiri pekee ambayo imekuwa ikihusishwa na matukio haya ni ulipizaji wa kisasi kwa wafanyakazi hasa wanataaluma kwa kuendesha mikutano endelevu mwanzoni mwa mwaka 2011 ili kutimiziwa madai mbalimbali yaliyokwamishwa na uongozi wa chuo kwa muda mrefu tangu Chuo Kikuu cha Dodoma kianzishwe. Mikutano ambayo ilimalizwa kwa ziara ya Waziri Mkuu Mh. Mizengo Kayanza Peter Pinda kuja kuzungumza na kuahidi kutatua matatizo yao mwishoni mwa mwezi Februari 2011.


Kutokana na baadhi ya wafanyakazi waliofukuzwa kutoridhika na uhalali wa kufukuzwa kwao, baadhi yao waliamua kuchukua hatua za kukata rufaa kwenye vyombo husika vilivyoundwa kwa mujibu wa sheria ili waweze kupata haki zao. Kwa upande wa Chuo Kikuu cha Dodoma, chombo pekee chenye mamlaka ya kupokea na kusikiliza rufaa ni KAMATI YA RUFAA YA NIDHAMU KWA WAFANYAKAZI (Staff Disciplinary Appeal Committee) kwa mujibu wa sheria inayoongoza chuo “University of Dodoma Charter” kanuni 58 (1). Uundwaji wa kamati hii ya rufaa ulikamilika mwishoni mwa mwezi Oktoba 2011. Kabla ya hapo hapakuwa na kamati hiyo ya rufaa tangu chuo kianzishwe. Mnamo tarehe 14/12/2011 kwenye kikao cha Baraza la Chuo, kamati hiyo ilipewa baraka ianze kazi rasmi tarehe 15/12/2011.


Baada ya kamati kuanza kazi, rufaa za wafanyakazi watano (5) waliofukuzwa ambao tayari walishapeleka rufaa zao Baraza la Usuluhishi na Uamuzi (CMA), walikubaliana na uongozi wa Chuo, kupitia mwakilishi wake kurudisha kesi hizo chuoni ili zisikilizwe kwenye Kamati ya Rufaa. Rufaa hizo baada ya kupokelewa zilianza kutafutiwa utaratibu wa kusikilizwa. Kamati hatimae ilipanga na iliwajulisha wa rufani kwa barua na ilifanikiwa kusikiliza rufaa hizo mnamo tarehe 10/02/2012. Kwa maelezo toka kwenye kamati, majibu ya rufaa yatatolewa baada ya kufikishwa kwenye baraza la Chuo ambalo lilifanyika tarehe 30/03/2012 siku ya Ijumaa. Kamati ilitimiza wajibu wake wa kupeleka taarifa ya majibu ili yapewe baraka ndipo yaweze kutolewa kwa wahusika.


Kwa mshangao mkubwa na kwa masikitiko, Baraza la Chuo lilikataa kupokea taarifa ya kamati kwa madai kwamba Menejimenti ya Chuo haikujulishwa kwa maandishi siku ambayo rufaa zilisikilizwa na hivyo mchakato wote haukuwa sahihi. Mbaya zaidi, Baraza liliamuru kamati irudie kusikiliza rufaa hizo upya. Kamati ya utendaji THTU tawi la UDOM inaweka wazi maeneo ambayo Baraza la Chuo Kikuu cha Dodoma hakikuzingatia, na ni kinyume na misingi ya utawala bora.


1. Madai ya kuwa Menejimjenti ya Chuo haikujulishwa siku ya kusikiliza rufaa na hivyo haikuwakilishwa hayana msingi wala ukweli wowote kwani ushahidi unaonesha menejimenti ya chuo iliwakilishwa na maafisa wa chuo wanaotambulika. Waliowakilisha menejimenti wakati wa usikilizaji wa rufaa ni 1. Bi Subira Sawasawa (DHRMA) Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala; 2. Bwana John Kusaja (PAO), Afisa Tawala Mkuu na 3. Bwana Melkiori Sanga (LO) Afisa Sheria wa chuo. Hawa watu walitumwa na nani na kwa maslahi ya nani? Kwa sababu wakati wa mashauri walikuwa wakitetea menejiment kwa kuwauliza maswali warufani.


2. Barua za kuitwa kwenye kamati ya rufaa, ziliandikwa na Afisa wa Sheria, kutoka ofisi ya Makamu Mkuu wa Chuo. Barua hiyo ilitumwa nakala ofisi zifuatazo: Makamu Mkuu wa Chuo na Manaibu zake wote wawili (Taaluma, Utafiti na Ushauri) na (Mpingo, Fedha na utawala), Katibu Baraza la Chuo.


3. Utetezi wa Menejiment ya Chuo Kikuu cha Dodoma, ulisomwa na Mwenyekiti wa kamati, na ulikuwa umewasilishwa kwa maandishi. Je ni nani aliempatia Mwenyekiti wa kamati utetezi huo?


