Sunday, December 25, 2011

WAJUMBE WA KAMATI YA TAIFA YA MAAFA YA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZNZ WALIPOMTEMBELEA LUKUVI KUTOA RAMBIRAMBI KUTOKANA NA MAFURIKO!

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) Mhe. William Lukuvi (Mb) akiongea na wajumbe wa Kamati ya Taifa ya Maafa ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar walipofika ofisini kwake Jijini Dar es Salaam leo kwa ajili ya kutoa mkono wa rambi rambi kwa Maafa ya Mafuriko yaliyotokea Jijini Dar es Salaam, wa kwanza Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mh. Mohammed Aboud Mohammed,wa Pili ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Bw. Said Shaban na watatu ni Kamishina wa Zimamoto Zanzibar, Ali Abdallah Malimussy. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) Mh. William Lukuvi (Mb) amekutana na Kamati ya Taifa ya Maafa ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar leo Jijini Dar es Salaam ambao wamemueleza jinsi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itakavyowasaidia waathirika wa maafa ya Mafuriko yaliyotokea Jijini Dar es Salaam kuanzia usiku wa tarehe 19 -20 Desemba, 2011.



Wajumbe wa Kamati ya Taifa ya Maafa ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakiongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mhe. Mohammed Aboud Mohammed ambaye alibainisha kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia kamati hiyo imeamua kuanzisha akaunti maalum itakayo ili wazanzibar wote wenye nia ya kuwasaidia waathirika wa maafa ya mafuriko wachangie kupitia akaunti hiyo.


“Serikali ya Zanzibar kupitia Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais imeamua kufungua akaunti maalumu pale Zanzibar ambayo itakuwa inaratibiwa na Serikali , ili wazanzinar wenye nia ya kuwasaidia waathirika wapitishe michango yao katika akaunti hiyo” alifafanua Aboud.


Aidha Aboud alisisitiza kuwa Serikali yake itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu katika kuhakikisha waathirika wa maafa ya Mafuriko wanakuwa salama na hatimaye wanarudi katika hali zao za kawaida za awali.


Awali Lukuvi aliieleza Kamati ya Taifa ya Maafa ya Zanzibar athari za maafa ya mafuriko kuwa katika mkoa wa Dar es Salaam, wilaya zote na kata zake zote 30 zimeathirika na mafuriko kwa kuaribiwa miundombinu yake ya Barabara, maji na umeme pamoja na makazi ya watu.


“Kutokana na mafuriko yaliyotokea nyumba nyingi zimeathirika kwa kuzingirwa na maji kulikopelekea watu zaidi ya 5000 kukimbia makazi yao, uharibifu mkubwa umefanyika kwa vitu na mali za wakazi hao ambapo hadi kufikia tarehe 22 Desemba,2012 ni wananchi 70 waliotolewa taarifa ya kuwa majeruhi huku wananchi 20 wametolewa taarifa ya kufariki ” alisema Lukuvi.

No comments:

Post a Comment