MKOA WA TABORA UNAKABILIWA NA UPUNGUFU WA MAJI CHINI YA ARDHI!
Serikali imeutaja Mkoa wa Tabora kuwa ni miongoni mwa mikoa inayokabiliwa na ukosefu wa maji ya chini ya ardhi jambo linalochangia visima vingi vinavyochimbwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo kutotoa maji au kukauka baada ya kipindi kifupi .
Akijibu swali Bungeni Naibu Waziri wa Maji JERRYSON LWENGE amesema jambo hilo linachangiwa na tatizo la usanifu linaloonesha uwepo wa maji lakini yanapochimbwa hukosekana na kwamba mkakati uliowekwa na serikali ni kutumia maji kutoka Ziwa Victoria.
Katika swali lake la msingi mbunge wa Viti Maalum CUF, MAGDALENA SAKAYA aliiuliza serikali ina mkakati gani ili kuhakikisha visima tisa vilivyochimbwa kutopatikana maji na vile vilivyoonekana vilivyopo vijiji vya uhindini, ushokora na songambele vinaunganishwa ili wananchi wa maeneo hayo waepukane na adha ya hiyo.
WIZARA YA ULINZI YATOLEA UFAFANUZI WALIOACHWA JWTZ ZANZIBAR!
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imetolea ufafanuzi kuhusiana na manung’uniko ya kuachwa kwa baadhi ya vijana kutoka Tanzania Zanzibar ambao walifuzu kujiunga na Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ baada ya kufanyiwa vipimo vya awali visiwani humo.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa DK HUSSEIN MWINYI amesema waombaji wote wanaotaka kujiunga na jeshi wanapimwa mara mbili kwani mafunzo ya jeshi ni magumu na yanahitaji watui wenye afya njema.
DK MWINYI alikuwa akijibu swali la AMINA ANDREW , Mbunge wa Baraza la Wawakilishi CCM Zanzibar aliyeuliza kuhusiana na kitendo cha vijana kutoka Tanzania Zanzibar wanapotaka kujiunga na JWTZ kutakiwa kupimwa tena afya hata kama wamefuzu vipimo vya awali visiwani humo.
BODI YA MAPATO ZNZ KUTHIBITISHWA KUKUSANYA KODI ZA MUUNGANO!
Licha ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kukiri kwamba Bodi ya Mapato Zanzibar ZRB kuwa na uzoefu wa kukusanya kodi visiwani humo kuna haja ya bodi hiyo ithibitishwe kama ina uwezo wa kukusanya kodi za muungano.
Naibu Waziri wa Fedha PEREIRA SILIMA amesema kwa sasa serikali haiwezi kusema lini suala hilo litakamilika kwani ni la kikatiba na kwa sasa lipo katika mchakato wa kukamilishwa ili mpango huo uanze kutumika.
Mbunge wa Mji Mkongwe, Maalim MUHAMMAD IBRAHIM SANYA katika swali lake la nyongeza aliuliza, kwa kuwa ZRB ni chombo chenye uzoefu na watalaam wa kutosha katika kukusanya mapato je serikali itamaliza lini mchakato wake ili chombo hicho kipewe dhamana kamili ya kukusanya mapato yote kwa upande wa Zanzibar.
SERIKALI YAOMBWA KUTOWAWEKA KANDO WANANCHI WALIOKO PEMBEZONI!
Wito umetolewa kwa Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi kutambua kwamba, katika baadhi ya maeneo nchini wananchi wanashindwa kuishi kwa uhuru na amani kutokana na migogoro ya ardhi baina yao na wawekezaji.
Akichangia hoja ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Bungeni mjini Dodoma, PAULINE GETUL Mbunge wa Viti Maalum Chadema amesema hali ilivyo sasa ni Watanzania kuona wanasogezwa pembeni katika rasilimali ya ardhi huku wawekezaji wakipewa kipaumbele.
Katika hatua nyingine amesema ili kuhakikisha suala la amani linaendelea kudumishwa nchini serikali haina budi kulinda haki za msingi za wananchi hususani wale wanaoishi pembezoni.
No comments:
Post a Comment