MAKAMU WA RAIS AIWAKILISHA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA MATAIFA YA TROPIKI YALIYO KATIKA UKANDA WENYE MISITU MIKUBWA NA YENYE KUVUNA MVUA NYINGI: JUNI 03, 2011 JIJINI BRAZZAVILLE, CONCO
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal ameiwakilisha Tanzania katika mkutano tajwa hapo juu uliofanyika katika jiji la Brazzaville, Jamhuri ya Watu wa Kongo ambapo Tanzania ilishiriki kama nchi mwalikwa.
Ujumbe wa Dkt. Bilal uliambatana na Mama Zakhia Bilal, Waziri wa Maliasili na Utalii Ezekiel Maige, Waziri katika Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar; Fatma Fereji na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mahadhi Juma Maalim.
Katika mkutano huo, ujumbe uliosomwa na Dkt. Bilal umebainisha nafasi ya Tanzania katika kushiriki makubaliano mbalimbali ya kimataifa yenye lengo la kuhifadhi mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Pia hotuba ya Makamu wa Rais Dkt. Bilal imefafanua changamoto ambazo Tanzania inakabiliana nazo ikiwa ni nchi yenye misitu mingi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Dkt. Bilal alifika jijini Brazzavile Juni 2, 2011 kisha kuhutubia mkutano huo Juni 03, 2011 majira ya saa 10 mchana ambayo ni sawa na saa 12 jioni kwa saa za Afrika Mashariki. Nchi zinaunda ukanda huu ni zaidi ya 30 ambazo zinapatikana katika mabara ya Afrika, Asia na Amerika ya Kusini. Taarifa zaidi inapatikana katika hotuba ya Makamu wa Rais aliyoitoa katika mkutano huo ambayo imeambatanishwa.
Imeandaliwa na: Boniphace Makene
Mwandishi wa Habari wa Makamu wa Rais
No comments:
Post a Comment