4. Kamati hiyo ililipwa fedha na Chuo Kikuu cha Dodoma. Je ni nani alieidhinisha fedha hizo, na bila kuwa na taarifa? Tunafahamu fika mchakato wa malipo ya fedha za umma, zilitokaje bila kuwa na dokezo la kikao??? Malipo yoyote lazima yapitishwe na Ofisi ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Mipango, Fedha na Utawala


5. Kikao hicho kilifanyika ukumbi wa baraza la chuo, idhini ya matumizi ya ofisi hiyo ilitoka wapi?


6. Kitendo cha agenda kutoka kwenye kamati ya rufaa kutopokelewa na Baraza la Chuo inaleta tafsiri ya kuwa kuna ushawishi wa makusudi ulifanywa na menejimenti ya chuo ili kukwamisha agenda husika kwa sababu zisizoeleweka. Ikumbukwe kwenye hicho kikao cha Baraza la Chuo iliandikwa kwamba ni moja ya agenda. Kama chuo hakikuwa na taarifa iliwekwaje kama ajenda kwenye kikao cha Baraza?


7. Kitendo cha Menejimenti ya Chuo kupeleka malalamiko yake kwenye Baraza kwamba haikutendewa haki ni kuvuruga utaratibu wa kisheria uliopo kihalali kwani Baraza la Chuo lilishakamilisha kazi yake ya kufukuza na halipaswi kwa namna yoyote ile kuingilia kati utaratibu wa rufaa kinyume na utaratibu. Kama Menejimenti inaona haikutendewa haki, kuna vyombo halali vilivyopo kisheria ambapo inaweza kupeleka malalamiko yake na ikatendewa haki mfano CMA.


8. Ifahamike pia kuwa kitendo cha baraza la chuo kuzima hoja kwa makusudi kutoka kwenye kamati ya rufaa ni matumizi mabaya ya Baraza ambalo ni chombo muhimu sana katika taasisi hii ya elimu ya juu kwani si kazi yake kufanya hivyo.


9. Uamuzi wa Baraza la Chuo kuagiza kamati irudie kusikiliza rufaa upya ni kupindisha sheria kwa makusudi kwa maslahi yasiyojulikana na kuwafanya watu wengi kujiuliza maswali kulikoni majibu kutotolewa kwa muda wote huu, kuna nini?


10. Uongozi wa chuo unaposema haukusikilizwa, na Mwenyekiti anakubali. Wakati ripoti husika haijasomwa mbele ya wajumbe, ili tujue kama walisikilizwa au la, huu ni ubababishaji na upotoshaji


11. Ikumbukwe kuna wafanyakazi ambao pia walifukuzwa kazi kwenye kikao cha baraza cha 14 Disemba 2012 bila kusikilizwa, na hoja hii ilipopelekwa kwenye Baraza, alikuwa ni Mwenyekiti huyuhuyu aliesema, wacha maamuzi yafanyike kama haki ipo ipo tu wataipata, wafuate taratibu, aliongeza kazi ya baraza la chuo ni kupokea na kuridhia maamuzi ya vikao vya chini na sio kuanzisha mjadala. Mpaka leo kesi hizo zipo CMA – Dodoma. Leo wanakataa kupokea rufaa, pamoja ya kuwa wamepata fursa ya kusikilizwa (Principle of natural justice). Hili hatulikubali hata kidogo


MSIMAMO WA THTU TAWI LA UDOM


Tunapenda watu wote na umma kwa ujumla ujue msimamo wetu kuhusiana na jambo husika kama ifuatavyo


1. Pamoja na kufahamu fika kwamba wafanyakazi wengi walifukuzwa bila kufuatwa taratibu za kisheria, sisi wafanyakazi wa UDOM, tumeonesha ustaarabu wa kuridhisha kwa kuwashauri wenzetu waliofukuzwa kufuata njia na taratibu za kisheria ya kudai haki zao kwenye vyombo vilivyoundwa kisheria kwa kukata rufaa badala ya kuingia kwenye migomo. Ustaarabu wetu huu unapaswa kutambuliwa na kuthaminiwa


2. Hatuko tayari kuona rufaa inasikilizwa upya kwani kufanya hivyo ni kutengeneza mazingira na desturi (precedence) ya sheria kupindishwa pasipo na sababu yeyote na pia ni tishio kubwa sana kwa misingi ya upatikanaji haki sio tu kwa waliokata rufaa sasa bali hata kwa wafanyakazi wengine waliobaki kwa siku za usoni.


3. Maombi yetu ni kwamba; majibu ya kamati ya rufaa yatolewe mapema iwezekanavyo, kama kuna upande wowote haujaridhika iwe upande wa Mlalamikiwa (Menejimenti ya chuo) au Walalamikaji (wakata rufaa) ni vyema ufuate taratibu zilizopo kupata haki kwani sheria ziko wazi.


4. Kama chama, hili litatupelekea kutangaza mgogoro na uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma na tuko tayari kutetea haki zetu kwa gharama yoyote. Haki itendeke na ionekane imetendeka.


5. Kitendo cha Chuo kukimbilia CMA, pia ni ucheleweshaji wa haki. Kimsingi majibu ya Kamati yatolewe, halafu upande usioridhika na taratibu uende ukaombe shauri lisikilizwe. Ikumbukwe hawa wafanyakazi tangu wafukuzwe ni zaidi ya miezi nane(8)


NIA NA MWELEKO WETU DAIMA NI KUJENGA!

M. S. Nashon

KAIMU MWENYEKITI

THTU- TAWI LA CHUO KIKUU CHA DODOMA

No comments:

Post a Comment