KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibrod Slaa amehitimisha ziara ya siku 10 ya kujenga chama na kukagua uhai wa chama katika mikoa mitano, Tabora, Shinyanga, Simiyu, Geita na Mwanza, ambako katika maeneo mbalimbali alikopita amesimamia vikao vya kiutendaji ambavyo vimelazimika kuchukua maamuzi mazito na muhimu dhidi ya watu waliobainika kuhujumu maendeleo ya wananchi, kukihujumu chama, kuvunja katiba, kanuni na taratibu za CHADEMA.
Moja ya maamuzi hayo mazito ni kuvuliwa kwa uanachama kwa aliyekuwa Diwani wa Kata ya Katoro, Gervas Daudi, kufutwa uongozi wa BAVICHA Geita, kuvuliwa uanachama baadhi ya viongozi na wanachama ambao baada ya kuhojiwa na vikao walibainika pasi na shaka kuwa wamekuwa wakihujumu chama hivyo kukwaza matumaini ya wananchi kwa CHADEMA, kuwa chama mbadala nchini. Watu hao waliovuliwa uanachama watalazimika kusubiri maamuzi zaidi ya Kamati Kuu inayotarajiwa kuketi hivi karibuni, ili kujua hatma yao ndani ya CHADEMA.
Akiwa katika vikao hivyo vilivyofanya maamuzi hayo mazito, Katibu Mkuu Dkt. Slaa alilazimika kutoa kauli kali akisema kuwa chama hakitakubali kulea viongozi wasiowajibika kwa watu, akisisitiza kuwa kama kuna kiongozi yeyote hawezi kuendana na kasi ya mahitaji ya chama hicho katika kuwatumikia watu, anapaswa kupisha mara moja badala ya kukwaza juhudi hizo.
“Viongozi wangu naomba mtambue, chama hiki si mali ya mtu, wala si chama cha viongozi, ni chama cha wananchi, ni chama cha watu, ni chama cha Watanzania. Hiki si chama cha kukaa siku nzima kutatua migogoro, ni chama cha kutafakari suluhisho la matatizo mbalimbali yanayowakabili Watanzania. Chadema ni tumaini pekee la Watanzania kwa sasa.
“Hatutavumilia ufisadi, hatutavumilia uzembe, hatutakubali viongozi wanaojali maslahi yao badala ya wananchi, katika hili CHADEMA tutakuwa wakali kwa yeyote hata kama angekuwa ni katibu mkuu, hatuwezi kujifungia kuzungumzia migogoro inayosababishwa na ubinafsi wa watu badala ya kutumia muda huu kuzungumzia kero na maendeleo ya watu,” amesisitiza Dkt. Slaa katika ziara hiyo.
Katika ziara hiyo iliyoanzia Nzega, mkoani Tabora, Aprili 13 na kumalizikia Jijini Mwanza Aprili 22, 2012, Katibu Mkuu Dkt. Slaa kupitia vikao hivyo vya kimaamuzi amelazimika pia kutoa kauli kali dhidi ya viongozi na wanachama wanaoonekana kukwaza jitihada za CHADEMA katika kuwatumikia watu, akisema kuwa chama hiki ndiyo tumaini pekee lililobaki kwa Watanzania katika harakati za ukombozi wa awamu ya pili, kutafuta mabadiliko ya kimfumo na kiutawala nchini kwa ajili ya maendeleo ya watu.
Wilayani Nzega, kikao cha kiutendaji kiliwavua uongozi aliyekuwa Mwenyekiti wa Jimbo, Tito Onesmo kutokana na kupata nafasi hiyo kinyume cha utaratibu na Katibu Mwenezi, Shaaban Mohamed kwa kosa la kughushi barua. Wote walipewa karipio kali na kutakiwa kuandika barua ya maelezo kwa nini wasichukuliwe hatua kali zaidi. Mohamed baada ya kubanwa na kukosa utetezi wa makosa yake, aliamua kurejesha kadi ya uanachama mbele ya kikao hicho.
Katika Wilaya ya Bariadi, Katibu Mkuu alifutilia mbali kile kilichoitwa uongozi wa Mkoa wa Simiyu kwani kwa taratibu za chama mkoa huo bado haupo, hivyo uchaguzi ulikuwa batili tangu mwanzo.
Viongozi wa Wilaya ya Bariadi waliohusika katika kuitisha uchaguzi huo, akiwemo Mwenyekiti Mwenyekiti wa Wilaya Limbu Ntalima, Katibu wake Elias Maduka Kaselabantu na Mwenyekiti wa Vijana wa Wilaya, Khamis Rajab, na Bwana Kube Kube aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Mkoa, walipewa onyo kali, kuwekwa chini ya uangalizi maalum kwa kipindi cha miezi 12, kuangalia mwenendo wao ndani ya chama, huku pia Kube akitakiwa kuandika barua ndani ya siku 30 kueleza kwa nini alikuwa nyuma ya suala hilo.
Mbali ya kufutilia mbali uongozi huo, kikao hicho kiliwaondoa madarakani viongozi wa wilaya waliochukua madaraka isivyohalali aliyekuwa Mwenyekiti wa Wilaya Limbu Ntalima, Katibu wake Elias Maduka Kaselabantu na Mwenyekiti wa Vijana wa Wilaya, Khamis Rajab kwa kukiuka katiba ya chama na kukihujumu katika uchaguzi mdogo wa kutafuta Diwani wa Kata ya Legangabilili, ambapo CHADEMA ilikuwa ikipewa asilimia kubwa ya kuibuka mshindi.
