Monday, April 2, 2012

RAIS AFANYA MAZUNGUMZO NA MKURUGENZI MTENDAJI WA BENKI YA AfDB

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, akiomuonesha maendeleo ya ujenzi wa barabara nchini katika ramani ya Tanzania Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Bi. Mary Consolata Muduuli (wa pili kulia) Ikulu, Dar es Salaam, leo Machi 31, 2012. Bi. Muduuli ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa AfDB kwa nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Seychelles, Rwanda, Ethiopia na Eritrea, alifuatana na Mwakilishi wa Benki hiyo katika Tanzania. Bi. Tonia Kandiero ( wa pili kushoto) na mshauri wa Mkurugenzi Mtendaji huyo, Bi. Salma M Salum. Picha na IKULU



                                        TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumamosi, Machi 31, 2012, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Bi. Mary Consolata Muduuli.


Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Bi. Muduuli ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa AfDB kwa nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Seychelles, Rwanda, Ethiopia na Eritrea, alifuatana na Mwakilishi wa Benki hiyo katika Tanzania. Bi. Tonia Kandiero na mshauri wa Mkurugenzi Mtendaji huyo, Bi. Salma M Salum.


Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete ameishukuru AfDB kwa misaada mingi ya maendeleo ambayo Benki hiyo imekuwa inatoka kwa Tanzania, na ameitaka kuendelea kusaidia jitihada za Watanzania kujiletea maendeleo.


Benki hiyo ambayo ilianza shughuli zake katika Tanzania mwaka 1971 hadi mwishoni mwa mwaka jana ilikuwa imeidhinisha miradi 121 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni tatu katika sekta za miundombinu, usafirishaji, kilimo, maji, huduma za kijamii, umememe, viwanda na madini na mawasiliano.

No comments:

Post a Comment