Tuesday, March 6, 2012

RAIS KIKWETE AFUNGAU MKUTANO MKUU WA MWAKA WA MAAFISA WAANDAMIZI WA JESHI LA POLISI LEO MJINI MOSHI!

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwasili Chuo cha Polisi mjini Moshi leo Machi 6, 2012 tayari kwa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi. Kulia kwake ni Waziri wa Mambo ya Ndani Mh Shamsi Vuai Nahodha na kushoto kwake ni Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema.

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUFUNGUA MKUTANO MKUU WA MWAKA WA MAAFISA WAANDAMIZI WA JESHI LA POLISI, CHUO CHA POLISI MOSHI, TAREHE 06 MACHI 2012.

Nataka kuwahakikishia kuwa mimi na viongozi wenzangu Serikalini tunatambua umuhimu wa kuendelea kuliongezea Jeshi la Polisi uwezo wa kibajeti ili liweze kutimiza kwa ufanisi zaidi majukumu yake. IGP ni shahidi kwa kiasi gani tumeendelea kuongeza bajeti ya Jeshi la Polisi mwaka hadi mwaka.


Kwa mfano, mwaka 2005 Bajeti ilikuwa Shilingi 69 bilioni na mwaka huu wa fedha zimetengwa Shilingi 134 bilioni. Nawaahidi kuwa tutaendelea kuongeza fedha kila mwaka katika miaka ijayo. Pia tumetumia uhusiano wetu na nchi rafiki kuomba misaada inayoendelea kuimarisha Jeshi letu kwa zana, mafunzo na weledi.


Napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza Maofisa, Wakaguzi na askari wote kwa kazi kubwa na nzuri muifanyayo katika kulinda maisha na mali za raia. Nawapongeza kwa uchapakazi wenu na moyo wenu wa kujitolea na kujituma. Hakika maudhui ya Kauli Mbiu yenu ya mwaka huu mmekuwa mnayatekeleza kwa vitendo. Matokeo ya jitihada zenu yanaonekana.

Mafanikio ya kutia moyo yanazidi kupatikana na sote tunayashuhudia. Mwenye macho haambiwi tazama. Uhalifu (hususan wa kutumia nguvu) unaendelea kupungua nchini kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma. Kulingana na takwimu za mwaka wa jana makosa makubwa ya jinai yalipungua kutoka 94,390 mwaka 2010 hadi 76,052 mwaka 2011.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi Chuo cha Polisi mjini Moshi leo Machi 6, 2012.

Haya ni mafanikio ya kutia moyo, lakini hamna budi mtambue kuwa bado idadi ya makosa 76,052 ni kubwa mno. Hivyo bado mnayo na tunayo kazi kubwa ya kufanya mbele yenu na yetu. Inatupasa tuongeze juhudi maradufu au hata zaidi ili tupunguze kabisa uhalifu nchini.


Ndugu Makamanda,
Maofisa Waandamizi wa Polisi;


Mheshimiwa Waziri na Inspekta Generali wamezieleza vizuri changamoto zinazolikabili Jeshi la Polisi na mimi sina haja ya kuzirudia. Napenda kutumia nafasi hii kurudia kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kusaidiana nanyi kwa kuwawezesha ili muweze kuzikabili changamoto hizo kwa mafanikio. Tumefanya hivyo miaka iliyopita, tunafanya hivyo hivi sasa na tutafanya hivyo miaka ijayo.

Rais Jakaya Kikwete akizindua mojawapo ya vitabu vya muongozi wa Jeshi la Polisi wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi Chuo cha Polisi mjini Moshi leo Machi 6, 2012 Kulia ni Waziri wa Mambo ya Ndani Mh Shamsi Vuai Nahodha wa kulia Rais ni Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema akifuatiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mh Leonidas Gama.

Tutaendelea kuliwezesha Jeshi la Polisi kifedha ili muweze kutekeleza ipasavyo majukumu yenu. Tutaendelea kuwawezesha muongeze idadi ya askari. Tutawawezesha mpate vyombo vya usafiri, zana na vitendea kazi vya kisasa vya kufanyia kazi za kukabiliana na uhalifu. Kazi ya kulipatia Jeshi la Polisi zana na vifaa vipya vya kazi inaendelea ikiwa ni sehemu ya Programu ya Maboresho ya Jeshi la Polisi. Nawahakikishia kuwa tutaendelea kutoa fedha za kutekeleza Programu hiyo na shughuli nyingine za Jeshi la Polisi.



Tutaendelea kuwawezesha katika kuboresha mafunzo ya askari na maafisa wa Jeshi la Polisi. Natambua mahitaji ya kuviboresha vyuo vilivyopo sasa. Panapohitaji kukarabati pakarabatiwe na panapotakiwa ujenzi wa majengo mapya yajengwe. Na panapotakiwa kuanzishwa chuo kipya kianzishwe.
Sehemu ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi Chuo cha Polisi uliofunguliwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete mjini Moshi leo Machi 6, 2012.
PICHA ZOTE NA IKULU.

Hatuna budi kuwekeza katika mafunzo kwani mafunzo ni msingi mzuri wa weledi na kuwa na askari wenye tabia na mwenendo mwema. Kupata zana za kisasa za upelelezi na kudhibiti uhalifu pekee hazitoshi kama zitakuwa mikononi mwa askari asiyejua kitu, asiyekuwa na nidhamu na utiifu. Kufanya hivyo kunalihakikishia Jeshi uwezo wa kutimiza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa na kuleta sifa kwa Jeshi la Polisi Tanzania.


Dunia imebadilika, Tanzania imebadilika na mbinu za uhalifu na aina za uhalifu yamebadilika. Pia, mbinu, mikakati na maarifa ya kukabiliana na uhalifu, nayo yamebadilika duniani. Lazima tusisitize mafunzo, kwani ndiyo msingi wa weledi na ufanisi. Mafunzo ndiyo njia ya kuwawezesha askari na maofisa wa Jeshi la Polisi kupata elimu na maarifa mapya kuhusu uhalifu na namna ya kukabiliana nao. Mafunzo ndiyo yatakayowezesha kuelewa zana na vifaa vipya vya kupambana na uhalifu na kujua namna ya kuvitumia. Hakuna badala ya mafunzo.

No comments:

Post a Comment