Viongozi hao waliomba radhi na kuahidi mbele ya kikao kuwa mara moja watakwenda kufuta kesi waliyofungua mahakamani kuhoji uhalali wa Kamati Maalum (task force) iliyoundwa kwa ajili ya kuongoza chama wilayani Bariadi kwa muda.
Katika Wilaya ya Kahama, Baraza la Mashauriano lilikubaliana kwa kauli moja Charles Dotto Lubala, Anastazia Kanyanda na Justine Mganga wavuliwe uanachama, huku wenzao 12 wakiwekwa chini ya uangalizi maalum kwa kosa la kusababisha mgogoro ndani ya chama wilayani humo, hali iliyosababisha chama kushindwa kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi katika maeneo mbalimbali kama vile ngazi ya vitongoji, vijiji na kata ambako wananchi waliichagua CHADEMA kuwatumikia.
Katika Jimbo la Busanda, Mkutano Mkuu wa Jimbo uliamua kwa sauti moja, baada ya kupiga kura, kumuachisha uanachama aliyekuwa Diwani wa Kata ya Katoro, Gervas Daudi, akikabiliwa na tuhuma kadhaa ikiwemo kukihujumu chama hicho. Ngazi husika za chama zitawasilisha taarifa ya maamuzi husika kwa ajili ya uamuzi wa mwisho kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama.
Mbele ya kikao hicho, Daudi alituhumiwa kukihujumu chama hicho kwa kuzuia uongozi wa Serikali ya Kijiji cha Katoro ambayo inaongozwa na Chadema kutekeleza ilani ya chama hicho katika kuwaletea maendeleo wananchi wa eneo hilo, hasa katika kusimamia rasilimali za wanakijiji, huku akishiriki vikao vya kuizushia tuhuma za kutengeneza.
Alituhumiwa kuzuia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa sekondari, kituo cha magari na urekebishaji wa mikataba mibovu ya upangaji wa vibanda vya biashara mali ya kijiji hicho ambayo iliingiwa wakati wa uongozi wa CCM katika Serikali ya Kijiji cha Katoro kabla ya uchaguzi uliokiondoa madarakani chama hicho katika eneo hilo.
Tuhuma zingine ni kuwachangisha fedha wananchi 9 kiasi cha shilingi laki 5 kinyume na taratibu, akiwaahidi kuwatoa waume zao ambao wanashikiliwa mahabusu wakituhumiwa kwa kosa la mauaji, pia alituhumiwa kushiriki vikao na wafanyabiashara, viongozi na wanachama wa CCM wakipanga kuipindua serikali ya kijiji hicho na pia kuwapindua viongozi wengine wa vitongoji wanaotokana na CHADEMA.
Daudi pia amesimamishwa nafasi zake zingine ndani ya chama hicho, ikiwemo Uenezi Jimbo la Busanda, Uenyekiti Wilaya ya Geita, ambapo Kamati Tendaji ya Wilaya ya Geita imeagizwa kukaa haraka kuteua mtu atakayeziba nafasi ya Daudi kisha jina hilo litumwe na kujadiliwa Kamati Kuu ya chama hicho inayotarajiwa kuketi hivi karibuni.
Halikadhalika katika Wilaya ya Geita, Baraza la Mashauriano kwa kauli moja, baada ya kupiga kura lilifikia uamuzi wa kuvuliwa uanachama kwa viongozi wa Baraza la Vijana (BAVICHA); aliyekuwa Mwenyekiti wa BAVICHA Jimbo la Geita, Emmanuel Otto, Katibu wake, Vincent Paul na Mratibu wa Uhamasishaji Philibert Msiba. Pia uongozi mzima wa baraza hilo ngazi ya jimbo uliondolewa. Diwani wa Marceline Simbasana aliandikiwa barua ya karipio kali kwa mwenendo wake kinyume na taratibu za chama.
Baraza la Mashauriano katika Wilaya ya Sengerema liliamua kwa kauli moja kuvunja Baraza la Uongozi la Wilaya, pia uongozi wa Mabaraza yote, yaani BAVICHA, BAWACHA na Baraza la Wazee katika majimbo mawili ya Buchosa na Sengerema ulivunjwa baada ya kuonekana haukidhi mahitaji ya kikatiba, kanuni na taratibu za chama.
Halikadhalika uongozi wa CHADEMA Jimbo la Sengerema wote ulivunjwa, ambapo ilikubaliwa kuwa viongozi wote waliohusika katika kuvunja katiba, kanuni na taratibu katika kusimamia shughuli za chama ikiwemo kuwafukuza wenzao uanachama wasihusike katika mchakato wa kujaza nafasi za uongozi wakati uchaguzi wa kukaimisha na pia katika uchaguzi wa ndani unaotarajiwa kuanza hivi karibuni na kukamilika mwaka 2013.
Katibu Mkuu, Dkt. Slaa amesema kuwa hatarudi nyuma katika kuendesha ‘safisha safisha’ hiyo kwani akiwa Mtendaji Mkuu wa chama anatekeleza azimio la Kamati Kuu iliyoazimia kuwa ofisi yake ifanye uhakiki wa uongozi na utendaji wa chama ili kujenga chama na kukagua uhai wa chama kuanzia ngazi ya chini, Msingi mpaka juu.
Imetolewa leo Aprili 26, 2012, Dar es Salaam na;
Tumaini Makene
Afisa Habari wa CHADEMA
No comments:
Post a Comment